Mathayo Mlango 23 Matthew

Mathayo 23:1 Matthew 23:1

Kisha Yesu akawaambia makutano na wanafunzi wake, akasema,

Mathayo 23:2 Matthew 23:2

Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa;

Mathayo 23:3 Matthew 23:3

basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi.

Mathayo 23:4 Matthew 23:4

Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao.

Mathayo 23:5 Matthew 23:5

Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao;

Mathayo 23:6 Matthew 23:6

hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi,

Mathayo 23:7 Matthew 23:7

na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi.

Mathayo 23:8 Matthew 23:8

Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu.

Mathayo 23:9 Matthew 23:9

Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni.

Mathayo 23:10 Matthew 23:10

Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo.

Mathayo 23:11 Matthew 23:11

Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu.

Mathayo 23:12 Matthew 23:12

Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.

Mathayo 23:13 Matthew 23:13

Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie.

Mathayo 23:14 Matthew 23:14

[Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnakula nyumba za wajane, na kwa unafiki mnasali sala ndefu; kwa hiyo mtapata hukumu iliyo kubwa zaidi.]

Mathayo 23:15 Matthew 23:15

Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe.

Mathayo 23:16 Matthew 23:16

Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga.

Mathayo 23:17 Matthew 23:17

Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au lile hekalu liitakasalo dhahabu?

Mathayo 23:18 Matthew 23:18

Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga.

Mathayo 23:19 Matthew 23:19

Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka?

Mathayo 23:20 Matthew 23:20

Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake.

Mathayo 23:21 Matthew 23:21

Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake.

Mathayo 23:22 Matthew 23:22

Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake.

Mathayo 23:23 Matthew 23:23

Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnalipa zaka za mnanaa na bizari na jira, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria, yaani, adili, na rehema, na imani; hayo imewapasa kuyafanya, wala yale mengine msiyaache.

Mathayo 23:24 Matthew 23:24

Viongozi vipofu, wenye kuchuja mbu na kumeza ngamia.

Mathayo 23:25 Matthew 23:25

Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang'anyi na kutokuwa na kiasi.

Mathayo 23:26 Matthew 23:26

Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.

Mathayo 23:27 Matthew 23:27

Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote.

Mathayo 23:28 Matthew 23:28

Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi.

Mathayo 23:29 Matthew 23:29

Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki,

Mathayo 23:30 Matthew 23:30

na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii.

Mathayo 23:31 Matthew 23:31

Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii.

Mathayo 23:32 Matthew 23:32

Kijazeni basi kipimo cha baba zenu.

Mathayo 23:33 Matthew 23:33

Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum?

Mathayo 23:34 Matthew 23:34

Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji;

Mathayo 23:35 Matthew 23:35

hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu.

Mathayo 23:36 Matthew 23:36

Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki.

Mathayo 23:37 Matthew 23:37

Ee Yerusalemu, Yerusalemu, uwauaye manabii, na kuwapiga kwa mawe wale waliotumwa kwako! Ni mara ngapi nimetaka kuwakusanya pamoja watoto wako, kama vile kuku avikusanyavyo pamoja vifaranga vyake chini ya mabawa yake, lakini hamkutaka!

Mathayo 23:38 Matthew 23:38

Angalieni, nyumba yenu mmeachiwa hali ya ukiwa.

Mathayo 23:39 Matthew 23:39

Kwa maana nawaambia, Hamtaniona kamwe tangu sasa, hata mtakaposema, Amebarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.