Mathayo Mlango 21 Matthew

Mathayo 21:1 Matthew 21:1

Hata walipokaribia Yerusalemu, na kufika Bethfage, katika mlima wa Mizeituni, ndipo Yesu alipotuma wanafunzi wawili akiwaambia,

Mathayo 21:2 Matthew 21:2

Enendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mara mtaona punda amefungwa, na mwana-punda pamoja naye; wafungueni mniletee.

Mathayo 21:3 Matthew 21:3

Na kama mtu akiwaambia neno, semeni, Bwana anawahitaji; na mara huyo atawapeleka.

Mathayo 21:4 Matthew 21:4

Haya yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na nabii, akisema,

Mathayo 21:5 Matthew 21:5

Mwambieni binti Sayuni Tazama, mfalme wako anakuja kwako, Mpole, naye amepanda punda, Na mwana-punda, mtoto wa punda.

Mathayo 21:6 Matthew 21:6

Wale wanafunzi wakaenda zao, wakafanya kama Yesu alivyowaamuru,

Mathayo 21:7 Matthew 21:7

wakamleta yule punda na mwana-punda, wakaweka nguo zao juu yao, naye akaketi juu yake.

Mathayo 21:8 Matthew 21:8

Watu wengi katika ule mkutano wakatandaza nguo zao njiani; na wengine wakakata matawi ya miti, wakayatandaza njiani.

Mathayo 21:9 Matthew 21:9

Na makutano waliotangulia, na wale waliofuata, wakapaza sauti, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi; ndiye mbarikiwa, yeye ajaye kwa jina la Bwana; Hosana juu mbinguni.

Mathayo 21:10 Matthew 21:10

Hata alipoingia Yerusalemu, mji wote ukataharuki, watu wakisema, Ni nani huyu?

Mathayo 21:11 Matthew 21:11

Makutano wakasema, Huyu ni yule nabii, Yesu, wa Nazareti ya Galilaya.

Mathayo 21:12 Matthew 21:12

Yesu akaingia ndani ya hekalu, akawafukuza wote waliokuwa wakiuza na kununua hekaluni, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa;

Mathayo 21:13 Matthew 21:13

akawaambia, Imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.

Mathayo 21:14 Matthew 21:14

Na vipofu na viwete wakamwendea mle hekaluni, akawaponya.

Mathayo 21:15 Matthew 21:15

Lakini wakuu wa makuhani na waandishi walipoyaona maajabu aliyoyafanya, na watoto waliopaza sauti zao hekaluni, wakisema, Hosana, Mwana wa Daudi! Walikasirika,

Mathayo 21:16 Matthew 21:16

wakamwambia, Wasikia hawa wasemavyo? Yesu akawaambia, Naam; hamkupata kusoma, Kwa vinywa vya watoto wachanga na wanyonyao umekamilisha sifa?

Mathayo 21:17 Matthew 21:17

Akawaacha, akatoka nje ya mji mpaka Bethania, akalala huko.

Mathayo 21:18 Matthew 21:18

Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa.

Mathayo 21:19 Matthew 21:19

Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; akauambia, Yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele. Mtini ukanyauka mara.

Mathayo 21:20 Matthew 21:20

Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, Jinsi gani mtini umenyauka mara?

Mathayo 21:21 Matthew 21:21

Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng'oka, ukatupwe baharini, litatendeka.

Mathayo 21:22 Matthew 21:22

Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.

Mathayo 21:23 Matthew 21:23

Hata alipokwisha kuingia hekaluni, wakuu wa makuhani na wazee wa watu wakamwendea alipokuwa akifundisha, wakasema, Ni kwa amri gani unatenda mambo haya? Naye ni nani aliyekupa amri hii?

Mathayo 21:24 Matthew 21:24

Yesu akajibu akawaambia, Na mimi nitawauliza neno moja; ambalo mkinijibu, nami nitawaambia ni kwa amri gani ninatenda haya.

Mathayo 21:25 Matthew 21:25

Ubatizo wa Yohana ulitoka wapi? Ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, Tukisema, Ulitoka mbinguni, atatuambia, Mbona basi hamkumwamini?

Mathayo 21:26 Matthew 21:26

Na tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, twaogopa mkutano; maana watu wote wamwona Yohana kuwa ni nabii.

Mathayo 21:27 Matthew 21:27

Wakamjibu Yesu wakasema, Hatujui. Naye akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa amri gani ninatenda haya.

Mathayo 21:28 Matthew 21:28

Lakini mwaonaje? Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; akamwendea yule wa kwanza, akasema, Mwanangu, leo nenda kafanye kazi katika shamba la mizabibu.

Mathayo 21:29 Matthew 21:29

Akajibu akasema, Naenda, Bwana; asiende.

Mathayo 21:30 Matthew 21:30

Akamwendea yule wa pili, akasema vile vile. Naye akajibu akasema, Sitaki; baadaye akatubu, akaenda.

Mathayo 21:31 Matthew 21:31

Je! Katika hao wawili ni yupi aliyefanya mapenzi ya babaye? Wakamwambia, Ni yule wa pili. Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu.

Mathayo 21:32 Matthew 21:32

Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini.

Mathayo 21:33 Matthew 21:33

Sikilizeni mfano mwingine. Kulikuwa na mtu mwenye nyumba, naye alipanda shamba la mizabibu, akalizungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo ndani yake, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri.

Mathayo 21:34 Matthew 21:34

Wakati wa matunda ulipokuwa karibu, akawatuma watumwa wake kwa wale wakulima, wapokee matunda yake.

Mathayo 21:35 Matthew 21:35

Wale wakulima wakawakamata watumwa wake, huyu wakampiga, na huyu wakamwua, na huyu wakampiga kwa mawe.

Mathayo 21:36 Matthew 21:36

Akawatuma tena watumwa wengine wengi kuliko wa kwanza wakawatenda vile vile.

Mathayo 21:37 Matthew 21:37

Mwishowe akamtuma mwanawe kwao, akisema, Watamstahi mwanangu.

Mathayo 21:38 Matthew 21:38

Lakini wale wakulima walipomwona yule mwana, wakasemezana wao kwa wao, Huyu ni mrithi; haya na tumwue, tuutwae urithi wake.

Mathayo 21:39 Matthew 21:39

Wakamkamata, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu, wakamwua.

Mathayo 21:40 Matthew 21:40

Basi atakapokuja yule bwana wa shamba la mizabibu, atawatendaje wale wakulima?

Mathayo 21:41 Matthew 21:41

Wakamwambia, Atawaangamiza vibaya wale wabaya; na shamba la mizabibu atawapangisha wakulima wengine, watakaomlipa matunda kwa wakati wake.

Mathayo 21:42 Matthew 21:42

Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu?

Mathayo 21:43 Matthew 21:43

Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake.

Mathayo 21:44 Matthew 21:44

Naye aangukaye juu ya jiwe hilo atavunjika-vunjika; naye ye yote ambaye litamwangukia, litamsaga tikitiki.

Mathayo 21:45 Matthew 21:45

Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, waliposikia mifano yake, walitambua ya kuwa anawanenea wao.

Mathayo 21:46 Matthew 21:46

Nao walipotafuta kumkamata, waliwaogopa makutano, kwa maana wao walimwona kuwa nabii.