Yeremia Mlango 35 Jeremiah

Yeremia 35:1 Jeremiah 35:1

Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, katika siku za Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, kusema,

Yeremia 35:2 Jeremiah 35:2

Enenda nyumbani kwa Warekabi, ukanene nao, ukawalete nyumbani kwa Bwana, katika chumba kimoja, ukawape divai wanywe.

Yeremia 35:3 Jeremiah 35:3

Basi nikamtwaa Yaazania, mwana wa Yeremia, mwana wa Habasinia, na ndugu zake, na wanawe wote, na nyumba yote ya Warekabi;

Yeremia 35:4 Jeremiah 35:4

nikawaleta ndani ya nyumba ya Bwana, ndani ya chumba cha wana wa Hanani, mwana wa Igdalia, mtu wa Mungu, kilichokuwa karibu na chumba cha wakuu, nacho kilikuwa juu ya chumba cha Maaseya, mwana wa Shalumu, bawabu;

Yeremia 35:5 Jeremiah 35:5

nikaweka mabakuli yaliyojaa divai, na vikombe, mbele ya wana wa nyumba ya Warekabi, nikawaambia, Nyweni divai.

Yeremia 35:6 Jeremiah 35:6

Lakini wakasema, Hatutakunywa divai; kwa maana Yonadabu, mwana wa Rekabu, baba yetu, alituamuru, akisema, Msinywe divai, ninyi wala wana wenu, hata milele;

Yeremia 35:7 Jeremiah 35:7

wala msijenge nyumba, wala msipande mbegu, wala msipande mizabibu, wala msiwe nayo; bali siku zenu zote mtakaa katika hema; mpate kuishi siku nyingi katika nchi ambayo mtakaa ndani yake hali ya wageni.

Yeremia 35:8 Jeremiah 35:8

Nasi tumeitii sauti ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, baba yetu, katika yote aliyotuamuru, kwamba tusinywe divai siku zetu zote, sisi, na wake zetu, na wana wetu, na binti zetu;

Yeremia 35:9 Jeremiah 35:9

wala tusijijengee nyumba za kukaa; wala hatuna shamba la mizabibu, wala konde, wala mbegu;

Yeremia 35:10 Jeremiah 35:10

bali tumekaa katika hema, nasi tumetii; tukafanya sawasawa na yote aliyotuamuru Yonadabu, baba yetu.

Yeremia 35:11 Jeremiah 35:11

Lakini ikawa, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alipopanda akaingia nchi hii, ndipo tukasema, Haya! Twende Yerusalemu, tukiliogopa jeshi la Wakaldayo, na tukiliogopa jeshi la Washami; basi hivyo tunakaa Yerusalemu.

Yeremia 35:12 Jeremiah 35:12

Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,

Yeremia 35:13 Jeremiah 35:13

Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Enenda ukawaambie wana wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, Je! Hamtaki kupokea mafundisho, myasikilize maneno yangu? Asema Bwana.

Yeremia 35:14 Jeremiah 35:14

Maneno ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, aliyowaamuru wanawe, kwamba wasinywe divai, yametimizwa, na hata leo hawanywi; maana waitii hiyo amri ya baba yao; lakini mimi nimesema nanyi, nikiamka mapema na kunena, bali ninyi hamkunisikiliza mimi.

Yeremia 35:15 Jeremiah 35:15

Pia naliwapeleka watumishi wangu wote, manabii, kwenu ninyi, nikiamka mapema na kuwapeleka, nikisema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu, wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia, nanyi mtakaa katika nchi hii, niliyowapa ninyi na baba zenu; lakini hamkutega masikio yenu, wala hamkunisikiliza.

Yeremia 35:16 Jeremiah 35:16

Basi, kwa kuwa wana wa Yonadabu, mwana wa Rekabu, wameitimiza amri ya baba yao aliyowaamuru, lakini watu hawa hawakunisikiliza mimi;

Yeremia 35:17 Jeremiah 35:17

kwa sababu hiyo, asema Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli; Tazama nitaleta juu ya Yuda, na juu ya wenyeji wote wa Yerusalemu, mabaya yote niliyoyatamka juu yao; kwa sababu nimesema nao, wasinisikilize; nimewaita, wala hawakuniitikia.

Yeremia 35:18 Jeremiah 35:18

Naye Yeremia akawaambia watu wa nyumba ya Warekabi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa sababu mmeitii amri ya Yonadabu, baba yenu, na kuyashika maagizo yake yote, na kutenda sawasawa na yote aliyowaamuru;

Yeremia 35:19 Jeremiah 35:19

basi, kwa sababu hiyo, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Yonadabu, mwana wa Rekabu, hatakosa kuwa na mtu wa kusimama mbele zangu hata milele.