Mwanzo Mlango 32 Genesis

Mwanzo 32:1 Genesis 32:1

Yakobo akashika njia yake na malaika wa Mungu wakakutana naye.

Mwanzo 32:2 Genesis 32:2

Naye Yakobo alipowaona, alisema, Hili ni jeshi la Mungu. Akapaita mahali pale, Mahanaimu.

Mwanzo 32:3 Genesis 32:3

Basi, Yakobo akapeleka wajumbe mbele yake kwenda kwa Esau nduguye mpaka nchi ya Seiri katika nyika ya Edomu.

Mwanzo 32:4 Genesis 32:4

Akawaagiza akisema, Mwambieni hivi bwana wangu, Esau, Hivi ndivyo asemavyo mtumwa wako, Yakobo; Nimekaa ugenini kwa Labani, na kukawia huko hata sasa,

Mwanzo 32:5 Genesis 32:5

nami nina ng'ombe, na punda, na kondoo, na watumwa, na vijakazi; nami nimepeleka watu nimpashe bwana wangu habari, nipate neema machoni pako.

Mwanzo 32:6 Genesis 32:6

Wale wajumbe wakarudi kwa Yakobo wakisema, Tulifika kwa ndugu yako, Esau, naye anakuja kukulaki, na watu mia nne pamoja naye.

Mwanzo 32:7 Genesis 32:7

Ndipo Yakobo akaogopa sana, na kufadhaika sana, akawagawanya watu waliopo pamoja naye, na kondoo, na ng'ombe, na ngamia, wawe matuo mawili.

Mwanzo 32:8 Genesis 32:8

Akasema, Akija Esau kwa kundi la kwanza, akalipiga, kundi litakalosalia litaokoka.

Mwanzo 32:9 Genesis 32:9

Yakobo akasema, Ee Mungu wa baba yangu Ibrahimu, na Mungu wa baba yangu Isaka, Bwana, uliyeniambia, Rudi uende mpaka nchi yako, na kwa jamaa zako, nami nitakutendea mema;

Mwanzo 32:10 Genesis 32:10

mimi sistahili hata kidogo hizo rehema zote na kweli yote uliyomfanyia mtumwa wako; maana nalivuka mto huo wa Yordani na fimbo yangu tu, na sasa nimekuwa matuo mawili.

Mwanzo 32:11 Genesis 32:11

Uniokoe sasa na mkono wa ndugu yangu, mkono wa Esau, maana mimi namwogopa, asije akanipiga, na mama pamoja na wana.

Mwanzo 32:12 Genesis 32:12

Nawe ulisema, Hakika nitakutendea mema, nami nitafanya uzao wako uwe kama mchanga wa bahari, usiohesabika kwa kuwa mwingi.

Mwanzo 32:13 Genesis 32:13

Akakaa huko usiku ule. Kisha akatwaa baadhi ya vitu alivyokuwa navyo, kuwa zawadi kwa Esau, nduguye;

Mwanzo 32:14 Genesis 32:14

mbuzi wake mia mbili, na mbuzi waume ishirini, kondoo wake mia mbili, na kondoo waume ishirini;

Mwanzo 32:15 Genesis 32:15

ngamia wanyonyeshao thelathini pamoja na wana wao, ng'ombe wake arobaini na mafahali kumi; punda wake ishirini na wana wao kumi.

Mwanzo 32:16 Genesis 32:16

Akawatia mkononi mwa watumwa wake, kila kundi peke yake. Naye akawaambia watumwa wake, Vukeni mbele yangu, mkaache nafasi kati ya kundi na kundi.

Mwanzo 32:17 Genesis 32:17

Akamwagiza yule wa kwanza akasema, Esau, ndugu yangu, akikukuta, na kukuuliza, akisema, Wewe u wa nani? Unakwenda wapi? Tena ni wa nani hawa walio mbele yako?

Mwanzo 32:18 Genesis 32:18

Basi, useme, Ni wa mtumwa wako, Yakobo, ni zawadi, aliyompelekea bwana wangu, Esau. Na tazama, yeye mwenyewe yuko nyuma yetu.

Mwanzo 32:19 Genesis 32:19

Akamwagiza tena wa pili, na wa tatu, wote waliofuata makundi, akisema, Hivi ndivyo mtakavyomwambia Esau, akiwakuta.

Mwanzo 32:20 Genesis 32:20

Tena semeni, Tazama, mtumwa wako, Yakobo, yuko nyuma yetu. Maana alisema, Nitamsuluhisha kwa zawadi inayonitangulia, baadaye nitamwona uso wake; huenda atanikubali uso wangu.

Mwanzo 32:21 Genesis 32:21

Basi ile zawadi ikavuka mbele yake, naye mwenyewe akakaa usiku ule kambini.

Mwanzo 32:22 Genesis 32:22

Akaondoka usiku ule akawatwaa wakeze wawili, na vijakazi wake wawili, na wanawe kumi na mmoja, akavuka kivuko cha Yaboki.

Mwanzo 32:23 Genesis 32:23

Akawatwaa, akawavusha mto, akavusha na vyote alivyokuwa navyo.

Mwanzo 32:24 Genesis 32:24

Yakobo akakaa peke yake; na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri.

Mwanzo 32:25 Genesis 32:25

Naye alipoona ya kuwa hamshindi, alimgusa panapo uvungu wa paja lake; ukateguka uvungu wa paja la Yakobo alipokuwa akishindana naye.

Mwanzo 32:26 Genesis 32:26

Akasema, Niache, niende, maana kunapambazuka. Akasema, Sikuachi, usiponibariki.

Mwanzo 32:27 Genesis 32:27

Akamwuliza, Jina lako n'nani? Akasema, Yakobo.

Mwanzo 32:28 Genesis 32:28

Akamwambia, Jina lako hutaitwa tena Yakobo, ila Israeli, maana umeshindana na Mungu, na watu, nawe umeshinda.

Mwanzo 32:29 Genesis 32:29

Yakobo akamwuliza, akasema, Niambie, tafadhali, jina lako? Akasema, Kwa nini waniuliza jina langu? Akambariki huko.

Mwanzo 32:30 Genesis 32:30

Yakobo akapaita mahali pale, Penueli, maana alisema, Nimeonana na Mungu uso kwa uso, na nafsi yangu imeokoka.

Mwanzo 32:31 Genesis 32:31

Jua likamzukia akivuka Penueli, akachechemea kwa sababu ya paja la mguu wake.

Mwanzo 32:32 Genesis 32:32

Kwa hiyo wana wa Israeli hawali ule mshipa ulio katika uvungu wa paja hata leo; maana alimgusa Yakobo panapo uvungu wa paja katika mshipa wa kiuno.