Mathayo Mlango 26 Matthew

Mathayo 26:1 Matthew 26:1

Ikawa Yesu alipomaliza maneno hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake,

Mathayo 26:2 Matthew 26:2

Mnajua ya kuwa baada ya siku mbili itakuwa Pasaka, na Mwana wa Adamu atasalitiwa asulibiwe.

Mathayo 26:3 Matthew 26:3

Wakati ule wakuu wa makuhani, na wazee wa watu, wakakusanyika katika behewa ya Kuhani Mkuu, jina lake Kayafa;

Mathayo 26:4 Matthew 26:4

wakafanya shauri pamoja, ili wamkamate Yesu kwa hila na kumwua.

Mathayo 26:5 Matthew 26:5

Lakini wakasema, Isiwe wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu.

Mathayo 26:6 Matthew 26:6

Naye Yesu alipokuwapo Bethania katika nyumba ya Simoni mkoma,

Mathayo 26:7 Matthew 26:7

mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya thamani kubwa alimkaribia akaimimina kichwani pake alipoketi chakulani.

Mathayo 26:8 Matthew 26:8

Wanafunzi wake walipoona, wakachukiwa, wakasema, Ni wa nini upotevu huu?

Mathayo 26:9 Matthew 26:9

Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa fedha nyingi wakapewa maskini.

Mathayo 26:10 Matthew 26:10

Yesu akatambua akawaambia, Mbona mnamtaabisha mwanamke? Maana ni kazi njema aliyonitendea mimi.

Mathayo 26:11 Matthew 26:11

Kwa maana siku zote mnao maskini pamoja nanyi; lakini mimi hamnami siku zote.

Mathayo 26:12 Matthew 26:12

Maana kwa kunimwagia mwili wangu marhamu hiyo, ametenda hivyo ili kuniweka tayari kwa maziko yangu.

Mathayo 26:13 Matthew 26:13

Amin, nawaambieni, Kila patakapohubiriwa Injili hii katika ulimwengu wote, tendo hilo alilolitenda huyu litatajwa pia kwa kumbukumbu lake.

Mathayo 26:14 Matthew 26:14

Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani,

Mathayo 26:15 Matthew 26:15

akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha.

Mathayo 26:16 Matthew 26:16

Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti.

Mathayo 26:17 Matthew 26:17

Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka?

Mathayo 26:18 Matthew 26:18

Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu.

Mathayo 26:19 Matthew 26:19

Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka.

Mathayo 26:20 Matthew 26:20

Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara.

Mathayo 26:21 Matthew 26:21

Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti.

Mathayo 26:22 Matthew 26:22

Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana?

Mathayo 26:23 Matthew 26:23

Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti.

Mathayo 26:24 Matthew 26:24

Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa.

Mathayo 26:25 Matthew 26:25

Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.

Mathayo 26:26 Matthew 26:26

Nao walipokuwa wakila Yesu alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa wanafunzi wake, akasema, Twaeni, mle; huu ndio mwili wangu

Mathayo 26:27 Matthew 26:27

Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa, akisema, Nyweni nyote katika hiki;

Mathayo 26:28 Matthew 26:28

kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi.

Mathayo 26:29 Matthew 26:29

Lakini nawaambieni, Sitakunywa kabisa tangu sasa uzao huu wa mzabibu, hata siku ile nitakapokunywa mpya pamoja nanyi katika ufalme wa Baba yangu.

Mathayo 26:30 Matthew 26:30

Nao walipokwisha kuimba, wakatoka nje kwenda mlima wa Mizeituni.

Mathayo 26:31 Matthew 26:31

Ndipo Yesu akawaambia, Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.

Mathayo 26:32 Matthew 26:32

Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya.

Mathayo 26:33 Matthew 26:33

Petro akajibu, akamwambia, Wajapochukizwa wote kwa ajili yako, mimi sitachukizwa kamwe.

Mathayo 26:34 Matthew 26:34

Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, usiku huu kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu.

Mathayo 26:35 Matthew 26:35

Petro akamwambia, Ijaponipasa kufa nawe, sitakukana kamwe. Na wanafunzi wote wakasema vivyo hivyo.

Mathayo 26:36 Matthew 26:36

Kisha Yesu akaenda pamoja nao mpaka bustani iitwayo Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, hata niende kule nikaombe.

Mathayo 26:37 Matthew 26:37

Akamchukua Petro na wale wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuhuzunika na kusononeka.

Mathayo 26:38 Matthew 26:38

Ndipo akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa, mkeshe pamoja nami.

Mathayo 26:39 Matthew 26:39

Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifulifuli, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke; walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe.

Mathayo 26:40 Matthew 26:40

Akawajia wale wanafunzi, akawakuta wamelala, akamwambia Petro, Je! Hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?

Mathayo 26:41 Matthew 26:41

Kesheni, mwombe, msije mkaingia majaribuni; roho i radhi, lakini mwili ni dhaifu.

Mathayo 26:42 Matthew 26:42

Akaenda tena mara ya pili, akaomba, akisema, Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe.

Mathayo 26:43 Matthew 26:43

Akaja tena, akawakuta wamelala; maana macho yao yamekuwa mazito.

