Mathayo Mlango 10 Matthew

Mathayo 10:1 Matthew 10:1

Akawaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina.

Mathayo 10:2 Matthew 10:2

Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya; Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohana nduguye;

Mathayo 10:3 Matthew 10:3

Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo;

Mathayo 10:4 Matthew 10:4

Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti.

Mathayo 10:5 Matthew 10:5

Hao Thenashara Yesu aliwatuma, akawaagiza, akisema, Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wo wote wa Wasamaria msiingie.

Mathayo 10:6 Matthew 10:6

Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.

Mathayo 10:7 Matthew 10:7

Na katika kuenenda kwenu, hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.

Mathayo 10:8 Matthew 10:8

Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure.

Mathayo 10:9 Matthew 10:9

Msichukue dhahabu, wala fedha, wala mapesa mishipini mwenu;

Mathayo 10:10 Matthew 10:10

wala mkoba wa safari, wala kanzu mbili, wala viatu, wala fimbo; maana mtenda kazi astahili posho lake.

Mathayo 10:11 Matthew 10:11

Na mji wo wote au kijiji cho chote mtakachoingia, tafuteni ni nani humo aliye mtu mwaminifu; mkae kwake hata mtakapotoka.

Mathayo 10:12 Matthew 10:12

Nanyi mkiingia katika nyumba isalimuni.

Mathayo 10:13 Matthew 10:13

Na nyumba ile ikistahili, amani yenu na iifikilie; la, kwamba haistahili, amani yenu na iwarudie ninyi.

Mathayo 10:14 Matthew 10:14

Na mtu asipowakaribisha wala kuyasikiliza maneno yenu, mtokapo katika nyumba ile, au mji ule, kung'uteni mavumbi ya miguuni mwenu.

Mathayo 10:15 Matthew 10:15

Amin, nawaambia, itakuwa rahisi nchi ya Sodoma na Gomora kustahimili adhabu ya siku ya hukumu, kuliko mji ule.

Mathayo 10:16 Matthew 10:16

Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa-mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua.

Mathayo 10:17 Matthew 10:17

Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga;

Mathayo 10:18 Matthew 10:18

nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa.

Mathayo 10:19 Matthew 10:19

Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema.

Mathayo 10:20 Matthew 10:20

Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu.

Mathayo 10:21 Matthew 10:21

Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha.

Mathayo 10:22 Matthew 10:22

Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka.

Mathayo 10:23 Matthew 10:23

Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.

Mathayo 10:24 Matthew 10:24

Mwanafunzi hampiti mwalimu wake, wala mtumwa hampiti bwana wake.

Mathayo 10:25 Matthew 10:25

Yamtosha mwanafunzi kuwa kama mwalimu wake, na mtumwa kuwa kama bwana wake. Ikiwa wamemwita mwenye nyumba Beelzebuli, je! Si zaidi wale walio wa nyumbani mwake?

Mathayo 10:26 Matthew 10:26

Basi, msiwaogope, kwa maana hakuna neno lililositirika, ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa, ambalo halitajulikana.

Mathayo 10:27 Matthew 10:27

Niwaambialo ninyi katika giza, lisemeni katika nuru; na msikialo kwa siri, lihubirini juu ya nyumba.

Mathayo 10:28 Matthew 10:28

Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum.

Mathayo 10:29 Matthew 10:29

Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu;

Mathayo 10:30 Matthew 10:30

lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.

Mathayo 10:31 Matthew 10:31

Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi.

Mathayo 10:32 Matthew 10:32

Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.

Mathayo 10:33 Matthew 10:33

Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.

Mathayo 10:34 Matthew 10:34

Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.

Mathayo 10:35 Matthew 10:35

Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu;

Mathayo 10:36 Matthew 10:36

na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.

Mathayo 10:37 Matthew 10:37

Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.

Mathayo 10:38 Matthew 10:38

Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.

Mathayo 10:39 Matthew 10:39

Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.

Mathayo 10:40 Matthew 10:40

Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma.

Mathayo 10:41 Matthew 10:41

Ampokeaye nabii kwa kuwa ni nabii, atapata thawabu ya nabii; naye ampokeaye mwenye haki kwa kuwa ni mwenye haki, atapata thawabu ya mwenye haki.

Mathayo 10:42 Matthew 10:42

Na mtu awaye yote atakayemnywesha mmojawapo wa wadogo hawa ngaa kikombe cha maji ya baridi, kwa kuwa ni mwanafunzi, amin, nawaambia, haitampotea kamwe thawabu yake.