Mambo ya Walawi Mlango 13 Leviticus

Mambo ya Walawi 13:1 Leviticus 13:1

Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,

Mambo ya Walawi 13:2 Leviticus 13:2

Mtu atakapokuwa na kivimbe katika ngozi ya mwili wake, au kikoko, au kipaku king'aacho, nalo likawa pigo la ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa wanawe, makuhani mmojawapo;

Mambo ya Walawi 13:3 Leviticus 13:3

na huyo kuhani ataliangalia hilo pigo lililo katika ngozi ya mwili; na kwamba malaika yaliyo katika hilo pigo yamegeuka kuwa meupe, na hilo pigo kuonekana kwake limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili wake, ni pigo la ukoma hilo; na kuhani atamwangalia na kusema kuwa yu mwenye unajisi.

Mambo ya Walawi 13:4 Leviticus 13:4

Na hicho kipaku king'aacho, kwamba ni cheupe katika ngozi ya mwili wake, na kuonekana kwake si shimo la kuingia ndani kuliko ngozi, na malaika hayakugeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba huyo aliye na hilo pigo;

Mambo ya Walawi 13:5 Leviticus 13:5

kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limeshangaa, na pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena;

Mambo ya Walawi 13:6 Leviticus 13:6

kisha siku ya saba kuhani atamwangalia tena; na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, wala pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atasema kuwa yu safi; ni kikoko; naye atazifua nguo zake, kisha atakuwa yu safi.

Mambo ya Walawi 13:7 Leviticus 13:7

Lakini kwamba kikoko kimeenea katika ngozi yake baada ya kuonyesha nafsi yake kwa kuhani kwa kupata kutakaswa kwake ataonyesha nafsi yake tena kwa kuhani;

Mambo ya Walawi 13:8 Leviticus 13:8

na kuhani ataangalia, na tazama ikiwa hicho kikoko kimeenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kuwa yu najisi; ni ukoma.

Mambo ya Walawi 13:9 Leviticus 13:9

Pigo la ukoma litakapokuwa katika mtu, ndipo ataletwa kwa kuhani;

Mambo ya Walawi 13:10 Leviticus 13:10

na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pana kivimbe cheupe katika ngozi yake, na malaika yamegeuzwa kuwa meupe, tena ikiwa pana nyama mbichi iliyomea katika kile kivimbe,

Mambo ya Walawi 13:11 Leviticus 13:11

ni ukoma wa zamani ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa yu najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye yuna unajisi.

Mambo ya Walawi 13:12 Leviticus 13:12

Tena kwamba huo ukoma ukitokeza katika ngozi yake, na ukoma ukamwenea ngozi yote, tangu kichwa hata miguuni, kama aonavyo kuhani;

Mambo ya Walawi 13:13 Leviticus 13:13

ndipo huyo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa ukoma umemwenea mwili wake wote, atasema kuwa yu safi huyo aliye na hilo pigo umegeuka kuwa mweupe wote; yeye ni safi.

Mambo ya Walawi 13:14 Leviticus 13:14

Lakini po pote itakapoonekana nyama mbichi kwake mtu huyo, atakuwa yu najisi.

Mambo ya Walawi 13:15 Leviticus 13:15

Kuhani ataiangalia hiyo nyama mbichi, naye atasema kuwa yu najisi; ile nyama mbichi ni najisi; ni ukoma.

Mambo ya Walawi 13:16 Leviticus 13:16

Au kama hiyo nyama mbichi iligeuka tena, na kugeuzwa kuwa nyeupe, ndipo atamwendea kuhani,

Mambo ya Walawi 13:17 Leviticus 13:17

na huyo kuhani atamwangalia; na tazama, ikiwa hilo pigo limegeuzwa kuwa jeupe, ndipo huyo kuhani atasema kuwa yu safi huyo aliyekuwa na pigo; yeye yu safi.

Mambo ya Walawi 13:18 Leviticus 13:18

Tena mwili wa mtu utakapokuwa na jipu katika ngozi yake, nalo limepoa,

Mambo ya Walawi 13:19 Leviticus 13:19

na mahali palipokuwa na lile jipu pana kivimbe cheupe, au kipaku king'aacho, cheupe lakini chekundu kidogo, ndipo atamwonyesha kuhani mahali hapo;

Mambo ya Walawi 13:20 Leviticus 13:20

na kuhani ataangalia, na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na malaika yakiwa yamegeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; ni pigo la ukoma limetokea katika hilo jipu.

Mambo ya Walawi 13:21 Leviticus 13:21

Lakini kuhani akipaangalia, na tazama hamna malaika meupe ndani yake, wala hapana pa kuingia ndani kuliko ile ngozi, lakini paanza kufifia, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;

Mambo ya Walawi 13:22 Leviticus 13:22

na kwamba pameenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo.

