Mwanzo Mlango 2 Genesis

Mwanzo 2:1 Genesis 2:1

Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote.

Mwanzo 2:2 Genesis 2:2

Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya.

Mwanzo 2:3 Genesis 2:3

Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.

Mwanzo 2:4 Genesis 2:4

Hivyo ndivyo vizazi vya mbingu na nchi zilipoumbwa. Siku ile Bwana Mungu alipoziumba mbingu na nchi

Mwanzo 2:5 Genesis 2:5

hapakuwa na mche wa kondeni bado, wala mboga ya kondeni haijachipuka bado, kwa maana Bwana Mungu hajainyeshea nchi mvua, wala hapana mtu wa kuilima ardhi;

Mwanzo 2:6 Genesis 2:6

ukungu ukapanda katika nchi, ukatia maji juu ya uso wote wa ardhi.

Mwanzo 2:7 Genesis 2:7

Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.

Mwanzo 2:8 Genesis 2:8

Bwana Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.

Mwanzo 2:9 Genesis 2:9

Bwana Mungu akachipusha katika ardhi kila mti unaotamanika kwa macho na kufaa kwa kuliwa; na mti wa uzima katikati ya bustani, na mti wa ujuzi wa mema na mabaya.

Mwanzo 2:10 Genesis 2:10

Ukatoka mto katika Edeni wa kuitilia bustani maji, na kutokea hapo ukagawanyika kuwa vichwa vinne.

Mwanzo 2:11 Genesis 2:11

Jina la wa kwanza ni Pishoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Havila, ambako kuna dhahabu;

Mwanzo 2:12 Genesis 2:12

na dhahabu ya nchi ile ni njema; huko kuna bedola, na vito shoham.

Mwanzo 2:13 Genesis 2:13

Na jina la mto wa pili ni Gihoni; ndio unaozunguka nchi yote ya Kushi.

Mwanzo 2:14 Genesis 2:14

Na jina la mto wa tatu ni Hidekeli; ndio unaopita mbele ya Ashuru. Na mto wa nne ni Frati.

Mwanzo 2:15 Genesis 2:15

Bwana Mungu akamtwaa huyo mtu, akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza.

Mwanzo 2:16 Genesis 2:16

Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula,

Mwanzo 2:17 Genesis 2:17

walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika.

Mwanzo 2:18 Genesis 2:18

Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye.

Mwanzo 2:19 Genesis 2:19

Bwana Mungu akafanyiza kutoka katika ardhi kila mnyama wa msituni, na kila ndege wa angani, akamletea Adamu ili aone atawaitaje; kila kiumbe hai, jina alilokiita Adamu likawa ndilo jina lake.

Mwanzo 2:20 Genesis 2:20

Adamu akawapa majina yao kila mnyama wa kufugwa, na ndege wa angani, na kila mnyama wa mwituni; lakini hakuonekana wa kumsaidia Adamu aliyefanana naye.

Mwanzo 2:21 Genesis 2:21

Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake,

Mwanzo 2:22 Genesis 2:22

na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu.

Mwanzo 2:23 Genesis 2:23

Adamu akasema, Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu, basi ataitwa mwanamke, kwa maana ametwaliwa katika mwanamume.

Mwanzo 2:24 Genesis 2:24

Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja.

Mwanzo 2:25 Genesis 2:25

Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya.