Yeremia Mlango 38 Jeremiah

Yeremia 38:1 Jeremiah 38:1

Na Shefatia, mwana wa Matani, na Gedalia, mwana wa Pashuri, na Yukali, mwana wa Shelemia, na Pashuri, mwana wa Malkiya, wakayasikia maneno ambayo Yeremia aliwaambia watu wote, kusema,

Yeremia 38:2 Jeremiah 38:2

Bwana asema hivi, Akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; bali yeye atokaye kwenda kwa Wakaldayo ataishi, naye atapewa maisha yake yawe kama nyara, naye ataishi.

Yeremia 38:3 Jeremiah 38:3

Bwana asema hivi, Bila shaka mji huu utatiwa katika mikono ya jeshi la mfalme wa Babeli, naye atautwaa.

Yeremia 38:4 Jeremiah 38:4

Ndipo wakuu wakamwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri, bali shari.

Yeremia 38:5 Jeremiah 38:5

Naye mfalme Sedekia akasema, Tazama, yu mikononi mwenu; maana mfalme siye awezaye kufanya neno lo lote kinyume chenu.

Yeremia 38:6 Jeremiah 38:6

Basi wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo katika uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo.

Yeremia 38:7 Jeremiah 38:7

Basi, Ebedmeleki, Mkushi, towashi, aliyekuwa katika nyumba ya mfalme, aliposikia kama wamemtia Yeremia shimoni; na wakati huo mfalme alikuwa amekaa katika lango la Benyamini;

Yeremia 38:8 Jeremiah 38:8

Ebedmeleki akatoka nyumbani mwa mfalme, akamwambia mfalme, akisema,

Yeremia 38:9 Jeremiah 38:9

Ee bwana wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika mambo yote waliyomtenda Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi atakufa pale alipo, kwa sababu ya njaa; kwa kuwa hapana mkate kabisa katika mji.

Yeremia 38:10 Jeremiah 38:10

Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mkushi, akisema, Chukua pamoja nawe watu thelathini toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla hajafa.

Yeremia 38:11 Jeremiah 38:11

Basi Ebedmeleki akawachukua watu hao pamoja naye, akaingia ndani ya nyumba ya mfalme chini ya ghala, akatoa mle nguo zilizotupwa, na vitambaa vikuukuu, akamtelemshia Yeremia shimoni kwa kamba.

Yeremia 38:12 Jeremiah 38:12

Naye Ebedmeleki, Mkushi, akamwambia Yeremia, Tia nguo hizi zilizotupwa, na vitambaa hivi vikuukuu, chini ya kamba kwapani. Naye Yeremia akafanya hivyo.

Yeremia 38:13 Jeremiah 38:13

Basi wakamwinua Yeremia kwa kamba hizo, wakamtoa shimoni; naye Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi.

Yeremia 38:14 Jeremiah 38:14

Kisha mfalme Sedekia akatuma watu, akamleta nabii Yeremia kwake, ndani ya maingilio ya tatu ya nyumba ya Bwana; mfalme akamwambia Yeremia, Nataka kukuuliza neno, nawe usinifiche neno lo lote.

Yeremia 38:15 Jeremiah 38:15

Basi Yeremia akamwambia Sedekia, Kama nikikufunulia neno hilo, je! Hutaniua wewe? Tena, mimi nikikupa shauri wewe hutanisikiliza.

Yeremia 38:16 Jeremiah 38:16

Basi Sedekia mfalme akamwapia Yeremia kwa siri, akisema, Kama Bwana aishivyo, yeye aliyetufanyia roho zetu, sitakuua, wala sitakutia katika mikono ya watu hao wanaokutafuta wakuue.

Yeremia 38:17 Jeremiah 38:17

Ndipo Yeremia akamwambia Sedekia, Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama ukitoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi nafsi yako utaishi, wala mji huu hautateketezwa; nawe utaishi na nyumba yako;

Yeremia 38:18 Jeremiah 38:18

bali ukikataa kutoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi, mji huu utatiwa katika mikono ya Wakaldayo nao watauteketeza, hata na wewe hutajiepusha na mikono yao.

Yeremia 38:19 Jeremiah 38:19

Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, Nawaogopa Wayahudi waliowakimbilia Wakaldayo, wasije wakanitia katika mikono yao, nao wakanidhihaki.

Yeremia 38:20 Jeremiah 38:20

Lakini Yeremia akasema, La! Hawatakutoa. Nakusihi, uitii sauti ya Bwana katika hayo ninayokuambia; ndivyo itakavyokufaa, na nafsi yako utaishi.

Yeremia 38:21 Jeremiah 38:21

Lakini kama ukikataa kutoka, hili ndilo neno ambalo Bwana amenionyesha;

Yeremia 38:22 Jeremiah 38:22

Tazama, wanawake wote, walioachwa ndani ya nyumba ya mfalme wa Yuda, watatolewa na kuchukuliwa kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, na wanawake hao watasema, Rafiki zako walio karibu wamekudanganya, nao wamekushinda; na kwa kuwa miguu yako imezama matopeni sasa, wamegeuka na kurudi nyuma.

Yeremia 38:23 Jeremiah 38:23

Na watawatoa wake zako, na watoto wako wote, na kuwachukua kwa Wakaldayo; wala wewe hutapona na mikono yao, bali utakamatwa kwa mkono wa mfalme wa Babeli, nawe utakuwa sababu ya kuteketezwa mji huu.

Yeremia 38:24 Jeremiah 38:24

Ndipo Sedekia akamwambia Yeremia, Mtu ye yote asipate habari ya maneno haya, nawe hutakufa.

Yeremia 38:25 Jeremiah 38:25

Lakini kama wakuu wakisikia ya kuwa nimenena nawe, nao wakija kwako, na kukuambia, Tufunulie sasa uliyomwambia mfalme; usimfiche, nasi hatutakuua; na pia uliyoambiwa na mfalme;

Yeremia 38:26 Jeremiah 38:26

basi, utawaambia, Nalimwomba mfalme asinirudishe nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafa humo.

Yeremia 38:27 Jeremiah 38:27

Ndipo wakuu wakamwendea Yeremia, wakamwuliza; naye akawaambia sawasawa na maneno aliyoamriwa na mfalme. Basi wakaacha kunena naye; maana neno lile halikujulikana.

Yeremia 38:28 Jeremiah 38:28

Basi Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi hata siku ile Yerusalemu ulipotwaliwa.