Luka Mlango 14 Luke

Luka 14:1 Luke 14:1

Ikawa alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia.

Luka 14:2 Luke 14:2

Na tazama, mbele yake palikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa safura.

Luka 14:3 Luke 14:3

Yesu akajibu, akawaambia wana-sheria na Mafarisayo, Je! Ni halali kuponya siku ya sabato, ama sivyo?

Luka 14:4 Luke 14:4

Wao wakanyamaza. Akamshika, akamponya, akamruhusu aende zake.

Luka 14:5 Luke 14:5

Akawaambia, Ni nani miongoni mwenu, ikiwa ng'ombe wake au punda wake ametumbukia kisimani, asiyemwopoa mara hiyo siku ya sabato?

Luka 14:6 Luke 14:6

Nao hawakuweza kujibu maneno haya.

Luka 14:7 Luke 14:7

Akawaambia mfano wale walioalikwa, alipoona jinsi walivyochagua viti vya mbele; akisema,

Luka 14:8 Luke 14:8

Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe,

Luka 14:9 Luke 14:9

akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma.

Luka 14:10 Luke 14:10

Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe.

Luka 14:11 Luke 14:11

Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.

Luka 14:12 Luke 14:12

Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo.

Luka 14:13 Luke 14:13

Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu,

Luka 14:14 Luke 14:14

nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.

Luka 14:15 Luke 14:15

Basi aliposikia hayo mmojawapo wa wale walioketi chakulani pamoja naye alimwambia, Heri yule atakayekula mkate katika ufalme wa Mungu.

Luka 14:16 Luke 14:16

Akamwambia, Mtu mmoja alifanya karamu kubwa akaalika watu wengi,

Luka 14:17 Luke 14:17

akamtuma mtumwa wake saa ya chakula awaambie wale walioalikwa, Njoni, kwa kuwa vitu vyote vimekwisha kuwekwa tayari.

Luka 14:18 Luke 14:18

Wakaanza wote kutoa udhuru kwa nia moja. Wa kwanza alimwambia, Nimenunua shamba, sharti niende nikalitazame; tafadhali unisamehe.

Luka 14:19 Luke 14:19

Mwingine akasema, Nimenunua ng'ombe jozi tano, ninakwenda kuwajaribu; tafadhali unisamehe.

Luka 14:20 Luke 14:20

Mwingine akasema, Nimeoa mke, na kwa sababu hiyo siwezi kuja.

Luka 14:21 Luke 14:21

Yule mtumwa akaenda, akampa bwana wake habari ya mambo hayo. Basi, yule mwenye nyumba akakasirika, akamwambia mtumwa wake, Toka upesi, uende katika njia kuu na vichochoro vya mji, ukawalete hapa maskini, na vilema, na vipofu, na viwete.

Luka 14:22 Luke 14:22

Mtumwa akasema, Bwana, hayo uliyoagiza yamekwisha tendeka, na hata sasa ingaliko nafasi.

Luka 14:23 Luke 14:23

Bwana akamwambia mtumwa, Toka nje uende barabarani na mipakani, ukawashurutishe kuingia ndani, nyumba yangu ipate kujaa.

Luka 14:24 Luke 14:24

Maana nawaambia ya kwamba katika wale walioalikwa, hapana hata mmoja atakayeionja karamu yangu.

Luka 14:25 Luke 14:25

Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,

Luka 14:26 Luke 14:26

Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Luka 14:27 Luke 14:27

Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Luka 14:28 Luke 14:28

Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?

Luka 14:29 Luke 14:29

Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,

Luka 14:30 Luke 14:30

wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.

Luka 14:31 Luke 14:31

Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?

Luka 14:32 Luke 14:32

Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.

Luka 14:33 Luke 14:33

Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Luka 14:34 Luke 14:34

Chumvi ni kitu chema; lakini chumvi ikiwa imeharibika, itiwe nini ikolee?

Luka 14:35 Luke 14:35

Haiifai nchi wala jaa; watu huitupa nje. Mwenye masikio ya kusikilia, na asikie.