Yeremia Mlango 51 Jeremiah

Yeremia 51:1 Jeremiah 51:1

Bwana asema hivi, Angalia, nitaamsha juu ya Babeli, na juu yao wakaao Leb-kamai upepo uharibuo.

Yeremia 51:2 Jeremiah 51:2

Nami nitapeleka wageni mpaka Babeli, watakaompepea; nao wataifanya nchi yake kuwa tupu; kwa kuwa katika siku ya taabu watakuwa juu yake pande zote.

Yeremia 51:3 Jeremiah 51:3

Juu yake apindaye upinde, mwenye upinde na apinde upinde wake, na juu yake ajiinuaye katika dirii yake; msiwaachilie vijana wake; liangamizeni jeshi lake lote.

Yeremia 51:4 Jeremiah 51:4

Nao wataanguka, hali ya kuuawa, katika nchi ya Wakaldayo, hali ya kutumbuliwa katika njia kuu zake.

Yeremia 51:5 Jeremiah 51:5

Kwa maana Israeli, wala Yuda, hakuachwa na Mungu wake, Bwana wa majeshi; ijapokuwa nchi yao imejaa hatia juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.

Yeremia 51:6 Jeremiah 51:6

Kimbieni kutoka kati ya Babeli, kila mtu na ajiokoe nafsi yake; msikatiliwe mbali katika uovu wake; maana ni wakati wa kisasi cha Bwana, atamlipa malipo.

Yeremia 51:7 Jeremiah 51:7

Babeli umekuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa Bwana; kilicholevya dunia yote; mataifa wamekunywa mvinyo wake; kwa sababu hiyo mataifa wameingiwa na wazimu.

Yeremia 51:8 Jeremiah 51:8

Babeli umeanguka na kuangamia ghafula; mpigieni yowe; twaeni zeri kwa maumivu yake; ili labda apate kuponywa.

Yeremia 51:9 Jeremiah 51:9

Tungependa kuuponya Babeli, Lakini haukuponyeka; Mwacheni, nasi twendeni zetu, Kila mtu hata nchi yake mwenyewe; Maana hukumu yake inafika hata mbinguni, Nayo imeinuliwa kufikilia mawinguni.

Yeremia 51:10 Jeremiah 51:10

Bwana ameitokeza haki yetu; Njoni, tutangaze katika Sayuni Habari za kazi ya Bwana, Mungu wetu.

Yeremia 51:11 Jeremiah 51:11

Inoeni hiyo mishale; zishikeni ngao kwa nguvu; Bwana ameziamsha roho za wafalme wa Wamedi; kwa sababu shauri lake ni juu ya Babeli auangamize; maana ni kisasi cha Bwana, kisasi cha hekalu lake.

Yeremia 51:12 Jeremiah 51:12

Twekeni bendera juu ya kuta za Babeli, yatieni malindo nguvu, wawekeni walinzi, tengenezeni waviziao; kwa maana Bwana ameazimia na kutenda yote aliyoyasema juu yao wakaao Babeli.

Yeremia 51:13 Jeremiah 51:13

Ewe ukaaye juu ya maji mengi, uliye na hazina nyingi, mwisho wako umewadia, kadiri ya tamaa zako.

Yeremia 51:14 Jeremiah 51:14

Bwana wa majeshi ameapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika nitakujaza watu, kama nzige, nao watapiga kelele juu yako.

Yeremia 51:15 Jeremiah 51:15

Ameiumba dunia kwa uweza wake, Ameuthibitisha ulimwengu kwa hekima yake, Na kwa ufahamu wake amezitandika mbingu.

Yeremia 51:16 Jeremiah 51:16

Atoapo sauti yake pana mshindo wa maji mbinguni, Naye hupandisha mawingu toka ncha za nchi; Huifanyia mvua umeme, Huutoa upepo katika hazina zake.

Yeremia 51:17 Jeremiah 51:17

Kila mtu amekuwa kama mnyama, hana maarifa; Kila mfua dhahabu amefedheheshwa na sanamu yake ya kuchonga; Maana sanamu yake ya kuyeyuka ni uongo, Wala hamna pumzi ndani yake.

Yeremia 51:18 Jeremiah 51:18

Ni ubatili tu, ni kazi za udanganyifu; Wakati wa kujiliwa kwao watapotea.

Yeremia 51:19 Jeremiah 51:19

Yeye, Fungu la Yakobo, siye kama hawa; Maana ndiye aliyeviumba vitu vyote; Na Israeli ni kabila ya urithi wake; Bwana wa majeshi ndilo jina lake.

Yeremia 51:20 Jeremiah 51:20

Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme;

Yeremia 51:21 Jeremiah 51:21

na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;

Yeremia 51:22 Jeremiah 51:22

na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke;

Yeremia 51:23 Jeremiah 51:23

na kwa wewe nitamvunja-vunja mchungaji na kundi lake; na kwa wewe nitamvunja-vunja mkulima na jozi yake ya ng'ombe; na kwa wewe nitawavunja-vunja maliwali na maakida.

