Mathayo Mlango 13 Matthew

Mathayo 13:1 Matthew 13:1

Siku ile Yesu akatoka nyumbani, akaketi kando ya bahari.

Mathayo 13:2 Matthew 13:2

Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani.

Mathayo 13:3 Matthew 13:3

Akawaambia mambo mengi kwa mifano, akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda.

Mathayo 13:4 Matthew 13:4

Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila;

Mathayo 13:5 Matthew 13:5

nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina;

Mathayo 13:6 Matthew 13:6

na jua lilipozuka ziliungua; na kwa kuwa hazina mizizi zikanyauka.

Mathayo 13:7 Matthew 13:7

Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga;

Mathayo 13:8 Matthew 13:8

nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini.

Mathayo 13:9 Matthew 13:9

Mwenye masikio na asikie.

Mathayo 13:10 Matthew 13:10

Wakaja wanafunzi, wakamwambia, Kwa nini wasema nao kwa mifano?

Mathayo 13:11 Matthew 13:11

Akajibu, akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za ufalme wa mbinguni, bali wao hawakujaliwa.

Mathayo 13:12 Matthew 13:12

Kwa maana ye yote mwenye kitu atapewa, naye atazidishiwa tele; lakini ye yote asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa.

Mathayo 13:13 Matthew 13:13

Kwa sababu hii nasema nao kwa mifano; kwa kuwa wakitazama hawaoni, na wakisikia hawasikii, wala kuelewa.

Mathayo 13:14 Matthew 13:14

Na neno la nabii Isaya linatimia kwao, likisema, Kusikia mtasikia, wala hamtaelewa; Kutazama mtatazama, wala hamtaona.

Mathayo 13:15 Matthew 13:15

Maana mioyo ya watu hawa imekuwa mizito, Na kwa masikio yao hawasikii vema, Na macho yao wameyafumba; Wasije wakaona kwa macho yao, Wakasikia kwa masikio yao, Wakaelewa kwa mioyo yao, Wakaongoka, nikawaponya.

Mathayo 13:16 Matthew 13:16

Lakini, heri macho yenu, kwa kuwa yanaona; na masikio yenu, kwa kuwa yanasikia.

Mathayo 13:17 Matthew 13:17

Kwa maana, amin, nawaambia, Manabii wengi na wenye haki walitamani kuyaona mnayoyaona ninyi, wasiyaone; na kuyasikia mnayoyasikia ninyi, wasiyasikie.

Mathayo 13:18 Matthew 13:18

Basi ninyi sikilizeni mfano wa mpanzi.

Mathayo 13:19 Matthew 13:19

Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake. Huyo ndiye aliyepandwa karibu na njia.

Mathayo 13:20 Matthew 13:20

Naye aliyepandwa penye miamba, huyo ndiye alisikiaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha;

Mathayo 13:21 Matthew 13:21

lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa.

Mathayo 13:22 Matthew 13:22

Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno; likawa halizai.

Mathayo 13:23 Matthew 13:23

Naye aliyepandwa penye udongo mzuri, huyo ndiye alisikiaye lile neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini, na huyu thelathini.

Mathayo 13:24 Matthew 13:24

Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;

Mathayo 13:25 Matthew 13:25

lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.

Mathayo 13:26 Matthew 13:26

Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.

Mathayo 13:27 Matthew 13:27

Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?

Mathayo 13:28 Matthew 13:28

Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?

Mathayo 13:29 Matthew 13:29

Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing'oa ngano pamoja nayo.

Mathayo 13:30 Matthew 13:30

Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu.

Mathayo 13:31 Matthew 13:31

Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na punje ya haradali, aliyoitwaa mtu akaipanda katika shamba lake;

Mathayo 13:32 Matthew 13:32

nayo ni ndogo kuliko mbegu zote; lakini ikiisha kumea, huwa kubwa kuliko mboga zote, ikawa mti, hata nyuni wa angani huja na kukaa katika matawi yake.

Mathayo 13:33 Matthew 13:33

Akawaambia mfano mwingine; Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.

Mathayo 13:34 Matthew 13:34

Hayo yote Yesu aliwaambia makutano kwa mifano; wala pasipo mfano hakuwaambia neno;

Mathayo 13:35 Matthew 13:35

ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema, Nitafumbua kinywa changu kwa mifano, Nitayatamka yaliyositirika tangu awali.

Mathayo 13:36 Matthew 13:36

Kisha Yesu akawaaga makutano, akaingia nyumbani; wanafunzi wake wakamwendea, wakasema, Tufafanulie mfano wa magugu ya kondeni.

Mathayo 13:37 Matthew 13:37

Akajibu, akasema, Azipandaye zile mbegu njema ni Mwana wa Adamu;

Mathayo 13:38 Matthew 13:38

lile konde ni ulimwengu; zile mbegu njema ni wana wa ufalme; na yale magugu ni wana wa yule mwovu;

Mathayo 13:39 Matthew 13:39

yule adui aliyeyapanda ni Ibilisi; mavuno ni mwisho wa dunia; na wale wavunao ni malaika.

Mathayo 13:40 Matthew 13:40

Basi, kama vile magugu yakusanywavyo na kuchomwa motoni; ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia.

Mathayo 13:41 Matthew 13:41

Mwana wa Adamu atawatuma malaika zake, nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi,

Mathayo 13:42 Matthew 13:42

na kuwatupa katika tanuru ya moto, ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Mathayo 13:43 Matthew 13:43

Ndipo wenye haki watakapong'aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio, na asikie.

Mathayo 13:44 Matthew 13:44

Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile.

Mathayo 13:45 Matthew 13:45

Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri;

Mathayo 13:46 Matthew 13:46

naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua.

Mathayo 13:47 Matthew 13:47

Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;

Mathayo 13:48 Matthew 13:48

hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa.

Mathayo 13:49 Matthew 13:49

Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki,

Mathayo 13:50 Matthew 13:50

na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.

Mathayo 13:51 Matthew 13:51

Yesu aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam.

Mathayo 13:52 Matthew 13:52

Akawaambia, Kwa sababu hiyo, kila mwandishi mwenye elimu ya ufalme wa mbinguni amefanana na mtu mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale.

Mathayo 13:53 Matthew 13:53

Ikawa Yesu alipoimaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake.

Mathayo 13:54 Matthew 13:54

Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii?

Mathayo 13:55 Matthew 13:55

Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda?

Mathayo 13:56 Matthew 13:56

Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote?

Mathayo 13:57 Matthew 13:57

Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe.

Mathayo 13:58 Matthew 13:58

Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.