Mwanzo Mlango 45 Genesis

Mwanzo 45:1 Genesis 45:1

Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze.

Mwanzo 45:2 Genesis 45:2

Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia.

Mwanzo 45:3 Genesis 45:3

Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake.

Mwanzo 45:4 Genesis 45:4

Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri.

Mwanzo 45:5 Genesis 45:5

Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu.

Mwanzo 45:6 Genesis 45:6

Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna.

Mwanzo 45:7 Genesis 45:7

Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu.

Mwanzo 45:8 Genesis 45:8

Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri.

Mwanzo 45:9 Genesis 45:9

Fanyeni haraka, mmwendee baba yangu, mkamwambie, Hivi ndivyo asemavyo mwanao Yusufu, Mungu ameniweka kuwa bwana katika Misri yote, basi unishukie, usikawie.

Mwanzo 45:10 Genesis 45:10

Nawe utakaa katika nchi ya Gosheni, utakuwa karibu nami, wewe, na wanao, na wana wa wanao, na wanyama wako, ng'ombe zako, na yote uliyo nayo. Nami nitakulisha huko;

Mwanzo 45:11 Genesis 45:11

maana bado imesalia miaka mitano ya njaa; usije ukaingia katika uhitaji, wewe, na nyumba yako, na yote uliyo nayo.

Mwanzo 45:12 Genesis 45:12

Na tazama, macho yenu yanaona, na macho ya ndugu yangu Benyamini, ya kwamba ni kinywa changu mimi kinachosema nanyi.

Mwanzo 45:13 Genesis 45:13

Nanyi mtamwarifu baba yangu habari za fahari yangu yote katika Misri, na za vyote mlivyoviona; mkafanye haraka kumleta huku baba yangu.

Mwanzo 45:14 Genesis 45:14

Akaanguka shingoni mwa ndugu yake Benyamini, akalia; Benyamini naye akalia shingoni mwake.

Mwanzo 45:15 Genesis 45:15

Akawabusu ndugu zake wote, akalia nao, baada ya hayo, nduguze wakazungumza naye

Mwanzo 45:16 Genesis 45:16

Habari ikasikika nyumbani mwa Farao kusema, Ndugu zake Yusufu wamekuja. Ikawa vema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake.

Mwanzo 45:17 Genesis 45:17

Farao akamwambia Yusufu, Uwaambie ndugu zako, Fanyeni hivi; wachukuzeni mizigo wanyama wenu, mwondoke mwende nchi ya Kanaani;

Mwanzo 45:18 Genesis 45:18

kisha mkamtwae baba yenu, na watu wa nyumbani mwenu, mkanijie; nami nitawapa mema ya nchi ya Misri, nanyi mtakula unono wa nchi.

Mwanzo 45:19 Genesis 45:19

Nawe umeamriwa; fanyeni hivi, mjitwalie magari katika nchi ya Misri kwa watoto wenu wadogo na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje.

Mwanzo 45:20 Genesis 45:20

Wala msivisumbukie vyombo vyenu, maana mema ya nchi yote ya Misri ni yenu.

Mwanzo 45:21 Genesis 45:21

Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli. Yusufu akawapa magari kama Farao alivyoamuru, akawapa na chakula cha njiani.

Mwanzo 45:22 Genesis 45:22

Akawapa kila mtu nguo za kubadili; lakini Benyamini, alimpa fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili.

Mwanzo 45:23 Genesis 45:23

Na babaye akampelekea kama hivi, punda kumi waliochukua mema ya Misri, na punda wake kumi waliochukua nafaka, na mikate, na chakula kwa babaye njiani.

Mwanzo 45:24 Genesis 45:24

Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao; naye akawaambia, Msigombane njiani.

Mwanzo 45:25 Genesis 45:25

Wakatoka Misri, wakafika nchi ya Kanaani kwa Yakobo, baba yao.

Mwanzo 45:26 Genesis 45:26

Wakampasha habari, wakisema, Yusufu angali hai; naye ndiye mtawala katika nchi yote ya Misri. Moyo wake ukazimia, kwa sababu hakuwasadiki.

Mwanzo 45:27 Genesis 45:27

Wakamwambia maneno yote ya Yusufu, aliyowaambia; na alipoona magari aliyoyapeleka Yusufu, ili kumchukua, roho ya Yakobo baba yao ikafufuka.

Mwanzo 45:28 Genesis 45:28

Israeli akasema, Yatosha! Yusufu mwanangu angali hai; nitakwenda, nionane naye kabla sijafa.