Mathayo Mlango 27 Matthew

Mathayo 27:1 Matthew 27:1

Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua;

Mathayo 27:2 Matthew 27:2

wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa liwali.

Mathayo 27:3 Matthew 27:3

Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, alipoona ya kuwa amekwisha kuhukumiwa, alijuta, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, Nalikosa nilipoisaliti damu isiyo na hatia.

Mathayo 27:4 Matthew 27:4

Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.

Mathayo 27:5 Matthew 27:5

Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga.

Mathayo 27:6 Matthew 27:6

Wakuu wa makuhani wakavitwaa vile vipande vya fedha, wakasema, Si halali kuviweka katika sanduku ya sadaka, kwa kuwa ni kima cha damu.

Mathayo 27:7 Matthew 27:7

Wakafanya shauri, wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.

Mathayo 27:8 Matthew 27:8

Kwa hiyo konde lile huitwa konde la damu hata leo.

Mathayo 27:9 Matthew 27:9

Ndipo likatimia neno lililonenwa na nabii Yeremia, akisema, Wakavitwaa vipande thelathini vya fedha, kima chake aliyetiwa kima, ambaye baadhi ya Waisraeli walimtia kima;

Mathayo 27:10 Matthew 27:10

wakavitumia kwa kununua konde la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza.

Mathayo 27:11 Matthew 27:11

Naye Yesu akasimama mbele ya liwali; liwali akamwuliza, akasema, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Yesu akamwambia, Wewe wasema.

Mathayo 27:12 Matthew 27:12

Lakini aliposhitakiwa na wakuu wa makuhani na wazee, hakujibu hata neno.

Mathayo 27:13 Matthew 27:13

Ndipo Pilato akamwambia, Husikii ni mambo mangapi wanayokushuhudia?

Mathayo 27:14 Matthew 27:14

Asimjibu hata neno moja, hata liwali akastaajabu sana.

Mathayo 27:15 Matthew 27:15

Basi wakati wa siku kuu, liwali desturi yake huwafungulia mkutano mfungwa mmoja waliyemtaka.

Mathayo 27:16 Matthew 27:16

Basi palikuwa na mfungwa mashuhuri siku zile, aitwaye Baraba.

Mathayo 27:17 Matthew 27:17

Basi walipokutanika, Pilato akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi? Yule Baraba, au Yesu aitwaye Kristo?

Mathayo 27:18 Matthew 27:18

Kwa maana alijua ya kuwa wamemtoa kwa husuda.

Mathayo 27:19 Matthew 27:19

Na alipokuwa ameketi juu ya kiti cha hukumu, mkewe alimpelekea mjumbe, kumwambia, Usiwe na neno na yule mwenye haki; kwa sababu nimeteswa mengi leo katika ndoto kwa ajili yake.

Mathayo 27:20 Matthew 27:20

Nao wakuu wa makuhani na wazee wakawashawishi makutano ili wamtake Baraba, na kumwangamiza Yesu.

Mathayo 27:21 Matthew 27:21

Basi liwali akajibu, akawaambia, Mnataka niwafungulie yupi katika hawa wawili? Wakasema, Baraba.

Mathayo 27:22 Matthew 27:22

Pilato akawaambia, Basi, nimtendeje Yesu aitwaye Kristo? Wakasema wote, Asulibiwe.

Mathayo 27:23 Matthew 27:23

Akasema, Kwani? Ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, wakisema, Na asulibiwe.

Mathayo 27:24 Matthew 27:24

Basi Pilato alipoona ya kuwa hafai lo lote, bali ghasia inazidi tu, akatwaa maji, akanawa mikono yake mbele ya mkutano, akasema, Mimi sina hatia katika damu ya mtu huyu mwenye haki; yaangalieni haya ninyi wenyewe.

Mathayo 27:25 Matthew 27:25

Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.

Mathayo 27:26 Matthew 27:26

Ndipo akawafungulia Baraba; na baada ya kumpiga Yesu mijeledi, akamtoa ili asulibiwe.

Mathayo 27:27 Matthew 27:27

Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima.

Mathayo 27:28 Matthew 27:28

Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu.

Mathayo 27:29 Matthew 27:29

Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi!

Mathayo 27:30 Matthew 27:30

Kisha wakamtemea mate, wakautwaa ule mwanzi, wakampiga-piga kichwani.

Mathayo 27:31 Matthew 27:31

Walipokwisha kumdhihaki, wakalivua lile vazi, wakamvika mavazi yake, wakamchukua kumsulibisha.

Mathayo 27:32 Matthew 27:32

Hata walipokuwa wakitoka, wakamwona mtu Mkirene, jina lake Simoni; huyu wakamshurutisha auchukue msalaba wake.

Mathayo 27:33 Matthew 27:33

Na walipofika mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa,

Mathayo 27:34 Matthew 27:34

wakampa kunywa divai iliyochanganyika na nyongo; lakini yeye alipoionja hakutaka kunywa.

Mathayo 27:35 Matthew 27:35

Walipokwisha kumsulibisha, waligawa mavazi yake, wakipiga kura; [ili litimie neno lililonenwa na nabii, Waligawa nguo zangu kati yao, na juu ya vazi langu walipiga kura.]

Mathayo 27:36 Matthew 27:36

Wakaketi, wakamlinda huko.

Mathayo 27:37 Matthew 27:37

Wakaweka juu ya kichwa chake mashitaka yake, yaliyoandikwa HUYU NI YESU, MFALME WA WAYAHUDI.

Mathayo 27:38 Matthew 27:38

Wakati uo huo wanyang'anyi wawili wakasulibiwa pamoja naye, mmoja mkono wake wa kuume, na mmoja mkono wake wa kushoto.

Mathayo 27:39 Matthew 27:39

Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa vyao, wakisema,

Mathayo 27:40 Matthew 27:40

Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka msalabani.

Mathayo 27:41 Matthew 27:41

Kadhalika na wale wakuu wa makuhani wakamdhihaki pamoja na waandishi na wazee, wakisema, Aliokoa wengine, hawezi kujiokoa mwenyewe.

Mathayo 27:42 Matthew 27:42

Yeye ni mfalme wa Israeli; na ashuke sasa msalabani, nasi tutamwamini.

Mathayo 27:43 Matthew 27:43

Amemtegemea Mungu; na amwokoe sasa, kama anamtaka; kwa maana alisema, Mimi ni Mwana wa Mungu.

Mathayo 27:44 Matthew 27:44

Pia wale wanyang'anyi waliosulibiwa pamoja naye walimshutumu vile vile.

Mathayo 27:45 Matthew 27:45

Basi tangu saa sita palikuwa na giza juu ya nchi yote hata saa tisa.

Mathayo 27:46 Matthew 27:46

Na kama saa tisa, Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu akisema, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Yaani, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?

Mathayo 27:47 Matthew 27:47

Na baadhi yao waliohudhuria, waliposikia, walisema, Huyu anamwita Eliya.

Mathayo 27:48 Matthew 27:48

Mara mmoja wao akaenda mbio, akatwaa sifongo, akaijaza siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha.

Mathayo 27:49 Matthew 27:49

Wale wengine wakasema, Acha; na tuone kama Eliya anakuja kumwokoa.

Mathayo 27:50 Matthew 27:50

Naye Yesu akiisha kupaza sauti tena kwa nguvu, akaitoa roho yake.

Mathayo 27:51 Matthew 27:51

Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;

Mathayo 27:52 Matthew 27:52

makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;

Mathayo 27:53 Matthew 27:53

nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi.

Mathayo 27:54 Matthew 27:54

Basi yule akida, na hao waliokuwa pamoja naye wakimlinda Yesu, walipoliona tetemeko la nchi na mambo yaliyofanyika, wakaogopa sana, wakisema, Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu.

Mathayo 27:55 Matthew 27:55

Palikuwa na wanawake wengi pale wakitazama kwa mbali, hao ndio waliomfuata Yesu toka Galilaya, na kumtumikia.

Mathayo 27:56 Matthew 27:56

Miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo na Yusufu, na mama yao wana wa Zebedayo.

Mathayo 27:57 Matthew 27:57

Hata ilipokuwa jioni akafika mtu tajiri wa Arimathaya, jina lake Yusufu, naye mwenyewe alikuwa mwanafunzi wa Yesu;

Mathayo 27:58 Matthew 27:58

mtu huyu alimwendea Pilato akauomba mwili wa Yesu. Ndipo Pilato akaamuru apewe.

Mathayo 27:59 Matthew 27:59

Yusufu akautwaa mwili, akauzonga-zonga katika sanda ya kitani safi,

Mathayo 27:60 Matthew 27:60

akauweka katika kaburi lake jipya, alilokuwa amelichonga mwambani; akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.

Mathayo 27:61 Matthew 27:61

Na pale walikuwapo Mariamu Magdalene, na Mariamu yule wa pili, wameketi kulielekea kaburi.

Mathayo 27:62 Matthew 27:62

Hata siku ya pili, ndiyo iliyo baada ya Maandalio, wakuu wa makuhani, na Mafarisayo wakamkusanyikia Pilato,

Mathayo 27:63 Matthew 27:63

wakasema, Bwana, tumekumbuka kwamba yule mjanja alisema, alipokuwa akali hai, Baada ya siku tatu nitafufuka.

Mathayo 27:64 Matthew 27:64

Basi amuru kwamba kaburi lilindwe salama hata siku ya tatu; wasije wanafunzi wake wakamwiba, na kuwaambia watu, Amefufuka katika wafu; na udanganyifu wa mwisho utapita ule wa kwanza.

Mathayo 27:65 Matthew 27:65

Pilato akawaambia, Mna askari; nendeni mkalilinde salama kadiri mjuavyo.

Mathayo 27:66 Matthew 27:66

Wakaenda, wakalilinda kaburi salama, kwa kulitia lile jiwe muhuri, pamoja na wale askari walinzi.