Mambo ya Walawi 13:23 Leviticus 13:23

Lakini ikiwa kipaku hicho king'aacho kimeshangaa pale pale, wala hakienei, ni kovu ya jipu; na kuhani atasema kwamba yu safi.

Mambo ya Walawi 13:24 Leviticus 13:24

Au mwili wa mtu ukiwa una mahali katika ngozi yake penye moto, na hiyo nyama iliyomea pale penye moto, kama kikiwa kipaku chekundu kidogo, au cheupe;

Mambo ya Walawi 13:25 Leviticus 13:25

ndipo kuhani atapaangalia; na tazama, yakiwa malaika yaliyo katika kile kipaku yamegeuka kuwa meupe, na kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe; ni ukoma, umetokea katika mahali penye moto; na kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo la ukoma.

Mambo ya Walawi 13:26 Leviticus 13:26

Lakini kuhani akipaangalia, na tazama, malaika meupe hamna katika hicho kipaku king'aacho, nacho hakikuingia ndani kuliko ngozi, lakini chafifia; ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;

Mambo ya Walawi 13:27 Leviticus 13:27

na kuhani atamwangalia siku ya saba; kama kimeenea katika ngozi, ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo la ukoma.

Mambo ya Walawi 13:28 Leviticus 13:28

Na kama hicho kipaku kikishangaa pale pale, wala hakikuenea katika ngozi, lakini kimefifia; ni kufura kwake pale penye moto, na kuhani atasema kwamba yu safi; kwa kuwa ni kovu la kuwasha hili.

Mambo ya Walawi 13:29 Leviticus 13:29

Tena mtu, mume au mke, akiwa na pigo juu ya kichwa, au katika ndevu zake,

Mambo ya Walawi 13:30 Leviticus 13:30

ndipo kuhani ataliangalia hilo pigo; na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, tena zikiwamo nywele za rangi ya manjano kisha nyembamba, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi, maana, ni kipwepwe, ni ukoma wa kichwa, au wa ndevu.

Mambo ya Walawi 13:31 Leviticus 13:31

Tena kuhani akiliangalia lile pigo la kipwepwe, na tazama, kwamba kumeonekana si kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, wala hamna nywele nyeusi ndani yake, ndipo kuhani atamweka mahali huyo aliye na pigo la kipwepwe muda wa siku saba;

Mambo ya Walawi 13:32 Leviticus 13:32

na siku ya saba kuhani ataliangalia hilo pigo; na ikiwa hicho kipwepwe hakikuenea, wala hamna nywele za rangi ya manjano ndani yake, na kwamba kipwepwe hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe,

Mambo ya Walawi 13:33 Leviticus 13:33

ndipo huyo mtu atanyolewa, lakini hicho kipwepwe hatakinyoa; na kuhani atamweka mahali huyo aliye na kipwepwe muda wa siku saba tena;

Mambo ya Walawi 13:34 Leviticus 13:34

na siku ya saba kuhani atakiangalia hicho kipwepwe, na tazama, ikiwa kipwepwe hakikuenea katika ngozi yake, wala hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi; ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu safi; naye atazifua nguo zake, naye atakuwa yu safi.

Mambo ya Walawi 13:35 Leviticus 13:35

Lakini hicho kipwepwe kama kikienea katika ngozi yake baada ya kutakasika kwake;

Mambo ya Walawi 13:36 Leviticus 13:36

ndipo kuhani atamwangalia; na ikiwa hicho kipwepwe kimeenea katika ngozi yake, kuhani hatatafuta hizo nywele za rangi ya manjano; yeye yu najisi.

Mambo ya Walawi 13:37 Leviticus 13:37

Lakini akiona ya kuwa hicho kipwepwe kimeshangaa, na nywele nyeusi zimemea humo; hicho kipwepwe kimepoa, naye yu safi, na huyo kuhani atasema kwamba yu safi.

Mambo ya Walawi 13:38 Leviticus 13:38

Mtu, mume au mke, atakapokuwa na vipaku ving'aavyo katika ngozi ya mwili, vipaku ving'aavyo vyeupe;

Mambo ya Walawi 13:39 Leviticus 13:39

ndipo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa vile vipaku ving'aavyo vilivyo katika ngozi ya mwili wake ni vyeupe kidogo; ni mba hivyo, imetokea katika ngozi; yeye yu safi.

Mambo ya Walawi 13:40 Leviticus 13:40

Kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani mwake, yeye ni mwenye upaa, yu safi.

Mambo ya Walawi 13:41 Leviticus 13:41

Tena kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani upande wa mbele, yeye ni mwenye upaa wa kipaji; yu safi.

Mambo ya Walawi 13:42 Leviticus 13:42

Lakini kwamba katika kile kichwa kilicho na upaa, au kile kipaji kilicho na upaa, laonekana pigo jeupe kisha jekundu kidogo; ni ukoma, unatokea katika kichwa chake cha upaa, au katika kipaji chake cha upaa.

Mambo ya Walawi 13:43 Leviticus 13:43

Ndipo kuhani atamwangalia; na tazama, kivimbe cha pigo kikiwa cheupe na chekundu-chekundu, katika kichwa chake chenye upaa, au katika kipaji chake cha upaa, kama vile kuonekana kwa ukoma katika ngozi ya mwili;

Mambo ya Walawi 13:44 Leviticus 13:44

yeye ni mtu mwenye ukoma, yu najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa yu najisi; pigo lake li katika kichwa chake.

Mambo ya Walawi 13:45 Leviticus 13:45

Kisha mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, nguo zake zitararuliwa, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu, naye atapiga kelele, Ni najisi, ni najisi.

Mambo ya Walawi 13:46 Leviticus 13:46

Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago.

Mambo ya Walawi 13:47 Leviticus 13:47

Tena, vazi nalo ambalo pigo la ukoma li ndani yake, kwamba ni vazi la sufu, au kwamba ni la kitani;

Mambo ya Walawi 13:48 Leviticus 13:48

likiwa limefumwa, au kusokotwa; likiwa ni la kitani au la sufu; kwamba ni katika ngozi, au kitu cho chote kilichofanywa cha ngozi;

Mambo ya Walawi 13:49 Leviticus 13:49

hilo pigo likiwa la rangi ya majani au jekundu, katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi; ni pigo la ukoma, nalo ataonyeshwa kuhani;

Mambo ya Walawi 13:50 Leviticus 13:50

na kuhani ataliangalia hilo pigo, naye atakiweka mahali kile kilicho na pigo muda wa siku saba;

Mambo ya Walawi 13:51 Leviticus 13:51

kisha siku ya saba ataliangalia hilo pigo; kama pigo limeenea katika hilo lililofumwa, au katika hilo lililosokotwa, au katika ngozi, ijapokuwa hiyo ngozi ina matumizi yo yote; hilo pigo ni ukoma unaokula; vazi hilo ni najisi.

Mambo ya Walawi 13:52 Leviticus 13:52

Naye atalichoma moto vazi hilo, kwamba ni lililofumwa au kwamba ni lililosokotwa, kama ni la sufu, au la kitani, au kitu cho chote cha ngozi, ambacho kina hilo pigo ndani yake; kwa maana, ni ukoma unaokula; vazi hilo litachomwa moto;

Mambo ya Walawi 13:53 Leviticus 13:53

Na kama kuhani akitazama, na tazama, ikiwa hilo pigo halikuenea katika hilo vazi, wala katika hilo lililofumwa, wala katika hilo lililosokotwa, wala katika kitu cho chote cha ngozi;

Mambo ya Walawi 13:54 Leviticus 13:54

ndipo kuhani ataamuru kwamba wakifue kitu kile kilicho na hilo pigo, naye atakiweka mahali muda wa siku saba tena;

Mambo ya Walawi 13:55 Leviticus 13:55

kisha kuhani ataangalia, baada ya kuoshwa hilo pigo; na tazama, ikiwa hilo pigo halikugeuka rangi yake, wala halikuenea, li najisi; utakichoma moto; ni uharibifu likiwa lina upaa ndani au nje.

Mambo ya Walawi 13:56 Leviticus 13:56

Huyo kuhani akiangalia, na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, baada ya kufuliwa kwake, ndipo atalirarua hilo pigo litoke katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa;

Mambo ya Walawi 13:57 Leviticus 13:57

kisha, likionekana li vivyo katika hilo vazi, katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi, ni pigo lenye kuenea; nawe vazi hilo lenye pigo utalichoma moto.

Mambo ya Walawi 13:58 Leviticus 13:58

Na hilo vazi, lililofumwa, au lililosokotwa, au kitu cho chote cha ngozi, utakalolifua, kama hilo pigo limetoka na kuliacha, ndipo litafuliwa mara ya pili, nalo litakuwa safi.

Mambo ya Walawi 13:59 Leviticus 13:59

Na katika pigo la ukoma katika vazi la sufu, au la kitani, kama ni katika lililofumwa, au lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi, sheria yake ni hiyo, kusema kwamba ni safi, au kusema kwamba ni najisi.