Yeremia Mlango 37 Jeremiah

Yeremia 37:1 Jeremiah 37:1

Na Sedekia, mwana wa Yosia, akamiliki badala ya Konia, mwana wa Yehoyakimu, ambaye Nebukadreza amemmilikisha katika nchi ya Yuda.

Yeremia 37:2 Jeremiah 37:2

Lakini yeye, wala watumishi wake, wala watu wa nchi, hawakuyasikiliza maneno ya Bwana aliyonena kwa kinywa cha nabii Yeremia.

Yeremia 37:3 Jeremiah 37:3

Sedekia, mfalme, akamtuma Yehukali, mwana wa Shelemia, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, kwa Yeremia, nabii, kusema, Utuombee sasa kwa Bwana, Mungu wetu.

Yeremia 37:4 Jeremiah 37:4

Basi Yeremia alikuwa akiingia na kutoka kati ya watu; kwa maana walikuwa hawakumfunga gerezani.

Yeremia 37:5 Jeremiah 37:5

Na jeshi la Farao lilikuwa limetoka nchi ya Misri; na Wakaldayo waliohusuru Yerusalemu, waliposikia habari zao, wakavunja kambi yao mbele ya Yerusalemu.

Yeremia 37:6 Jeremiah 37:6

Ndipo neno la Bwana likamjia nabii Yeremia, kusema,

Yeremia 37:7 Jeremiah 37:7

Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mtamwambia hivi mfalme wa Yuda, aliyewatuma kwangu kuniuliza; Angalieni, jeshi la Farao, ambalo linakuja kuwasaidia, litarudi Misri, nchi yao wenyewe.

Yeremia 37:8 Jeremiah 37:8

Na Wakaldayo watakuja tena, na kupigana na mji huu; nao watautwaa, na kuuteketeza.

Yeremia 37:9 Jeremiah 37:9

Bwana asema hivi, Msijidanganye mkisema, Bila shaka Wakaldayo watatuacha na kwenda zao; maana hawatawaacha.

Yeremia 37:10 Jeremiah 37:10

Maana mngelipiga jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki kati yao watu waliojeruhiwa tu, hata hivyo wangeondoka kila mtu katika hema yake, na kuuteketeza mji huu.

Yeremia 37:11 Jeremiah 37:11

Hata ikawa, jeshi la Wakaldayo lilipokuwa limevunja kambi yao mbele ya Yerusalemu, kwa kuliogopa jeshi la Farao,

Yeremia 37:12 Jeremiah 37:12

ndipo Yeremia akatoka Yerusalemu, ili aende mpaka nchi ya Benyamini, alipokee huko fungu lake kati ya watu.

Yeremia 37:13 Jeremiah 37:13

Naye alipokuwa katika lango la Benyamini, akida wa walinzi alikuwapo, jina lake Iriya, mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania; akamkamata Yeremia, nabii, akisema, Unakwenda kujiunga na Wakaldayo.

Yeremia 37:14 Jeremiah 37:14

Ndipo Yeremia akasema, Ni uongo, siendi kujiunga na Wakaldayo; lakini yeye asimsadiki; basi Iriya akamkamata Yeremia, akamleta kwa wakuu.

Yeremia 37:15 Jeremiah 37:15

Nao wakuu wakamkasirikia Yeremia, wakampiga, wakamtia gerezani katika nyumba ya Yonathani, mwandishi; kwa maana ndiyo waliyoifanya kuwa gereza.

Yeremia 37:16 Jeremiah 37:16

Basi, Yeremia alipokuwa ameingia katika nyumba ya shimo, na katika vyumba vya ndani; na Yeremia alipokuwa amekaa humo siku nyingi;

Yeremia 37:17 Jeremiah 37:17

ndipo Sedekia, mfalme, akatuma watu wamlete; naye mfalme akamwuliza kwa siri ndani ya nyumba yake, akasema, Je! Liko neno lililotoka kwa Bwana? Yeremia akasema, Liko. Akasema pia, Utatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli.

Yeremia 37:18 Jeremiah 37:18

Pamoja na haya Yeremia akamwambia mfalme Sedekia, Nimefanya kosa gani juu yako, au juu ya watumishi wako, au juu ya watu hawa, hata mkanitia gerezani?

Yeremia 37:19 Jeremiah 37:19

Wako wapi sasa manabii wenu waliowatabiria, wakisema, Mfalme wa Babeli hatakuja juu yenu, wala juu ya nchi hii?

Yeremia 37:20 Jeremiah 37:20

Na sasa unisikilize, Ee bwana wangu mfalme; maombi yangu yakapate kibali mbele yako; usinirudishe nyumbani mwa Yonathani, mwandishi, nisije nikafa humo.

Yeremia 37:21 Jeremiah 37:21

Ndipo Sedekia mfalme akatoa amri, wakamtia Yeremia katika uwanda wa walinzi; wakampa kila siku mkate mmoja uliotoka katika njia ya waokaji, hata mkate wote wa mji ulipokwisha. Basi Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi.