Mwanzo Mlango 41 Genesis

Mwanzo 41:1 Genesis 41:1

Ikawa, mwisho wa miaka miwili mizima, Farao akaota ndoto; na tazama, amesimama kando ya mto.

Mwanzo 41:2 Genesis 41:2

Na tazama, ng'ombe saba wazuri, wanono, walipanda kutoka mtoni, wakajilisha manyasini.

Mwanzo 41:3 Genesis 41:3

Na tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda nyuma yao kutoka mtoni, wabaya, wamekonda, wakasimama karibu na wale ng'ombe wengine ukingoni mwa mto.

Mwanzo 41:4 Genesis 41:4

Kisha hao ng'ombe wabaya waliokonda wakawala wale ng'ombe saba wazuri, wanono. Basi Farao akaamka.

Mwanzo 41:5 Genesis 41:5

Akalala, akaota ndoto mara ya pili. Tazama, masuke saba yalimea katika bua moja, makubwa, mema.

Mwanzo 41:6 Genesis 41:6

Na tazama, masuke saba membamba, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao.

Mwanzo 41:7 Genesis 41:7

Kisha hayo masuke membamba saba yakayala yale masuke saba makubwa yaliyojaa. Basi Farao akaamka, kumbe! Ni ndoto tu.

Mwanzo 41:8 Genesis 41:8

Hata asubuhi roho yake ikafadhaika; akapeleka watu kuwaita waganga wote wa Misri, na watu wote wenye hekima walioko. Farao akawahadithia ndoto yake, wala hakuna aliyeweza kumfasiria Farao mambo hayo.

Mwanzo 41:9 Genesis 41:9

Basi mkuu wa wanyweshaji akamwambia Farao akisema, Nayakumbuka makosa yangu leo.

Mwanzo 41:10 Genesis 41:10

Farao aliwakasirikia watumwa wake, akanitia nifungwe nyumbani mwa mkuu wa askari, mimi na mkuu wa waokaji.

Mwanzo 41:11 Genesis 41:11

Tukaota ndoto usiku mmoja, mimi na yeye; kila mtu kwa tafsiri ya ndoto yake tukaota.

Mwanzo 41:12 Genesis 41:12

Na huko pamoja nasi palikuwa na kijana; Mwebrania, mtumishi wa mkuu wa askari, tukamhadithia, naye akatufasiria ndoto zetu; akamfasiria kila mtu kama ilivyokuwa ndoto yake.

Mwanzo 41:13 Genesis 41:13

Ikawa, kama vile alivyotufasiria ndivyo ilivyotokea; mimi nalirudishwa katika kazi yangu, na yeye alitundikwa.

Mwanzo 41:14 Genesis 41:14

Ndipo Farao akapeleka watu, akamwita Yusufu, wakamleta upesi kutoka gerezani. Akanyoa, akabadili nguo zake, na kuingia kwa Farao.

Mwanzo 41:15 Genesis 41:15

Farao akamwambia Yusufu, Nimeota ndoto, wala hakuna awezaye kunifasiria; nami nimesikia habari zako, ya kwamba, usikiapo ndoto, waweza kuifasiri.

Mwanzo 41:16 Genesis 41:16

Yusufu akamjibu Farao, akisema, Si mimi; Mungu atampa Farao majibu ya amani.

Mwanzo 41:17 Genesis 41:17

Farao akamwambia Yusufu, Katika ndoto yangu nalikuwa nikisimama ukingoni mwa mto;

Mwanzo 41:18 Genesis 41:18

na tazama, ng'ombe saba wanatoka mtoni, wanono, wazuri, wakajilisha manyasini.

Mwanzo 41:19 Genesis 41:19

Kisha, tazama, ng'ombe saba wengine wakapanda baada yao, dhaifu, wabaya sana, wamekonda; katika nchi yote ya Misri sijaona kama hao kwa udhaifu.

Mwanzo 41:20 Genesis 41:20

Na hao ng'ombe waliokonda, wabaya, wakawala wale ng'ombe saba wa kwanza, wale wanono.

Mwanzo 41:21 Genesis 41:21

Na walipokwisha kuwala haikutambulikana ya kwamba wamewala, bali wakaonekana wabaya kama kwanza. Basi nikaamka.

Mwanzo 41:22 Genesis 41:22

Kisha nikaona katika ndoto yangu, na tazama, masuke saba yanatokeza katika bua moja, mema, yamejaa.

Mwanzo 41:23 Genesis 41:23

Na tazama, masuke saba membamba, dhaifu, yamekaushwa na upepo wa mashariki, yakatokeza baada yao.

Mwanzo 41:24 Genesis 41:24

Na hayo masuke dhaifu yakameza yale masuke saba mema. Nami nikawaambia hao waganga, wala hakuna aliyeweza kunionyesha maana yake.

Mwanzo 41:25 Genesis 41:25

Yusufu akamwambia Farao, Ndoto ya Farao ni moja; Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.

Mwanzo 41:26 Genesis 41:26

Wale ng'ombe saba wema ni miaka saba; na yale masuke saba mema ni miaka saba. Ndoto ni moja.

Mwanzo 41:27 Genesis 41:27

Na wale ng'ombe saba, dhaifu, wabaya, waliopanda baada yao, ni miaka saba; na yale masuke saba matupu yaliyokaushwa na upepo wa mashariki, yatakuwa miaka saba ya njaa.

Mwanzo 41:28 Genesis 41:28

Ndivyo nilivyomwambia Farao, ya kwamba Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibu.

Mwanzo 41:29 Genesis 41:29

Tazama, miaka saba ya shibe inakuja, katika nchi yote ya Misri.

Mwanzo 41:30 Genesis 41:30

Kisha kutakuja miaka saba ya njaa baada yake; na shibe ile yote itasahauliwa katika nchi ya Misri, na njaa itaiharibu nchi.

Mwanzo 41:31 Genesis 41:31

Wala shibe ile haitajulikana katika nchi kwa sababu ya njaa inayokuja baadaye, maana itakuwa nzito sana.

Mwanzo 41:32 Genesis 41:32

Na ndoto ya Farao kwa vile ilivyokuja mara mbili, ni kwa sababu neno hilo Mungu amelithibitisha, na Mungu atalitimiza upesi.

Mwanzo 41:33 Genesis 41:33

Basi, Farao na ajitafutie mtu wa akili na hekima amweke juu ya nchi ya Misri.

Mwanzo 41:34 Genesis 41:34

Farao na afanye hivi, tena akaweke wasimamizi juu ya nchi, na kutwaa sehemu ya tano katika nchi ya Misri, katika miaka hii saba ya kushiba.

Mwanzo 41:35 Genesis 41:35

Na wakusanye chakula chote cha miaka hii myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika miji.

Mwanzo 41:36 Genesis 41:36

Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa.

Mwanzo 41:37 Genesis 41:37

Neno hilo likawa jema machoni pa Farao, na machoni pa watumwa wake wote.

Mwanzo 41:38 Genesis 41:38

Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake?

Mwanzo 41:39 Genesis 41:39

Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe.

Mwanzo 41:40 Genesis 41:40

Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.

Mwanzo 41:41 Genesis 41:41

Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri.

Mwanzo 41:42 Genesis 41:42

Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake.

Mwanzo 41:43 Genesis 41:43

Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri.

Mwanzo 41:44 Genesis 41:44

Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.

Mwanzo 41:45 Genesis 41:45

Farao akamwita Yusufu, Safenath-panea; akamwoza Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, kuwa mkewe Yusufu akaenda huko na huko katika nchi yote ya Misri.

Mwanzo 41:46 Genesis 41:46

Naye Yusufu alikuwa mwenye miaka thelathini, aliposimama mbele ya Farao, mfalme wa Misri. Yusufu akatoka mbele ya uso wa Farao, akapita katika nchi yote ya Misri.

Mwanzo 41:47 Genesis 41:47

Ikawa katika miaka ile saba ya shibe, nchi ikazaa kwa wingi.

Mwanzo 41:48 Genesis 41:48

Akakusanya chakula chote cha miaka ile saba katika nchi ya Misri. Akaweka chakula katika miji; chakula cha mashamba yaliyouzunguka kila mji, akakiweka ndani yake.

Mwanzo 41:49 Genesis 41:49

Yusufu akakusanya nafaka kama mchanga wa pwani, nyingi mno, hata akaacha kuhesabu, maana ilikuwa haina hesabu.

Mwanzo 41:50 Genesis 41:50

Kabla ya kuja miaka ya njaa, Yusufu akazaliwa wana wawili, ambao Asenathi, binti Potifera, kuhani wa Oni, alimzalia.

Mwanzo 41:51 Genesis 41:51

Yusufu akamwita jina lake yule aliyezaliwa kwanza, Manase, maana alisema, Mungu amenisahaulisha taabu zangu zote, na nyumba yote ya baba yangu.

Mwanzo 41:52 Genesis 41:52

Na wa pili akamwita jina lake Efraimu, maana alisema, Mungu amenipa uzazi katika nchi ya mateso yangu.

Mwanzo 41:53 Genesis 41:53

Miaka ile saba ya shibe ikaisha katika nchi ya Misri,

Mwanzo 41:54 Genesis 41:54

ikaanza kuja miaka ile saba ya njaa, kama vile Yusufu alivyosema. Kukawa na njaa katika nchi zote, bali katika nchi yote ya Misri palikuwa na chakula.

Mwanzo 41:55 Genesis 41:55

Na nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walimlilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote, Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni.

Mwanzo 41:56 Genesis 41:56

Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri.

Mwanzo 41:57 Genesis 41:57

Watu wa nchi zote wakaja Misri kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote.