Yeremia Mlango 50 Jeremiah

Yeremia 50:1 Jeremiah 50:1

Neno hili ndilo alilosema Bwana, katika habari za Babeli, na katika habari za Wakaldayo, kwa kinywa cha Yeremia, nabii.

Yeremia 50:2 Jeremiah 50:2

Tangazeni katika mataifa, Mkahubiri na kutweka bendera; Hubirini, msifiche, semeni, Babeli umetwaliwa! Beli amefedheheka; Merodaki amefadhaika; Sanamu zake zimeaibishwa, Vinyago vyake vimefadhaika.

Yeremia 50:3 Jeremiah 50:3

Maana toka kaskazini taifa linakuja juu yake, litakaloifanya nchi yake kuwa ukiwa; wala hapana mtu atakayekaa humo; wamekimbia, wamekwenda zao, mwanadamu na mnyama pia.

Yeremia 50:4 Jeremiah 50:4

Katika siku hizo, na wakati huo, asema Bwana, wana wa Israeli watakuja, wao na wana wa Yuda pamoja; Wataendelea njiani mwao wakilia, nao watamtafuta Bwana, Mungu wao.

Yeremia 50:5 Jeremiah 50:5

Watauliza habari za Sayuni, na nyuso zao zitaelekea huko, wakisema, Njoni ninyi, mjiunge na Bwana, kwa agano la milele ambalo halitasahauliwa.

Yeremia 50:6 Jeremiah 50:6

Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao wamewapoteza; wamewapotosha milimani; wamekwenda toka mlima hata kilima, wamesahau mahali pao pa kupumzika.

Yeremia 50:7 Jeremiah 50:7

Watu wote waliowaona wamewala; na adui zao walisema, Sisi hatuna hatia, kwa kuwa hao wametenda dhambi juu ya Bwana, aliye kao la haki, yaani, Bwana, tumaini la baba zao.

Yeremia 50:8 Jeremiah 50:8

Kimbieni kutoka kati ya Babeli, mkatoke katika nchi ya Wakaldayo, mkawe kama mabeberu mbele ya makundi.

Yeremia 50:9 Jeremiah 50:9

Kwa maana juu ya Babeli nitaamsha na kuleta kusanyiko la mataifa makubwa, toka nchi ya kaskazini; nao watajipanga juu yake; kutoka huko atatwaliwa; mishale yao itakuwa kama ya mtu shujaa aliye stadi; hapana hata mmoja utakaorudi bure.

Yeremia 50:10 Jeremiah 50:10

Nao Ukaldayo utakuwa mateka; wote wautekao watashiba, asema Bwana.

Yeremia 50:11 Jeremiah 50:11

Kwa sababu mnafurahi, kwa sababu mnashangilia, enyi mnaouteka urithi wangu, kwa sababu mmewanda kama mtamba akanyagaye nafaka, nanyi mnalia kama farasi wenye nguvu;

Yeremia 50:12 Jeremiah 50:12

mama yenu atatahayarika sana; yeye aliyewazaa atafadhaika; tazama, atakuwa taifa lililo nyuma katika mataifa yote, atakuwa jangwa, nchi ya ukame, na nyika.

Yeremia 50:13 Jeremiah 50:13

Kwa sababu ya ghadhabu ya Bwana haitakaliwa na mtu, bali itakuwa ukiwa mtupu; kila mtu apitaye karibu na Babeli atashangaa, atazomea kwa sababu ya mapigo yake yote.

Yeremia 50:14 Jeremiah 50:14

Jipangeni juu ya Babeli pande zote, Ninyi nyote mpindao upinde; Mpigeni, msiuzuie hata mshale mmoja; Kwa maana amemtenda Bwana dhambi.

Yeremia 50:15 Jeremiah 50:15

Mpigieni kelele pande zote; amejitoa; Maboma yake yameanguka, kuta zake zimebomolewa; Kwa maana ni kisasi cha Bwana; mlipizeni kisasi; Kama yeye alivyotenda, mtendeni yeye.

Yeremia 50:16 Jeremiah 50:16

Mpanzi mkatilie mbali na Babeli, Naye ashikaye mundu wakati wa mavuno; Kwa sababu ya kuuogopa upanga uoneao, Watageuka kila mtu kwa watu wake, Nao wataikimbilia kila mmoja nchi yake.

Yeremia 50:17 Jeremiah 50:17

Israeli ni kondoo aliyetawanywa; simba wamemfukuzia mbali; kwanza mfalme wa Ashuru amemla, na mwisho Nebukadreza huyu, mfalme wa Babeli, amemvunja mifupa yake.

Yeremia 50:18 Jeremiah 50:18

Basi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, mimi nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na nchi yake, kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.

Yeremia 50:19 Jeremiah 50:19

Nami nitamleta Israeli tena malishoni kwake, naye atalisha juu ya Karmeli, na Bashani, na nafsi yake itashiba juu ya milima ya Efraimu, na katika Gileadi.

Yeremia 50:20 Jeremiah 50:20

Katika siku hizo na wakati huo, asema Bwana, uovu wa Israeli utatafutwa, wala uovu hapana; na dhambi za Yuda zitatafutwa, wala hazitaonekana; maana nitawasamehe wale niwaachao kuwa mabaki.

Yeremia 50:21 Jeremiah 50:21

Panda juu ya nchi ya Merathaimu, naam, juu yake, na juu yao wakaao Pekodi; ua, ukaangamize nyuma yao, asema Bwana, ukatende kama nilivyokuagiza, yote pia.

