Mathayo Mlango 17 Matthew

Mathayo 17:1 Matthew 17:1

Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani;

Mathayo 17:2 Matthew 17:2

akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru.

Mathayo 17:3 Matthew 17:3

Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye.

Mathayo 17:4 Matthew 17:4

Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya.

Mathayo 17:5 Matthew 17:5

Alipokuwa katika kusema, tazama, wingu jeupe likawatia uvuli; na tazama, sauti ikatoka katika lile wingu, ikasema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye.

Mathayo 17:6 Matthew 17:6

Na wale wanafunzi waliposikia, walianguka kifulifuli, wakaogopa sana.

Mathayo 17:7 Matthew 17:7

Yesu akaja, akawagusa, akasema, Inukeni, wala msiogope.

Mathayo 17:8 Matthew 17:8

Wakainua macho yao, wasione mtu ila Yesu peke yake.

Mathayo 17:9 Matthew 17:9

Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu.

Mathayo 17:10 Matthew 17:10

Wanafunzi wake wakamwuliza, wakisema, Basi kwa nini waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza?

Mathayo 17:11 Matthew 17:11

Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza yote,

Mathayo 17:12 Matthew 17:12

ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao.

Mathayo 17:13 Matthew 17:13

Ndipo wale wanafunzi walipofahamu ya kuwa amesema nao habari za Yohana Mbatizaji.

Mathayo 17:14 Matthew 17:14

Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema,

Mathayo 17:15 Matthew 17:15

Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini.

Mathayo 17:16 Matthew 17:16

Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya.

Mathayo 17:17 Matthew 17:17

Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu.

Mathayo 17:18 Matthew 17:18

Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile.

Mathayo 17:19 Matthew 17:19

Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa?

Mathayo 17:20 Matthew 17:20

Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.

Mathayo 17:21 Matthew 17:21

[Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]

Mathayo 17:22 Matthew 17:22

Nao walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka.

Mathayo 17:23 Matthew 17:23

Wakasikitika sana.

Mathayo 17:24 Matthew 17:24

Hata walipofika Kapernaumu, wale watozao nusu-shekeli walimwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi nusu-shekeli? Akasema, Hutoa.

Mathayo 17:25 Matthew 17:25

Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? Kwa wana wao au kwa wageni?

Mathayo 17:26 Matthew 17:26

Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru.

Mathayo 17:27 Matthew 17:27

Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukaye kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.