Yeremia Mlango 20 Jeremiah

Yeremia 20:1 Jeremiah 20:1

Basi Pashuri, mwana wa Imeri, kuhani, aliyekuwa msimamizi mkuu katika nyumba ya Bwana, alimsikia Yeremia alipokuwa akitabiri maneno hayo.

Yeremia 20:2 Jeremiah 20:2

Ndipo Pashuri akampiga Yeremia, nabii, akamtia katika mkatale, uliokuwa pale penye lango la juu la Benyamini, lililokuwa katika nyumba ya Bwana.

Yeremia 20:3 Jeremiah 20:3

Hata ikawa, asubuhi, Pashuri huyo akamtoa Yeremia katika mkatale. Ndipo Yeremia akamwambia, Bwana hakukuita jina lako Pashuri, bali Magor-misabibu.

Yeremia 20:4 Jeremiah 20:4

Maana Bwana asema hivi, Tazama, nitakufanya kuwa hofu kuu kwa nafsi yako, na kwa rafiki zako wote; nao wataanguka kwa upanga wa adui zao, na macho yako yataona hayo; nami nitatia Yuda yote katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atawachukua mateka mpaka Babeli, na kuwaua kwa upanga.

Yeremia 20:5 Jeremiah 20:5

Tena mali zote za mji huu, na mapato yake yote, na vitu vyake vya thamani vyote pia, naam, hazina zote za wafalme wa Yuda, nitavitia katika mikono ya adui zao, watakaowateka nyara, na kuwakamata, na kuwachukua mpaka Babeli.

Yeremia 20:6 Jeremiah 20:6

Na wewe, Pashuri, na watu wote wanaokaa katika nyumba yako, mtakwenda utumwani; nawe utafika Babeli, na huko utakufa, na huko utazikwa, wewe, na rafiki zako wote, uliowatabiria maneno ya uongo.

Yeremia 20:7 Jeremiah 20:7

Ee Bwana, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki.

Yeremia 20:8 Jeremiah 20:8

Maana kila ninenapo napiga kelele, nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la Bwana limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa.

Yeremia 20:9 Jeremiah 20:9

Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.

Yeremia 20:10 Jeremiah 20:10

Maana nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote, wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki, huenda akahadaika, nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake.

Yeremia 20:11 Jeremiah 20:11

Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe.

Yeremia 20:12 Jeremiah 20:12

Lakini, Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.

Yeremia 20:13 Jeremiah 20:13

Mwimbieni Bwana; msifuni Bwana; Kwa maana ameiponya roho ya mhitaji Katika mikono ya watu watendao maovu.

Yeremia 20:14 Jeremiah 20:14

Na ilaaniwe siku niliyozaliwa, isibarikiwe siku ile aliyonizaa mama yangu.

Yeremia 20:15 Jeremiah 20:15

Na alaaniwe mtu yule aliyemletea baba yangu habari, akisema, Umezaliwa mtoto mwanamume; akimfurahisha.

Yeremia 20:16 Jeremiah 20:16

Mtu huyo na awe kama miji ile, ambayo Bwana aliiangamiza, asijute; na asikie kilio asubuhi, na kelele za fujo adhuhuri;

Yeremia 20:17 Jeremiah 20:17

kwa sababu hakuniua nilipotoka tumboni, na hivyo mama yangu angekuwa kaburi langu, na mimba yake sikuzote nzito.

Yeremia 20:18 Jeremiah 20:18

Nalitoka tumboni kwa sababu gani, kuona taabu na huzuni, hata siku zangu ziharibike katika aibu?