Yeremia 50:22 Jeremiah 50:22

Pana mshindo wa vita katika nchi, Mshindo wa uharibifu mkuu.

Yeremia 50:23 Jeremiah 50:23

Imekuwaje nyundo ya dunia yote Kukatiliwa mbali na kuvunjwa? Imekuwaje Babeli kuwa ukiwa Katikati ya mataifa?

Yeremia 50:24 Jeremiah 50:24

Nimekutegea mtego, Ee Babeli, nawe ukanaswa, nawe ulikuwa huna habari; umeonekana, ukakamatwa, kwa sababu ulishindana na Bwana.

Yeremia 50:25 Jeremiah 50:25

Bwana amefungua akiba yake ya silaha, naye amezitoa silaha za ghadhabu yake; maana Bwana, Bwana wa majeshi, ana kazi atakayofanya katika nchi ya Wakaldayo.

Yeremia 50:26 Jeremiah 50:26

Njoni juu yake toka mpaka ulio mbali; Zifungueni ghala zake; Mfanyeni kuwa magofu na kumharibu kabisa; Msimsazie kitu cho chote.

Yeremia 50:27 Jeremiah 50:27

Wachinjeni mafahali wake wote; Na watelemkie machinjoni; Ole wao! Maana siku yao imewadia, Wakati wa kujiliwa kwao.

Yeremia 50:28 Jeremiah 50:28

Sauti yao wakimbiao na kuokoka, Kutoka katika nchi ya Babeli, Ili kutangaza Sayuni kisasi cha Bwana, Mungu wetu, Kisasi cha hekalu lake.

Yeremia 50:29 Jeremiah 50:29

Waiteni wapiga mishale juu ya Babeli, Naam, wote waupindao upinde; Pangeni hema kumzunguka pande zote; Ili asiokoke hata mtu mmoja wao; Mlipeni kwa kadiri ya kazi yake; Mtendeni sawasawa na yote aliyoyatenda; Kwa sababu amefanya kiburi juu ya Bwana, Juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.

Yeremia 50:30 Jeremiah 50:30

Kwa sababu hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wake wa vita, wote pia, watanyamazishwa katika siku hiyo, asema Bwana.

Yeremia 50:31 Jeremiah 50:31

Tazama, mimi ni juu yako, Ewe mwenye kiburi, asema Bwana, Bwana wa majeshi; maana siku yako imewadia, wakati nitakapokujilia.

Yeremia 50:32 Jeremiah 50:32

Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua; nami nitawasha moto katika miji yake, nao utawala wote wamzungukao pande zote.

Yeremia 50:33 Jeremiah 50:33

Bwana wa majeshi asema hivi, Wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wameonewa pamoja; na wote waliowachukua mateka wanawashika sana; wanakataa kuwaacha.

Yeremia 50:34 Jeremiah 50:34

Mkombozi wao ni hodari; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; yeye atawatetea kwa bidii, apate kuistarehesha nchi, na kuwasumbua wakaao katika Babeli.

Yeremia 50:35 Jeremiah 50:35

Upanga u juu ya Wakaldayo, asema Bwana, na juu yao wakaao Babeli, na juu ya wakuu wake, na juu ya watu wake wenye hekima.

Yeremia 50:36 Jeremiah 50:36

Upanga u juu ya hao wajisifuo, nao watapumbazika; upanga u juu ya mashujaa wake, nao watafadhaika.

Yeremia 50:37 Jeremiah 50:37

Upanga u juu ya farasi zao, na juu ya magari yao ya vita; na juu ya watu wote waliochanganyika ndani yake, nao watakuwa kama wanawake; upanga u juu ya hazina zake, nazo zitaibwa.

Yeremia 50:38 Jeremiah 50:38

Ukosefu wa mvua u juu ya maji yake, nayo yatakaushwa; maana ni nchi ya sanamu za kuchongwa, nao wameingiwa na wazimu kwa ajili ya sanamu.

Yeremia 50:39 Jeremiah 50:39

Basi, wanyama wakali wa jangwani, pamoja na mbwa-mwitu, watakaa huko, na mbuni watakaa ndani yake; wala haitakaliwa na watu milele; wala hapana mtu atakayekaa huko tangu kizazi hata kizazi.

Yeremia 50:40 Jeremiah 50:40

Kama vile vilivyotokea Mungu alipoangusha Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema Bwana; kadhalika hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama wageni wakaavyo.

Yeremia 50:41 Jeremiah 50:41

Angalia, watu wanakuja watokao kaskazini; na taifa kubwa, na wafalme wengi wataamshwa toka pande za mwisho za dunia.

Yeremia 50:42 Jeremiah 50:42

Wanashika upinde na mkuki; Ni wakatili, hawana huruma; Sauti yao inanguruma kama bahari, Nao wamepanda farasi; Kila mmoja amejipanga kama aendaye vitani, Juu yako, Ee binti Babeli.

Yeremia 50:43 Jeremiah 50:43

Mfalme wa Babeli amesikia habari zao, Na mikono yake imekuwa dhaifu; Dhiki imemshika, na maumivu, Kama ya mwanamke katika utungu wake.

Yeremia 50:44 Jeremiah 50:44

Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafula ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu?

Yeremia 50:45 Jeremiah 50:45

Basi, lisikieni shauri la Bwana, Alilolifanya juu ya Babeli; Na makusudi yake aliyoyakusudia Juu ya nchi ya Wakaldayo. Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi; Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao.

Yeremia 50:46 Jeremiah 50:46

Kwa mshindo wa kutwaliwa Babeli nchi yatetemeka, Na kilio chake chasikiwa katika mataifa.