Mathayo 26:44 Matthew 26:44

Akawaacha tena, akaenda, akaomba mara ya tatu, akisema maneno yale yale.

Mathayo 26:45 Matthew 26:45

Kisha akawajia wanafunzi wake, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike tazama, saa imekaribia, na Mwana wa Adamu anatiwa katika mikono ya wenye dhambi.

Mathayo 26:46 Matthew 26:46

Ondokeni, twende zetuni! Tazama, yule anayenisaliti amekaribia.

Mathayo 26:47 Matthew 26:47

Basi alipokuwa katika kusema, tazama, Yuda, mmoja wa wale Thenashara akaja, na pamoja naye kundi kubwa wenye panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani na wazee wa watu.

Mathayo 26:48 Matthew 26:48

Na yule mwenye kumsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni.

Mathayo 26:49 Matthew 26:49

Mara akamwendea Yesu, akasema, Salamu, Rabi, akambusu.

Mathayo 26:50 Matthew 26:50

Yesu akamwambia, Rafiki, fanya ulilolijia. Wakaenda, wakanyosha mikono yao wakamkamata Yesu.

Mathayo 26:51 Matthew 26:51

Na tazama, mmoja wao waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono wake, akaufuta upanga wake, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.

Mathayo 26:52 Matthew 26:52

Ndipo Yesu akamwambia, Rudisha upanga wako mahali pake, maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga.

Mathayo 26:53 Matthew 26:53

Ama wadhani ya kuwa mimi siwezi kumsihi Baba yangu, naye ataniletea sasa hivi zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?

Mathayo 26:54 Matthew 26:54

Yatatimizwaje basi maandiko, ya kwamba hivyo ndivyo vilivyopasa kujiri?

Mathayo 26:55 Matthew 26:55

Saa ile Yesu akawaambia makutano, Je, mmetoka kama kumkamata mnyang'anyi, wenye panga na marungu, ili kunishika? Kila siku naliketi hekaluni nikifundisha, msinikamate.

Mathayo 26:56 Matthew 26:56

Lakini haya yote yamekuwa, ili maandiko ya manabii yatimizwe. Ndipo wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.

Mathayo 26:57 Matthew 26:57

Nao waliomkamata Yesu wakampeleka kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokuwa wamekutanika waandishi na wazee.

Mathayo 26:58 Matthew 26:58

Na Petro akamfuata kwa mbali mpaka behewa ya Kuhani Mkuu, akaingia ndani, akaketi pamoja na watumishi, auone mwisho.

Mathayo 26:59 Matthew 26:59

Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda wa uongo juu ya Yesu, wapate kumwua;

Mathayo 26:60 Matthew 26:60

wasiuone wangawa walitokea mashahidi wa uongo wengi.

Mathayo 26:61 Matthew 26:61

Hata baadaye wawili wakatokea, wakasema, Huyu alisema, Naweza kulivunja hekalu la Mungu, na kulijenga kwa siku tatu.

Mathayo 26:62 Matthew 26:62

Kisha Kuhani Mkuu akasimama akamwambia, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini?

Mathayo 26:63 Matthew 26:63

Lakini, Yesu akanyamaza. Kuhani Mkuu akamwambia, Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, utuambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu.

Mathayo 26:64 Matthew 26:64

Yesu akamwambia, Wewe umesema; lakini nawaambieni, Tangu sasa mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija juu ya mawingu ya mbinguni.

Mathayo 26:65 Matthew 26:65

Ndipo Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akisema, Amekufuru; mna haja gani tena ya mashahidi? Tazameni, sasa mmesikia hiyo kufuru yake;

Mathayo 26:66 Matthew 26:66

mwaonaje ninyi? Wakajibu, wakasema, Imempasa kuuawa.

Mathayo 26:67 Matthew 26:67

Ndipo wakamtemea mate ya uso, wakampiga makonde; wengine wakampiga makofi,

Mathayo 26:68 Matthew 26:68

wakisema, Ewe Kristo, tufumbulie; ni nani aliyekupiga?

Mathayo 26:69 Matthew 26:69

Na Petro alikuwa ameketi nje behewani; kijakazi mmoja akamwendea, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na Yesu wa Galilaya.

Mathayo 26:70 Matthew 26:70

Akakana mbele ya wote, akisema, Sijui usemalo.

Mathayo 26:71 Matthew 26:71

Naye alipotoka nje hata ukumbini, mwanamke mwingine alimwona, akawaambia watu waliokuwako huko, Huyu alikuwapo pamoja na Yesu Mnazareti.

Mathayo 26:72 Matthew 26:72

Akakana tena kwa kiapo, Simjui mtu huyu.

Mathayo 26:73 Matthew 26:73

Punde kidogo, wale waliohudhuria wakamwendea, wakamwambia Petro, Hakika wewe nawe u mmoja wao; kwa sababu hata usemi wako wakutambulisha.

Mathayo 26:74 Matthew 26:74

Ndipo akaanza kulaani na kuapa akisema, Simjui mtu huyu. Na mara akawika jogoo.

Mathayo 26:75 Matthew 26:75

Petro akalikumbuka lile neno la Yesu alilolisema, Kabla ya kuwika jogoo, utanikana mara tatu. Akatoka nje, akalia kwa majonzi.