Mwanzo Mlango 29 Genesis

Mwanzo 29:1 Genesis 29:1

Kisha Yakobo akashika njia yake, akafika nchi ya wana wa mashariki.

Mwanzo 29:2 Genesis 29:2

Naye akaangalia, na tazama, kiko kisima kondeni, na makundi matatu ya kondoo yamelala karibu nacho, kwa sababu katika kisima kile hunywesha makundi; na palikuwa na jiwe kubwa juu ya kinywa cha kisima.

Mwanzo 29:3 Genesis 29:3

Makundi yote hukusanyika huko, watu wakafingirisha hilo jiwe katika kinywa cha kisima wakawanywesha kondoo, na kulirudisha jiwe juu ya kinywa cha kisima mahali pake.

Mwanzo 29:4 Genesis 29:4

Yakobo akawauliza, Ndugu zangu, watu wa wapi ninyi? Wakasema, Tu wa Harani sisi.

Mwanzo 29:5 Genesis 29:5

Akawauliza, Je! Mnamjua Labani, mwana wa Nahori? Wakasema, Tunamjua.

Mwanzo 29:6 Genesis 29:6

Akawauliza, Je! Hajambo? Wakasema, Hajambo; tazama, Raheli binti yake anakuja na kondoo.

Mwanzo 29:7 Genesis 29:7

Akasema, Tazama, ukali mchana bado, wala sio wakati wa kukusanya wanyama; wanywesheni kondoo, mwende kuwalisha.

Mwanzo 29:8 Genesis 29:8

Wakasema, Hatuwezi, hata yakusanyike makundi yote, watu wakafingirishe jiwe katika kinywa cha kisima, ndipo tunapowanywesha kondoo.

Mwanzo 29:9 Genesis 29:9

Hata alipokuwa akisema nao, Raheli akaja na kondoo za baba yake, maana aliwachunga.

Mwanzo 29:10 Genesis 29:10

Ikawa Yakobo alipomwona Raheli binti Labani, ndugu wa mamaye, na kondoo za Labani, ndugu wa mamaye, Yakobo akakaribia, na kulifingirisha lile jiwe litoke katika kinywa cha kisima, akawanywesha kondoo za Labani, ndugu wa mamaye.

Mwanzo 29:11 Genesis 29:11

Yakobo akambusu Raheli, akainua sauti yake akalia.

Mwanzo 29:12 Genesis 29:12

Yakobo akamwarifu Raheli ya kuwa yeye ni ndugu wa babaye, na ya kuwa ni mwana wa Rebeka. Basi akapiga mbio akampasha babaye habari.

Mwanzo 29:13 Genesis 29:13

Ikawa Labani aliposikia habari za Yakobo, mwana wa nduguye, akaenda mbio amlaki, akamkumbatia, akambusu, akamleta nyumbani kwake. Naye akamwambia Labani maneno hayo yote.

Mwanzo 29:14 Genesis 29:14

Labani akamwambia, Ndiwe kweli mfupa wangu na nyama yangu. Naye akakaa kwake muda wa mwezi mmoja.

Mwanzo 29:15 Genesis 29:15

Labani akamwambia Yakobo, Kwa sababu wewe ni ndugu yangu, basi, je! Unitumikie bure? Niambie mshahara wako utakuwa nini?

Mwanzo 29:16 Genesis 29:16

Labani alikuwa na binti wawili, jina la mkubwa ni Lea, na jina la mdogo ni Raheli.

Mwanzo 29:17 Genesis 29:17

Naye Lea macho yake yalikuwa dhaifu, lakini Raheli alikuwa mzuri wa umbo, na mzuri uso.

Mwanzo 29:18 Genesis 29:18

Yakobo akampenda Raheli akasema, Nitakutumikia miaka saba kwa kumpata Raheli, binti yako mdogo.

Mwanzo 29:19 Genesis 29:19

Labani akasema, Afadhali nikupe wewe kuliko mtu mwingine; kaa kwangu.

Mwanzo 29:20 Genesis 29:20

Yakobo akatumika miaka saba kwa kumpata Raheli. Ikawa machoni pake kama siku chache tu kwa vile alivyompenda.

Mwanzo 29:21 Genesis 29:21

Yakobo akamwambia Labani, Nipe mke wangu, maana siku zangu zimetimia; niingie kwake.

Mwanzo 29:22 Genesis 29:22

Labani akakusanya watu wote wa mahali pale, akafanya karamu.

Mwanzo 29:23 Genesis 29:23

Ikawa wakati wa jioni akamtwaa Lea, binti yake, akamletea Yakobo, naye akaingia kwake.

Mwanzo 29:24 Genesis 29:24

Labani akampa Lea mjakazi wake Zilpa, awe mjakazi wake.

Mwanzo 29:25 Genesis 29:25

Ikawa, kulipokuwa asubuhi, kumbe! Ni Lea. Akamwambia Labani, Nini hii uliyonitenda?

Mwanzo 29:26 Genesis 29:26

Sikukutumikia kwa Raheli? Mbona umenidanganya? Labani akasema, Havitendeki hivi kwetu, kumtoa mdogo kabla ya mkubwa;

Mwanzo 29:27 Genesis 29:27

timiza siku zake saba, nasi tutakupa huyu naye kwa utumishi utakaonitumikia, miaka saba mingine.

Mwanzo 29:28 Genesis 29:28

Yakobo akafanya hivi, akatimiza siku zake saba. Naye akampa Raheli binti yake kuwa mkewe.

Mwanzo 29:29 Genesis 29:29

Labani akampa binti yake Raheli mjakazi wake Bilha, awe mjakazi wake.

Mwanzo 29:30 Genesis 29:30

Akaingia kwa Raheli naye, akampenda Raheli kuliko Lea, akatumika kwa ajili yake miaka saba mingine.

Mwanzo 29:31 Genesis 29:31

Bwana akaona ya kwamba Lea hakupendwa, naye akafungua tumbo lake; bali Raheli alikuwa hazai.

Mwanzo 29:32 Genesis 29:32

Lea akapata mimba akazaa mwana, akampa jina lake, Reubeni, maana alisema, Kwa kuwa Bwana ameona teso langu; sasa mume wangu atanipenda.

Mwanzo 29:33 Genesis 29:33

Akapata mimba tena akazaa mwana, akasema, Kwa kuwa Bwana amesikia ya kwamba mimi sikupendwa, amenipa na huyu; akamwita jina lake Simeoni.

Mwanzo 29:34 Genesis 29:34

Akapata mimba tena, akazaa mwana, akasema, Basi wakati huu mume wangu ataungana nami, kwa sababu nimemzalia wana watatu. Kwa hiyo akamwita jina lake Lawi.

Mwanzo 29:35 Genesis 29:35

Akapata mimba tena, akazaa mwana. Akasema, Mara hii nitamsifu Bwana; kwa hiyo akamwita jina lake Yuda; akaacha kuzaa.