Luka Mlango 11 Luke

Luka 11:1 Luke 11:1

Ikawa alipokuwa mahali fulani akiomba, alipokwisha, mmoja katika wanafunzi wake alimwambia, Bwana, tufundishe sisi kusali, kama vile Yohana alivyowafundisha wanafunzi wake.

Luka 11:2 Luke 11:2

Akawaambia, Msalipo, semeni, Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.]

Luka 11:3 Luke 11:3

Utupe siku kwa siku riziki yetu.

Luka 11:4 Luke 11:4

Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye. Na usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu].

Luka 11:5 Luke 11:5

Akawaambia, Ni nani kwenu aliye na rafiki, akamwendea usiku wa manane, na kumwambia, Rafiki yangu, nikopeshe mikate mitatu,

Luka 11:6 Luke 11:6

kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu, atoka safarini, nami sina kitu cha kuweka mbele yake;

Luka 11:7 Luke 11:7

na yule wa ndani amjibu akisema, Usinitaabishe; mlango umekwisha fungwa, nasi tumelala kitandani mimi na watoto wangu; siwezi kuondoka nikupe?

Luka 11:8 Luke 11:8

Nawaambia ya kwamba, ijapokuwa haondoki ampe kwa kuwa ni rafiki yake, lakini kwa vile asivyoacha kumwomba, ataondoka na kumpa kadiri ya haja yake.

Luka 11:9 Luke 11:9

Nami nawaambia, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.

Luka 11:10 Luke 11:10

Kwa kuwa kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.

Luka 11:11 Luke 11:11

Maana ni yupi kwenu aliye baba, ambaye mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe au samaki, badala ya samaki atampa nyoka?

Luka 11:12 Luke 11:12

Au akimwomba yai, atampa nge?

Luka 11:13 Luke 11:13

Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho Mtakatifu hao wamwombao?

Luka 11:14 Luke 11:14

Naye alikuwa akitoa pepo bubu; ikawa pepo alipotoka, yule bubu akanena, makutano wakastaajabu.

Luka 11:15 Luke 11:15

Wengine wao wakasema, Atoa pepo kwa Beelzebuli, mkuu wa pepo.

Luka 11:16 Luke 11:16

Wengine walimjaribu, wakimtaka ishara itokayo mbinguni.

Luka 11:17 Luke 11:17

Naye akajua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme uliofitinika wenyewe kwa wenyewe hufanyika ukiwa; na nyumba juu ya nyumba huanguka.

Luka 11:18 Luke 11:18

Basi, ikiwa Shetani naye amefitinika juu ya nafsi yake, ufalme wake utasimamaje? Kwa kuwa ninyi mnasema kwamba mimi natoa pepo kwa Beelzebuli.

Luka 11:19 Luke 11:19

Basi, kama mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, wana wenu je! Huwatoa kwa nani? Kwa sababu hiyo, hao ndio watakaowahukumu.

Luka 11:20 Luke 11:20

Lakini, ikiwa mimi natoa pepo kwa kidole cha Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia.

Luka 11:21 Luke 11:21

Mtu mwenye nguvu aliyejifunga silaha zake, alindapo nyumba yake, vitu vyake vi salama;

Luka 11:22 Luke 11:22

lakini mtu mwenye nguvu kuliko yeye atakapomwendea na kumshinda, amnyang'anya silaha zake zote alizokuwa akizitegemea, na kuyagawanya mateka yake.

Luka 11:23 Luke 11:23

Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya.

Luka 11:24 Luke 11:24

Pepo mchafu amtokapo mtu, hupitia mahali pasipo maji, akitafuta mahali pa kupumzika; asipoona, husema,

Luka 11:25 Luke 11:25

Nitairudia nyumba yangu niliyotoka.

