Mathayo Mlango 4 Matthew

Mathayo 4:1 Matthew 4:1

Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani, ili ajaribiwe na Ibilisi.

Mathayo 4:2 Matthew 4:2

Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa.

Mathayo 4:3 Matthew 4:3

Mjaribu akamjia akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, amuru kwamba mawe haya yawe mikate.

Mathayo 4:4 Matthew 4:4

Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu.

Mathayo 4:5 Matthew 4:5

Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu,

Mathayo 4:6 Matthew 4:6

akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe.

Mathayo 4:7 Matthew 4:7

Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.

Mathayo 4:8 Matthew 4:8

Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mlima mrefu mno, akamwonyesha milki zote za ulimwengu, na fahari yake,

Mathayo 4:9 Matthew 4:9

akamwambia, Haya yote nitakupa, ukianguka kunisujudia.

Mathayo 4:10 Matthew 4:10

Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.

Mathayo 4:11 Matthew 4:11

Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.

Mathayo 4:12 Matthew 4:12

Basi Yesu aliposikia ya kwamba Yohana amefungwa, alikwenda zake mpaka Galilaya;

Mathayo 4:13 Matthew 4:13

akatoka Nazareti, akaja akakaa Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali;

Mathayo 4:14 Matthew 4:14

ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema,

Mathayo 4:15 Matthew 4:15

Nchi ya Zabuloni na nchi ya Naftali, Njia ya bahari, ng'ambo ya Yordani, Galilaya ya mataifa,

Mathayo 4:16 Matthew 4:16

Watu wale waliokaa katika giza Wameona mwanga mkuu, Nao waliokaa katika nchi na uvuli wa mauti Mwanga umewazukia.

Mathayo 4:17 Matthew 4:17

Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia.

Mathayo 4:18 Matthew 4:18

Naye alipokuwa akitembea kando ya bahari ya Galilaya, aliona ndugu wawili, Simoni aitwaye Petro, na Andrea nduguye, wakitupa jarife baharini; kwa maana walikuwa wavuvi.

Mathayo 4:19 Matthew 4:19

Akawaambia, Nifuateni, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu.

Mathayo 4:20 Matthew 4:20

Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

Mathayo 4:21 Matthew 4:21

Akaendelea mbele, akaona ndugu wengine wawili, Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye, ambao walikuwamo chomboni pamoja na Zebedayo baba yao, wakizitengeneza nyavu zao; akawaita.

Mathayo 4:22 Matthew 4:22

Mara wakakiacha chombo na baba yao, wakamfuata.

Mathayo 4:23 Matthew 4:23

Naye alikuwa akizunguka katika Galilaya yote, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri Habari Njema ya ufalme, na kuponya ugonjwa na udhaifu wa kila namna katika watu.

Mathayo 4:24 Matthew 4:24

Na habari zake zikaenea katika Shamu yote; wakamletea wote waliokuwa hawawezi, walioshikwa na maradhi mbalimbali na mateso, wenye pepo, na wenye kifafa, na wenye kupooza; akawaponya.

Mathayo 4:25 Matthew 4:25

Na makutano mengi wakamfuata, kutoka Galilaya, na Dekapoli, na Yerusalemu, na Uyahudi, na ng'ambo ya Yordani