1 Wakorintho Mlango 12 1st Corinthians

1 Wakorintho 12:1 1stCorinthians 12:1

Basi, ndugu zangu, kwa habari ya karama za roho, sitaki mkose kufahamu.

1 Wakorintho 12:2 1stCorinthians 12:2

Mwajua ya kuwa mlipokuwa watu wa Mataifa, mlichukuliwa kufuata sanamu zisizonena, kama mlivyoongozwa.

1 Wakorintho 12:3 1stCorinthians 12:3

Kwa hiyo nawaarifu, ya kwamba hakuna mtu anenaye katika Roho wa Mungu, kusema, Yesu amelaaniwa; wala hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu.

1 Wakorintho 12:4 1stCorinthians 12:4

Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.

1 Wakorintho 12:5 1stCorinthians 12:5

Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.

1 Wakorintho 12:6 1stCorinthians 12:6

Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.

1 Wakorintho 12:7 1stCorinthians 12:7

Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana.

1 Wakorintho 12:8 1stCorinthians 12:8

Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule;

1 Wakorintho 12:9 1stCorinthians 12:9

mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja;

1 Wakorintho 12:10 1stCorinthians 12:10

na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha;

1 Wakorintho 12:11 1stCorinthians 12:11

lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye.

1 Wakorintho 12:12 1stCorinthians 12:12

Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo.

1 Wakorintho 12:13 1stCorinthians 12:13

Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja.

1 Wakorintho 12:14 1stCorinthians 12:14

Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi.

1 Wakorintho 12:15 1stCorinthians 12:15

Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo?

1 Wakorintho 12:16 1stCorinthians 12:16

Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo?

1 Wakorintho 12:17 1stCorinthians 12:17

Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa?

1 Wakorintho 12:18 1stCorinthians 12:18

Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka.

1 Wakorintho 12:19 1stCorinthians 12:19

Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?

1 Wakorintho 12:20 1stCorinthians 12:20

Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja.

1 Wakorintho 12:21 1stCorinthians 12:21

Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi.

1 Wakorintho 12:22 1stCorinthians 12:22

Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi.

1 Wakorintho 12:23 1stCorinthians 12:23

Na vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa havina heshima, viungo vile twavipa heshima zaidi; na viungo vyetu visivyo na uzuri vina uzuri zaidi sana.

1 Wakorintho 12:24 1stCorinthians 12:24

Kwa maana viungo vyetu vilivyo na uzuri havina uhitaji; bali Mungu ameuungamanisha mwili, na kukipa heshima zaidi kile kiungo kilichopungukiwa;

1 Wakorintho 12:25 1stCorinthians 12:25

ili kusiwe na faraka katika mwili, bali viungo vitunzane kila kiungo na mwenziwe.

1 Wakorintho 12:26 1stCorinthians 12:26

Na kiungo kimoja kikiumia, viungo vyote huumia nacho, na kiungo kimoja kikitukuzwa, viungo vyote hufurahi pamoja nacho.

1 Wakorintho 12:27 1stCorinthians 12:27

Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake.

1 Wakorintho 12:28 1stCorinthians 12:28

Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.

1 Wakorintho 12:29 1stCorinthians 12:29

Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?

1 Wakorintho 12:30 1stCorinthians 12:30

Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?

1 Wakorintho 12:31 1stCorinthians 12:31

Takeni sana karama zilizo kuu. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora.