Mwanzo Mlango 4 Genesis

Mwanzo 4:1 Genesis 4:1

Adamu akamjua Hawa mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, Nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana.

Mwanzo 4:2 Genesis 4:2

Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi.

Mwanzo 4:3 Genesis 4:3

Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana.

Mwanzo 4:4 Genesis 4:4

Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake;

Mwanzo 4:5 Genesis 4:5

bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.

Mwanzo 4:6 Genesis 4:6

Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?

Mwanzo 4:7 Genesis 4:7

Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.

Mwanzo 4:8 Genesis 4:8

Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani,Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua.

Mwanzo 4:9 Genesis 4:9

Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?

Mwanzo 4:10 Genesis 4:10

Akasema, Umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi.

Mwanzo 4:11 Genesis 4:11

Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako;

Mwanzo 4:12 Genesis 4:12

utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani.

Mwanzo 4:13 Genesis 4:13

Kaini akamwambia Bwana, Adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki.

Mwanzo 4:14 Genesis 4:14

Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua.

Mwanzo 4:15 Genesis 4:15

Bwana akamwambia, Kwa sababu hiyo ye yote atakayemwua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga.

Mwanzo 4:16 Genesis 4:16

Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, akakaa katika nchi ya Nodi, mbele ya Edeni.

Mwanzo 4:17 Genesis 4:17

Kaini akamjua mkewe; naye akapata mimba, akamzaa Henoko; akajenga mji akauita Henoko, kwa jina la mwanawe.

Mwanzo 4:18 Genesis 4:18

Henoko akamzaa Iradi, Iradi akamzaa Mehuyaeli; Mehuyaeli akamzaa Methushaeli; Methushaeli akamzaa Lameki.

Mwanzo 4:19 Genesis 4:19

Lameki akajitwalia wake wawili, jina la wa kwanza ni Ada, na jina la wa pili ni Sila.

Mwanzo 4:20 Genesis 4:20

Ada akamzaa Yabali; huyo ndiye baba yao wakaao katika hema na kufuga wanyama.

Mwanzo 4:21 Genesis 4:21

Na jina la nduguye aliitwa Yubali; huyo ndiye baba yao wapigao kinubi na filimbi.

Mwanzo 4:22 Genesis 4:22

Sila naye akamzaa Tubal-kaini, mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma; na umbu lake Tubal-kaini alikuwa Naama.

Mwanzo 4:23 Genesis 4:23

Lameki akawaambia wake zake, Sikieni sauti yangu, Ada na Sila; Enyi wake za Lameki, sikilizeni usemi wangu; Maana nimemwua mtu kwa kunitia jeraha; Kijana kwa kunichubua;

Mwanzo 4:24 Genesis 4:24

Kama Kaini akilipiwa kisasi mara saba, Hakika Lameki atalipiwa mara sabini na saba.

Mwanzo 4:25 Genesis 4:25

Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.

Mwanzo 4:26 Genesis 4:26

Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la Bwana.