Yeremia 51:24 Jeremiah 51:24

Nami nitamlipa Babeli, na wote wakaao ndani ya Ukaldayo, mabaya yao yote, waliyoyatenda katika Sayuni mbele ya macho yenu, asema Bwana.

Yeremia 51:25 Jeremiah 51:25

Tazama, mimi ni juu yako, Ee mlima uharibuo, asema Bwana; wewe uiharibuye dunia nzima; nami nitaunyosha mkono wangu juu yako, na kukufingirisha chini toka majabalini; nami nitakufanya kuwa mlima ulioteketezwa.

Yeremia 51:26 Jeremiah 51:26

Wala hawatatwaa kwako jiwe moja liwe la pembeni, wala jiwe moja liwe msingi; bali wewe utakuwa ukiwa daima, asema Bwana.

Yeremia 51:27 Jeremiah 51:27

Itwekeni bendera katika nchi, pigeni tarumbeta kati ya mataifa, yawekeni mataifa tayari juu yake; ziiteni juu yake falme za Ararati, na Mini, na Ashkenazi; agizeni jemadari juu yake; wapandisheni farasi, kama tunutu.

Yeremia 51:28 Jeremiah 51:28

Wekeni mataifa tayari juu yake, wafalme wa Wamedi, na maliwali wake, na maakida wake, na nchi yote ya mamlaka yake.

Yeremia 51:29 Jeremiah 51:29

Nayo nchi yatetemeka, nayo ina utungu; maana makusudi ya Bwana juu ya Babeli yasimama, kuifanya nchi ya Babeli ukiwa, isikaliwe na mtu.

Yeremia 51:30 Jeremiah 51:30

Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana; Wanakaa katika ngome zao; Ushujaa wao umewapungukia; Wamekuwa kama wanawake; Makao yake yameteketea; Makomeo yake yamevunjika.

Yeremia 51:31 Jeremiah 51:31

Tarishi mmoja atapiga mbio kumlaki mwingine, Na mjumbe mmoja atapiga mbio kumlaki mwenziwe, Ili kumpasha habari mfalme wa Babeli, Ya kuwa mji wake umetwaliwa kila upande.

Yeremia 51:32 Jeremiah 51:32

Navyo vivuko vimeshambuliwa, Nayo makangaga wameyatia moto, Nao watu wa vita wameingiwa na hofu.

Yeremia 51:33 Jeremiah 51:33

Kwa maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi; Binti Babeli amekuwa kama sakafu ya kufikichia wakati wa kukanyagwa kwake; bado kitambo kidogo na wakati wa mavuno utafika kwake.

Yeremia 51:34 Jeremiah 51:34

Nebukadreza, mfalme wa Babeli, amenila, ameniseta, amenifanya kuwa chombo kitupu; amenimeza kama joka, amelijaza tumbo lake vitu vyangu vya anasa; amenitupa

Yeremia 51:35 Jeremiah 51:35

Udhalimu niliotendwa mimi, na uliotendwa mwili wangu, umpate Babeli; ndivyo atakavyosema yeye akaaye Sayuni; na Yerusalemu atasema, Damu yangu na iwe juu yao wakaao katika Ukaldayo.

Yeremia 51:36 Jeremiah 51:36

Basi, Bwana asema hivi, Tazama, nitakutetea, nami nitatwaa kisasi kwa ajili yako; nami nitaikausha bahari yake, nitaifanya chemchemi yake kuwa pakavu.

Yeremia 51:37 Jeremiah 51:37

Na Babeli utakuwa magofu, makao ya mbwa-mwitu, ajabu, na mazomeo, pasipo mtu wa kukaa huko.

Yeremia 51:38 Jeremiah 51:38

Watanguruma pamoja kama wana-simba; watanguruma kama simba wachanga.

Yeremia 51:39 Jeremiah 51:39

Wakiingiwa na ukali, nitawafanyizia karamu yao, nami nitawalevya, wapate kufurahi, na kulala usingizi wa milele, wasiamke tena, asema Bwana.

Yeremia 51:40 Jeremiah 51:40

Nitawatelemsha kama wana-kondoo machinjoni, kama kondoo waume pamoja na mabeberu.

Yeremia 51:41 Jeremiah 51:41

Jinsi Sheshaki alivyotwaliwa! Naye sifa ya dunia yote alivyoshambuliwa! Jinsi Babeli alivyokuwa ukiwa katikati ya mataifa.

Yeremia 51:42 Jeremiah 51:42

Bahari imefika juu ya Babeli, Umefunikwa kwa wingi wa mawimbi yake.

Yeremia 51:43 Jeremiah 51:43

Miji yake imekuwa maganjo; Nchi ya ukame, na jangwa; Nchi asimokaa mtu ye yote, Wala hapiti mwanadamu huko.

Yeremia 51:44 Jeremiah 51:44

Nami nitafanya hukumu juu ya Beli katika Babeli, nami nitavitoa katika kinywa chake alivyovimeza; wala mataifa hawatamwendea tena; naam, ukuta wa Babeli utaanguka.

