Luka Mlango 19 Luke

Luka 19:1 Luke 19:1

Naye alipoingia Yeriko alipita katikati yake.

Luka 19:2 Luke 19:2

Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri.

Luka 19:3 Luke 19:3

Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo.

Luka 19:4 Luke 19:4

Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile.

Luka 19:5 Luke 19:5

Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako.

Luka 19:6 Luke 19:6

Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha.

Luka 19:7 Luke 19:7

Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi.

Luka 19:8 Luke 19:8

Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne.

Luka 19:9 Luke 19:9

Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu.

Luka 19:10 Luke 19:10

Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

Luka 19:11 Luke 19:11

Waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara.

Luka 19:12 Luke 19:12

Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi.

Luka 19:13 Luke 19:13

Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja.

Luka 19:14 Luke 19:14

Lakini watu wa mji wake walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale.

Luka 19:15 Luke 19:15

Ikawa aliporudi, ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila mtu kwa biashara yake.

Luka 19:16 Luke 19:16

Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.

Luka 19:17 Luke 19:17

Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.

Luka 19:18 Luke 19:18

Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.

Luka 19:19 Luke 19:19

Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano.

Luka 19:20 Luke 19:20

Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu lako, ambalo nililiweka akiba katika leso.

Luka 19:21 Luke 19:21

Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa usichoweka, wavuna usichopanda.

Luka 19:22 Luke 19:22

Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe. Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda;

Luka 19:23 Luke 19:23

basi, mbona hukuiweka fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake?

Luka 19:24 Luke 19:24

Akawaambia waliosimama karibu, Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi.

Luka 19:25 Luke 19:25

Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.

Luka 19:26 Luke 19:26

Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho.

Luka 19:27 Luke 19:27

Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu.

Luka 19:28 Luke 19:28

Na alipokwisha kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.

Luka 19:29 Luke 19:29

Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi,

Luka 19:30 Luke 19:30

akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa.

Luka 19:31 Luke 19:31

Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji.

Luka 19:32 Luke 19:32

Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia.

Luka 19:33 Luke 19:33

Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda?

Luka 19:34 Luke 19:34

Wakasema, Bwana ana haja naye.

Luka 19:35 Luke 19:35

Wakampeleka kwa Yesu, wakatandika nguo zao juu ya mwana-punda, wakampandisha Yesu.

Luka 19:36 Luke 19:36

Na alipokuwa akienda walitandaza nguo zao njiani.

Luka 19:37 Luke 19:37

Hata alipokuwa amekaribia matelemko ya mlima wa Mizeituni, kundi zima la wanafunzi wake walianza kufurahi na kumsifu Mungu kwa sauti kuu, kwa ajili ya matendo yote ya uwezo waliyoyaona,

Luka 19:38 Luke 19:38

wakasema, Ndiye mbarikiwa Mfalme ajaye kwa jina la Bwana; amani mbinguni, na utukufu huko juu.

Luka 19:39 Luke 19:39

Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa katika mkutano wakamwambia, Mwalimu, uwakanye wanafunzi wako.

Luka 19:40 Luke 19:40

Akajibu, akasema, Nawaambia ninyi, wakinyamaza hawa, mawe yatapiga kelele.

Luka 19:41 Luke 19:41

Alipofika karibu aliuona mji, akaulilia,

Luka 19:42 Luke 19:42

akisema, Laiti ungalijua, hata wewe katika siku hii, yapasayo amani! Lakini sasa yamefichwa machoni pako.

Luka 19:43 Luke 19:43

Kwa kuwa siku zitakuja, adui zako watakapokujengea boma, likuzunguke; watakuzingira na kukuhusuru pande zote;

Luka 19:44 Luke 19:44

watakuangusha chini wewe na watoto wako ndani yako, wasikuachie jiwe juu ya jiwe, kwa sababu hukutambua majira ya kujiliwa kwako.

Luka 19:45 Luke 19:45

Akaingia hekaluni, akaanza kuwatoa wale waliokuwa wakifanya biashara,

Luka 19:46 Luke 19:46

akiwaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.

Luka 19:47 Luke 19:47

Naye akawa akifundisha kila siku hekaluni. Lakini wakuu wa makuhani, na waandishi, na wakuu wa watu walikuwa wakitafuta njia ya kumwangamiza;

Luka 19:48 Luke 19:48

wasione la kutenda, kwa kuwa watu wote walikuwa wakiandamana naye, wakimsikiliza.