Luka Mlango 15 Luke

Luka 15:1 Luke 15:1

Basi watoza ushuru wote na wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize.

Luka 15:2 Luke 15:2

Mafarisayo na waandishi wakanung'unika, wakisema, Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi, tena hula nao.

Luka 15:3 Luke 15:3

Akawaambia mfano huu, akisema,

Luka 15:4 Luke 15:4

Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?

Luka 15:5 Luke 15:5

Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi.

Luka 15:6 Luke 15:6

Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.

Luka 15:7 Luke 15:7

Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.

Luka 15:8 Luke 15:8

Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione?

Luka 15:9 Luke 15:9

Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.

Luka 15:10 Luke 15:10

Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye.

Luka 15:11 Luke 15:11

Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili;

Luka 15:12 Luke 15:12

yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake.

Luka 15:13 Luke 15:13

Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati.

Luka 15:14 Luke 15:14

Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji.

Luka 15:15 Luke 15:15

Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.

Luka 15:16 Luke 15:16

Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.

Luka 15:17 Luke 15:17

Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa.

Luka 15:18 Luke 15:18

Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako;

Luka 15:19 Luke 15:19

sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.

Luka 15:20 Luke 15:20

Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.

Luka 15:21 Luke 15:21

Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena.

Luka 15:22 Luke 15:22

Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni;

Luka 15:23 Luke 15:23

mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi;

Luka 15:24 Luke 15:24

kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia.

Luka 15:25 Luke 15:25

Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo.

Luka 15:26 Luke 15:26

Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini?

Luka 15:27 Luke 15:27

Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima.

Luka 15:28 Luke 15:28

Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi.

Luka 15:29 Luke 15:29

Akamjibu baba yake, akasema, Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;

Luka 15:30 Luke 15:30

lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona.

Luka 15:31 Luke 15:31

Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.

Luka 15:32 Luke 15:32

Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.