Yeremia 51:45 Jeremiah 51:45

Enyi watu wangu; tokeni katikati yake, mkajiokoe nafsi zenu na hasira kali ya Bwana, kila mmoja wenu.

Yeremia 51:46 Jeremiah 51:46

Wala isizimie mioyo yenu, wala msiiogope habari itakayosikiwa katika nchi; maana habari itakuja mwaka mmoja, na baadaye mwaka wa pili habari itakuja, na udhalimu katika nchi, mwenye kutawala akishindana na mwenye kutawala.

Yeremia 51:47 Jeremiah 51:47

Basi angalia, siku zitakuja, ambazo katika siku hizo, nitafanya hukumu juu ya sanamu za Babeli, na nchi yake yote itatahayarika; na watu wake wote waliouawa wataanguka katikati yake.

Yeremia 51:48 Jeremiah 51:48

Ndipo mbingu, na nchi, na vitu vyote vilivyomo, vitaimba kwa furaha juu ya Babeli; kwa maana watu waangamizao watamjilia kutoka kaskazini, asema Bwana.

Yeremia 51:49 Jeremiah 51:49

Kama vile Babeli alivyowaangusha watu wa Israeli waliouawa, ndivyo watakavyoanguka katika Babeli watu wa nchi yake nzima waliouawa.

Yeremia 51:50 Jeremiah 51:50

Ninyi mliojiepusha na upanga, Enendeni zenu, msisimame; Mkumbukeni Bwana tokea mbali, Na Yerusalemu ukatiwe mioyoni mwenu.

Yeremia 51:51 Jeremiah 51:51

Twaona haya kwa kuwa tumesikia mashutumu; Fedheha imetufunikiza nyuso zetu; Kwa sababu wageni wamepaingia Patakatifu pa nyumba ya Bwana.

Yeremia 51:52 Jeremiah 51:52

Kwa sababu hiyo siku zinakuja, asema Bwana, nitakapozihukumu sanamu zake; na katika nchi yake yote waliojeruhiwa wataugua.

Yeremia 51:53 Jeremiah 51:53

Babeli ujapopanda mbinguni, na ujapopafanya mahali pa juu penye nguvu zake kuwa ngome, hata hivyo toka kwangu wenye kuangamiza watamwendea, asema Bwana.

Yeremia 51:54 Jeremiah 51:54

Sauti ya kilio kutoka Babeli, Na ya uangamivu mkuu toka nchi ya Wakaldayo!

Yeremia 51:55 Jeremiah 51:55

Maana Bwana amwangamiza Babeli, Na kuikomesha sauti kuu ndani yake; Na mawimbi yake yavuma kama maji mengi, Mshindo wa sauti zao wafanya makelele;

Yeremia 51:56 Jeremiah 51:56

Kwa maana mwenye kuangamiza amefika kwake; Naam, amefika Babeli; Na mashujaa wake wametwaliwa; Pinde zao zimevunjika kabisa; Maana Bwana ni Mungu wa kisasi; Hakika yake yeye atalipa.

Yeremia 51:57 Jeremiah 51:57

Nami nitawalevya wakuu wake, na watu wake wenye hekima, maliwali wake, na maakida wake, na mashujaa wake; nao watalala usingizi wa milele, wasiamke, asema Mfalme, Bwana wa majeshi, ambaye jina lake ni Bwana.

Yeremia 51:58 Jeremiah 51:58

Bwana wa majeshi asema hivi, Kuta pana za Babeli zitabomolewa kabisa, na malango yake marefu yatateketezwa; nao watu watajitaabisha kwa ubatili, na mataifa kwa moto; nao watachoka.

Yeremia 51:59 Jeremiah 51:59

Neno ambalo Yeremia, nabii, alimwamuru Seraya, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa kumiliki kwake. Basi Seraya alikuwa msimamizi mkuu wa nyumba ya mfalme.

Yeremia 51:60 Jeremiah 51:60

Naye Yeremia akaandika katika kitabu habari ya mabaya yote yatakayoupata Babeli, maneno hayo yote yaliyoandikwa juu ya Babeli.

Yeremia 51:61 Jeremiah 51:61

Naye Yeremia akamwambia Seraya, Utakapofika Babeli, basi angalia uyasome maneno haya yote,

Yeremia 51:62 Jeremiah 51:62

ukaseme, Ee Bwana, umenena habari za mji huu kwamba utakatiliwa mbali, usikaliwe na awaye yote, wala wanadamu wala wanyama, lakini uwe ukiwa hata milele.

Yeremia 51:63 Jeremiah 51:63

Tena itakuwa utakapokwisha kukisoma kitabu hicho, utakifungia jiwe, na kukitupa katika mto Frati;

Yeremia 51:64 Jeremiah 51:64

nawe utasema, Hivyo ndivyo utakavyozama Babeli, wala hautazuka tena, kwa sababu ya mabaya yote nitakayoleta juu yake; nao watachoka. Maneno ya Yeremia yamefika hata hapa.