Yeremia Mlango 14 Jeremiah

Yeremia 14:1 Jeremiah 14:1

Neno la Bwana lililomjia Yeremia, katika habari ya ukosefu wa mvua.

Yeremia 14:2 Jeremiah 14:2

Yuda huomboleza, Na malango yake yamelegea; Wameketi chini wamevaa kaniki; Na kilio cha Yerusalemu kimepaa juu.

Yeremia 14:3 Jeremiah 14:3

Na wakuu wao huwatuma watoto wao kwenye maji; Nao hufika visimani wasione maji; Hurudi, na vyombo vyao ni vitupu; Wametahayarika na kufadhaika, Na kuvifunika vichwa vyao.

Yeremia 14:4 Jeremiah 14:4

Kwa sababu ya nchi iliyopasuka, Kwa kuwa mvua haikunyesha katika nchi, Wenye kulima wametahayarika, Na kuvifunika vichwa vyao.

Yeremia 14:5 Jeremiah 14:5

Naam, kulungu naye uwandani amezaa, Akamwacha mwanawe kwa kuwa hapana majani.

Yeremia 14:6 Jeremiah 14:6

Na punda-mwitu husimama juu ya vilele vya milima, Hutwetea pumzi kama mbwa-mwitu; Macho yao hayaoni sawasawa, Kwa kuwa hapana majani.

Yeremia 14:7 Jeremiah 14:7

Ijapokuwa maovu yetu yanatushuhudia, lakini utende wewe kwa ajili ya jina lako, Ee Bwana, maana kurudi nyuma kwetu ni kwingi; tumekutenda dhambi.

Yeremia 14:8 Jeremiah 14:8

Wewe uliye tumaini la Israeli, wewe uliye Mwokozi wake wakati wa taabu, kwa nini wewe umekuwa kama mtu akaaye katika nchi, hali ya mgeni, na kama mtu mwenye kusafiri, ageukaye upande ili kukaa usiku mmoja tu?

Yeremia 14:9 Jeremiah 14:9

Kwa nini wewe umekuwa kama mtu aliyesituka, kama shujaa asiyeweza kuokoa? Lakini wewe, Bwana, u katikati yetu, nasi tunaitwa kwa jina lako; usituache.

Yeremia 14:10 Jeremiah 14:10

Bwana awaambia watu hawa hivi, Hivyo ndivyo walivyopenda kutanga-tanga; hawakuizuia miguu yao; basi, Bwana hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, atawapatiliza dhambi zao.

Yeremia 14:11 Jeremiah 14:11

Naye Bwana akaniambia, Usiwaombee watu hawa wapate heri.

Yeremia 14:12 Jeremiah 14:12

Wafungapo, mimi sitasikia kilio chao; na watoapo sadaka za kuteketezwa na sadaka ya unga, sitazitakabali; bali nitawaangamiza kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni.

Yeremia 14:13 Jeremiah 14:13

Ndipo nikasema, Aa, Bwana, MUNGU! Tazama, manabii huwaambia, Hamtauona upanga, wala hamtakuwa na njaa; bali nitawapa amani iliyo thabiti mahali hapa.

Yeremia 14:14 Jeremiah 14:14

Ndipo Bwana akaniambia, Hao manabii wanatabiri uongo kwa jina langu mimi; mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao; wanawapeni unabii wa maono ya uongo, na uaguzi, na neno la ubatili, na hadaa ya mioyo yao.

Yeremia 14:15 Jeremiah 14:15

Basi, kwa hiyo Bwana asema hivi, Kwa habari za manabii wanaotabiri kwa jina langu, wala mimi sikuwatuma, lakini husema, Upanga na njaa havitaingia katika nchi hii; Kwa upanga na njaa manabii hao wataangamizwa.

Yeremia 14:16 Jeremiah 14:16

Na watu hao, waliopewa unabii na wao, watatupwa nje katika njia kuu za Yerusalemu kwa sababu ya upanga na njaa; wala hawatakuwa na mtu wa kuwazika, wao na wake zao, na wana wao, na binti zao; maana nitamwaga uovu wao wenyewe juu yao.

Yeremia 14:17 Jeremiah 14:17

Nawe utawaambia neno hili, Macho yangu na yatiririke machozi, usiku na mchana, wala yasikome; kwa maana bikira, binti ya watu wangu, amevunjika mavunjiko makuu, kwa jeraha isiyoponyeka.

Yeremia 14:18 Jeremiah 14:18

Nikitoka kwenda shambani, tazama, wako huko waliouawa kwa upanga! Na nikiingia mjini, tazama, wamo humo wanaougua kwa sababu ya njaa! Maana nabii na kuhani, wote wawili, huenda huko na huko katika nchi, wala hawana maarifa.

Yeremia 14:19 Jeremiah 14:19

Je! Umemkataa Yuda kabisa? Roho yako imeichukia Sayuni? Mbona umetupiga, tusiwe na dawa ya kutuponya? Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yo yote, tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu!

Yeremia 14:20 Jeremiah 14:20

Ee Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi.

Yeremia 14:21 Jeremiah 14:21

Usituchukie, kwa ajili ya jina lako; usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako, kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi.

Yeremia 14:22 Jeremiah 14:22

Je! Katika vitu vya ubatili vya mataifa, kiko kitu kiwezacho kuleta mvua? Je! Mbingu zaweza kutoa manyunyu? Je! Si wewe, Ee Bwana, Mungu wetu? Kwa sababu hiyo tutakungoja; kwa kuwa wewe umevifanya vitu hivi vyote.