Mwanzo Mlango 31 Genesis

Mwanzo 31:1 Genesis 31:1

Basi Yakobo akasikia maneno ya wana wa Labani, wakisema, Yakobo amechukua mali yote ya baba yetu; na kwa mali ya baba yetu amepata fahari hii yote.

Mwanzo 31:2 Genesis 31:2

Yakobo akaona uso wa Labani, ya kuwa hakumtazama vema kama jana na juzi.

Mwanzo 31:3 Genesis 31:3

Bwana akamwambia Yakobo, Urudi mpaka nchi ya baba zako na kwa jamaa zako, nami nitakuwa pamoja nawe.

Mwanzo 31:4 Genesis 31:4

Yakobo akatuma watu, akawaita Raheli na Lea waje nyikani kwenye wanyama wake. Akawaambia,

Mwanzo 31:5 Genesis 31:5

Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami.

Mwanzo 31:6 Genesis 31:6

Nanyi mmejua ya kwamba kwa nguvu zangu zote nimemtumikia baba yenu.

Mwanzo 31:7 Genesis 31:7

Na baba yenu amenidanganya, akabadili mshahara wangu mara kumi; lakini Mungu hakumwacha kunidhuru.

Mwanzo 31:8 Genesis 31:8

Aliposema, Walio na madoadoa watakuwa mshahara wako, wanyama wote wakazaa madoadoa. Aliposema, Walio na milia watakuwa mshahara wako, ndipo wanyama wote wakazaa wenye milia.

Mwanzo 31:9 Genesis 31:9

Hivi Mungu akamnyang'anya mali yake baba yenu, na kunipa mimi.

Mwanzo 31:10 Genesis 31:10

Ikawa, wakati wale wanyama walipochukua mimba, naliinua macho yangu nikaona katika ndoto, na tazama, mabeberu waliowapanda hao wanyama walikuwa na milia, na madoadoa, na marakaraka.

Mwanzo 31:11 Genesis 31:11

Na malaika wa Mungu akaniambia katika ndoto, Yakobo! Nikasema, Mimi hapa.

Mwanzo 31:12 Genesis 31:12

Akasema, Inua, basi, macho yako, ukaone; mabeberu wote wanaopanda wanyama wana milia, na madoadoa, na marakaraka; maana nimeona yote aliyokutendea Labani.

Mwanzo 31:13 Genesis 31:13

Mimi ni Mungu wa Betheli, huko ulikotia mafuta nguzo, na kuniwekea nadhiri. Sasa ondoka, toka katika nchi hii, urudi mpaka nchi ile uliyozaliwa.

Mwanzo 31:14 Genesis 31:14

Raheli na Lea wakajibu, wakamwambia, Je! Imetubakia sehemu au urithi katika nyumba ya baba yetu?

Mwanzo 31:15 Genesis 31:15

Hakutufanya kama wageni, maana ametuuza, naye amekula fedha zetu kabisa?

Mwanzo 31:16 Genesis 31:16

Maana mali yote ambayo Mungu amemnyang'anya baba yetu, mali hiyo ndiyo yetu na ya wana wetu. Basi yo yote Mungu aliyokuambia, uyafanye.

Mwanzo 31:17 Genesis 31:17

Ndipo Yakobo akaondoka, akapandisha wanawe na wakeze juu ya ngamia.

Mwanzo 31:18 Genesis 31:18

Akachukua wanyama wake wote, na mali yake yote aliyokuwa ameyapata, na wanyama aliowapata katika Padan-aramu, ili afike kwa Isaka babaye katika nchi ya Kanaani.

Mwanzo 31:19 Genesis 31:19

Basi Labani alikuwa amekwenda kuwakata manyoya kondoo zake, na Raheli akaviiba vinyago vya babaye.

Mwanzo 31:20 Genesis 31:20

Yakobo akamhadaa Labani, Mshami, kwa kuwa hakumwambia ya kwamba anakimbia.

Mwanzo 31:21 Genesis 31:21

Basi akakimbia yeye na yote aliyokuwa nayo; akaondoka akauvuka mto, akaelekeza uso wake kwenda mlima wa Gileadi.

Mwanzo 31:22 Genesis 31:22

Hata siku ya tatu Labani akaambiwa ya kwamba Yakobo amekimbia,

Mwanzo 31:23 Genesis 31:23

akatwaa ndugu zake pamoja naye, akamfuata mwendo wa siku saba. Akampata katika mlima wa Gileadi.

Mwanzo 31:24 Genesis 31:24

Mungu akamjia Labani, Mshami, katika ndoto ya usiku, akamwambia, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.

Mwanzo 31:25 Genesis 31:25

Labani akamfikia Yakobo, na Yakobo alikuwa amepiga hema zake katika mlima, na Labani na ndugu zake wakapiga hema zao katika mlima wa Gileadi.

Mwanzo 31:26 Genesis 31:26

Labani akamwambia Yakobo, Umefanya nini? Umenihadaa, ukawachukua binti zangu kama mateka waliotwaliwa kwa upanga.

Mwanzo 31:27 Genesis 31:27

Mbona umekimbia kwa siri ukanihadaa, wala hukuniambia, nipate kuagana nawe uende zako kwa furaha, na nyimbo, na ngoma, na kinubi?

Mwanzo 31:28 Genesis 31:28

Wala hukuniacha niwabusu wanangu, na binti zangu; basi umetenda upumbavu.

Mwanzo 31:29 Genesis 31:29

Ninao uwezo mkononi mwangu wa kukufanyia madhara; lakini Mungu wa baba yako usiku huu ameniambia, akisema, Ujihadhari, usimwambie Yakobo neno la heri wala la shari.

