Yeremia Mlango 41 Jeremiah

Yeremia 41:1 Jeremiah 41:1

Basi ikawa katika mwezi wa saba, Ishmaeli, mwana wa Nethania, mwana wa Elishama, mmoja wa wazao wa kifalme, tena ni mmoja wa majemadari wa mfalme, na watu kumi pamoja naye, wakamwendea Gedalia, mwana wa Ahikamu, huko Mizpa; nao walikula chakula pamoja huko Mizpa.

Yeremia 41:2 Jeremiah 41:2

Akaondoka huyo Ishmaeli, mwana wa Nethania, na watu wale kumi waliokuwa pamoja naye, wakampiga Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, kwa upanga, wakamwua; yeye ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa liwali wa nchi.

Yeremia 41:3 Jeremiah 41:3

Tena Ishmaeli akawaua Wayahudi wote waliokuwa pamoja naye, yaani, pamoja na Gedalia, huko Mizpa, na hao Wakaldayo walioonekana huko, yaani, watu wa vita.

Yeremia 41:4 Jeremiah 41:4

Ikawa siku ya pili baada ya kumwua Gedalia, wala hapakuwa na mtu aliyejua habari hii,

Yeremia 41:5 Jeremiah 41:5

wakafika watu kadha wa kadha toka Shekemu, na toka Shilo, na toka Samaria, watu themanini, nao wamenyoa ndevu zao, na kurarua nguo zao, nao wamejikata-kata, wakichukua sadaka na ubani mikononi mwao, ili wazilete nyumbani kwa Bwana.

Yeremia 41:6 Jeremiah 41:6

Na Ishmaeli, mwana wa Nethania, akatoka Mizpa kwenda kuwalaki, akilia alipokuwa akiendelea; ikawa alipokutana nao akawaambia, Njoni kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu.

Yeremia 41:7 Jeremiah 41:7

Basi ikawa walipokuwa katikati ya mji, Ishmaeli, mwana wa Nethania, akawaua, akawatupa katika shimo, yeye na watu wale waliokuwa pamoja naye.

Yeremia 41:8 Jeremiah 41:8

Lakini watu kumi walionekana miongoni mwao, waliomwambia Ishmaeli, Usituue; kwa maana tuna akiba zetu zilizofichwa kondeni, za ngano, na shayiri, na mafuta, na asali. Basi, akawaacha, asiwaue watu hao pamoja na ndugu zao.

Yeremia 41:9 Jeremiah 41:9

Basi, shimo lile, ambalo Ishmaeli ameitupa mizoga ya watu aliowaua, karibu na Gedalia, (ni lile lile alilolichimba Asa, mfalme, kwa kuwa alimwogopa Baasha, mfalme wa Israeli), Ishmaeli, mwana wa Nethania, akalijaza kwa watu wale aliowaua.

Yeremia 41:10 Jeremiah 41:10

Kisha Ishmaeli akawachukua mateka watu wote waliosalia, waliokuwa huko Mizpa, yaani, binti za mfalme, na watu wote waliobaki Mizpa, ambao Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, alikuwa amemkabidhi Gedalia, mwana wa Ahikamu; Ishmaeli, mwana wa Nethania, akawachukua mateka. akaondoka, ili awaendee wana wa Amoni.

Yeremia 41:11 Jeremiah 41:11

Lakini Yohana, mwana wa Karea, na maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, waliposikia habari za hayo mabaya yote aliyoyatenda Ishmaeli, mwana wa Nethania,

Yeremia 41:12 Jeremiah 41:12

wakawatwaa watu wote, wakaenda ili kupigana na Ishmaeli, mwana wa Nethania, nao wakampata karibu na maji makuu ya Gibeoni.

Yeremia 41:13 Jeremiah 41:13

Basi, ikawa, watu wote waliokuwa pamoja na Ishmaeli, walipomwona Yohana, mwana wa Karea, na hao maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, ndipo wakafurahi.

Yeremia 41:14 Jeremiah 41:14

Basi, watu wote, ambao Ishmaeli amewachukua mateka kutoka Mizpa, wakazunguka, wakarudi, wakamwendea Yohana, mwana wa Karea.

Yeremia 41:15 Jeremiah 41:15

Lakini Ishmaeli, mwana wa Nethania, akaokoka pamoja na watu wanane, Yohana asimpate, akawaendea wana wa Amoni.

Yeremia 41:16 Jeremiah 41:16

Ndipo Yohana, mwana wa Karea, na maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, wakawatwaa hao watu wote waliosalia, aliowapata tena katika mikono ya Ishmaeli, mwana wa Nethania, huko Mizpa, baada ya kumwua Gedalia, mwana wa Ahikamu, yaani, watu wa vita, na wanawake na watoto, na matowashi, aliowarudisha toka Gibeoni;

Yeremia 41:17 Jeremiah 41:17

wakaenda zao, wakakaa katika Geruthi Kimhamu, ulio karibu na Bethlehemu, ili wapate kuingia Misri,

Yeremia 41:18 Jeremiah 41:18

kwa sababu ya Wakaldayo; maana waliwaogopa, kwa sababu Ishmaeli, mwana wa Nethania, amemwua Gedalia, mwana wa Ahikamu, ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa liwali juu ya nchi.