Luka 11:26 Luke 11:26

Hata afikapo, akaiona imefagiwa na kupambwa, ndipo huenda akachukua pepo wengine saba, walio waovu kuliko yeye mwenyewe, wakaingia na kukaa humo; na mtu yule hali yake ya mwisho huwa mbaya kuliko ya kwanza.

Luka 11:27 Luke 11:27

Ikawa alipokuwa akisema maneno hayo, mwanamke mmoja katika mkutano alipaza sauti yake, akamwambia, Heri tumbo lililokuzaa, na matiti uliyonyonya.

Luka 11:28 Luke 11:28

Lakini yeye alisema, Afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika.

Luka 11:29 Luke 11:29

Na makutano walipokuwa wakimkusanyikia, alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona.

Luka 11:30 Luke 11:30

Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki.

Luka 11:31 Luke 11:31

Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka ncha za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani.

Luka 11:32 Luke 11:32

Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.

Luka 11:33 Luke 11:33

Hakuna mtu awashaye taa na kuiweka mahali palipositirika, au chini ya pishi; bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuuona mwanga.

Luka 11:34 Luke 11:34

Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote unao mwanga; lakini likiwa bovu, mwili wako nao una giza.

Luka 11:35 Luke 11:35

Angalia basi, mwanga ulio ndani yako usije ukawa giza.

Luka 11:36 Luke 11:36

Basi kama mwanga umeenea katika mwili wako wote, wala hauna sehemu iliyo na giza, mwili wako wote utakuwa na mwanga mtupu; kama vile taa ikumulikiapo kwa mwanga wake.

Luka 11:37 Luke 11:37

Alipokuwa akinena, Farisayo mmoja alimwita aje kwake ale chakula; akaingia, akaketi chakulani.

Luka 11:38 Luke 11:38

Farisayo huyo alipomwona, alistaajabu kwa sababu hakunawa kabla ya chakula.

Luka 11:39 Luke 11:39

Bwana akamwambia, Ninyi Mafarisayo mwasafisha kikombe na sahani kwa nje, lakini ndani yenu mmejaa unyang'anyi na uovu.

Luka 11:40 Luke 11:40

Enyi wapumbavu; aliyevifanya vya nje, siye yeye aliyevifanya vya ndani pia?

Luka 11:41 Luke 11:41

Lakini, toeni sadaka vile vya ndani, na tazama, vyote huwa safi kwenu.

Luka 11:42 Luke 11:42

Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili.

Luka 11:43 Luke 11:43

Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni.

Luka 11:44 Luke 11:44

Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo.

Luka 11:45 Luke 11:45

Mtu mmoja katika wana-sheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi.

Luka 11:46 Luke 11:46

Akasema, Nanyi wana-sheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.

Luka 11:47 Luke 11:47

Ole wenu, kwa kuwa mwajenga maziara ya manabii, na baba zenu ndio waliowaua.

Luka 11:48 Luke 11:48

Basi, mwashuhudia na kuziridhia kazi za baba zenu; kwa kuwa wao waliwaua nanyi mwawajengea maziara.

Luka 11:49 Luke 11:49

Na kwa sababu hiyo hekima ya Mungu ilisema, Tazama, nitatuma kwao manabii na mitume, nao watawaua baadhi yao na kuwafukuza,

Luka 11:50 Luke 11:50

ili kwa kizazi hiki itakwe damu ya manabii wote, iliyomwagika tangu kupigwa msingi wa ulimwengu;

Luka 11:51 Luke 11:51

tangu damu ya Habili hata damu ya Zakaria, aliyeuawa kati ya madhabahu na hekalu. Naam, nawaambieni ya kwamba itatakwa kwa kizazi hiki.

Luka 11:52 Luke 11:52

Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.

Luka 11:53 Luke 11:53

Alipotoka humo, waandishi na Mafarisayo walianza kumsonga vibaya, na kumchokoza kwa maswali mengi,

Luka 11:54 Luke 11:54

wakimvizia, ili wapate neno litokalo kinywani mwake.