Mwanzo 31:30 Genesis 31:30

Basi sasa, umetoka kwa sababu umetamani sana nyumba ya baba yako. Mbona basi umeiiba miungu yangu?

Mwanzo 31:31 Genesis 31:31

Yakobo akajibu, akamwambia Labani, Kwa sababu naliogopa, nikasema, Usije ukaninyang'anya binti zako kwa nguvu.

Mwanzo 31:32 Genesis 31:32

Awaye yote utakayemwona kuwa nayo miungu yako, yeye asiishi. Mbele ya ndugu zetu ukitambue kilicho chako kwangu, ukakichukue. Maana Yakobo hakujua ya kwamba Raheli ameiiba.

Mwanzo 31:33 Genesis 31:33

Labani akaingia katika hema ya Yakobo, na hema ya Lea, na hema ya vijakazi wawili, wala hakuiona. Akatoka katika hema ya Lea, akaingia katika hema ya Raheli.

Mwanzo 31:34 Genesis 31:34

Basi Raheli alikuwa amevitwaa vile vinyago ameviweka katika matandiko ya ngamia, na kuvikalia. Labani akapapasa hema yote wala hakuviona.

Mwanzo 31:35 Genesis 31:35

Naye Raheli akamwambia babaye, Bwana wangu asikasirike kwa sababu siwezi kuinuka mbele yako, maana nimeshikwa na mambo ya kike. Akatafuta, wala hakuviona vile vinyago.

Mwanzo 31:36 Genesis 31:36

Yakobo akakasirika, akagombana na Labani. Yakobo akajibu, akamwambia Labani, N'nini hatia yangu? Nayo ni nini dhambi yangu, hata ukanifuatia namna hii?

Mwanzo 31:37 Genesis 31:37

Umepapasa-papasa vyombo vyangu vyote; ni kitu gani ulichokiona cha nyumbani mwako? Kiweke hapa mbele ya ndugu zangu, na ndugu zako, wakaamue kati yetu.

Mwanzo 31:38 Genesis 31:38

Miaka hii ishirini nimekaa kwako; kondoo zako wala mbuzi zako wake hawakuharibu mimba wala waume katika wanyama wako sikuwala.

Mwanzo 31:39 Genesis 31:39

Kilichoraruliwa na hayawani sikukuletea, mimi mwenyewe nimetwaa hasara yake, wewe umekidai katika mkono wangu, ikiwa kilichukuliwa mchana, au ikiwa kilichukuliwa usiku.

Mwanzo 31:40 Genesis 31:40

Hii ilikuwa hali yangu; mchana jua likanipata, na baridi usiku, usingizi ukanitoka machoni mwangu.

Mwanzo 31:41 Genesis 31:41

Miaka hii ishirini nimekaa nyumbani mwako; nilikutumikia miaka kumi na minne kwa binti zako wawili, na miaka sita kwa wanyama wako, nawe umebadili mshahara wangu mara kumi.

Mwanzo 31:42 Genesis 31:42

Kama Mungu wa baba yangu, Mungu wa Ibrahimu na Hofu ya Isaka, hangalikuwa pamoja nami, hakika sasa ungalinifukuza mikono mitupu. Mateso yangu na kazi za mikono yangu Mungu ameziona, akakukemea usiku huu.

Mwanzo 31:43 Genesis 31:43

Labani akajibu, akamwambia Yakobo, Hao binti ni binti zangu, na wana ni wanangu, na wanyama ni wanyama wangu, na yote uyaonayo ni yangu; nami naweza kuwatendea nini leo binti zangu na wana wao waliowalea?

Mwanzo 31:44 Genesis 31:44

Haya! Na tufanye agano, mimi na wewe, liwe kwa ushahidi kati ya mimi na wewe.

Mwanzo 31:45 Genesis 31:45

Yakobo akatwaa jiwe akalisimamisha kama nguzo.

Mwanzo 31:46 Genesis 31:46

Yakobo akawaambia ndugu zake, Kusanyeni mawe. Wakatwaa mawe, wakafanya chungu, nao wakala huko karibu na ile chungu.

Mwanzo 31:47 Genesis 31:47

Labani aliiita Yegarsahadutha, lakini Yakobo aliiita Galedi.

Mwanzo 31:48 Genesis 31:48

Labani akasema, Chungu hii ni shahidi kati ya mimi na wewe hivi leo. Kwa hiyo likaitwa jina lake Galedi,

Mwanzo 31:49 Genesis 31:49

na Mispa, maana alisema, Mungu avizie kati ya mimi na wewe, wakati tusipoonana.

Mwanzo 31:50 Genesis 31:50

Ukiwatesa binti zangu, na ukitwaa wake zaidi ya binti zangu, wala hapana mtu pamoja nasi, tazama, Mungu ni shahidi kati ya mimi na wewe.

Mwanzo 31:51 Genesis 31:51

Labani akamwambia Yakobo, Tazama chungu hii utazame na nguzo niliyoitia kati ya mimi na wewe.

Mwanzo 31:52 Genesis 31:52

Chungu hii na iwe shahidi, na nguzo hii na iwe shahidi, ya kuwa mimi sitapita chungu hii kuja kwako, wala wewe hutapita chungu hii na nguzo hii uje kwangu, kwa madhara.

Mwanzo 31:53 Genesis 31:53

Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Nahori, Mungu wa baba yao, ahukumu kati yetu.

Mwanzo 31:54 Genesis 31:54

Yakobo akachinja sadaka katika mlima, akawaita ndugu zake waje wale chakula, nao wakala chakula, wakakaa usiku kucha mlimani.

Mwanzo 31:55 Genesis 31:55

Labani akaondoka asubuhi na mapema, akawabusu wanawe na binti zake, akawabariki; kisha Labani akaenda zake, akarudi kwao.