Mwanzo Mlango 21 Genesis

Mwanzo 21:1 Genesis 21:1

Bwana akamjia Sara kama alivyonena, na Bwana akamfanyia kama alivyosema.

Mwanzo 21:2 Genesis 21:2

Sara akapata mimba akamzalia Ibrahimu mwana wa kiume katika uzee wake, kwa muhula alioambiwa na Mungu.

Mwanzo 21:3 Genesis 21:3

Ibrahimu akamwita jina lake Isaka, yule mwana aliyezaliwa, ambaye Sara alimzalia.

Mwanzo 21:4 Genesis 21:4

Ibrahimu akamtahiri Isaka mwanawe, alipokuwa mwenye siku nane, kama Mungu alivyomwamuru.

Mwanzo 21:5 Genesis 21:5

Naye Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka.

Mwanzo 21:6 Genesis 21:6

Sara akasema, Mungu amenifanyia kicheko; kila asikiaye atacheka pamoja nami.

Mwanzo 21:7 Genesis 21:7

Akasema, N'nani angemwambia Ibrahimu, Sara atanyonyesha wana? Maana nimemzalia mwana katika uzee wake.

Mwanzo 21:8 Genesis 21:8

Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya; Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya.

Mwanzo 21:9 Genesis 21:9

Sara akamwona yule mwana wa Hajiri Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka.

Mwanzo 21:10 Genesis 21:10

Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka.

Mwanzo 21:11 Genesis 21:11

Na neno hilo lilikuwa baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe.

Mwanzo 21:12 Genesis 21:12

Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huyo mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa.

Mwanzo 21:13 Genesis 21:13

Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa, maana huyu naye ni uzao wako.

Mwanzo 21:14 Genesis 21:14

Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji, akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa la Beer-sheba.

Mwanzo 21:15 Genesis 21:15

Yale maji yakaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja.

Mwanzo 21:16 Genesis 21:16

Akaenda akakaa akimkabili, mbali naye kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye akakaa akimkabili, akapaza sauti yake, akalia.

Mwanzo 21:17 Genesis 21:17

Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti ya kijana huko aliko.

Mwanzo 21:18 Genesis 21:18

Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa taifa kubwa.

Mwanzo 21:19 Genesis 21:19

Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji, akamnywesha kijana.

Mwanzo 21:20 Genesis 21:20

Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa mpiga upinde.

Mwanzo 21:21 Genesis 21:21

Akakaa katika jangwa la Parani; mama yake akamtwalia mke katika nchi ya Misri.

Mwanzo 21:22 Genesis 21:22

Ikawa wakati ule Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakamwambia Ibrahimu, wakinena, Mungu yu pamoja nawe katika yote unayotenda.

Mwanzo 21:23 Genesis 21:23

Basi sasa uniapie kwa Mungu, ya kuwa hutanitenda hila, wala mwanangu, wala mjukuu wangu, lakini kwa kadiri ya fadhili niliyokutendea utanitendea mimi, na nchi hii ambayo umetembea ndani yake.

Mwanzo 21:24 Genesis 21:24

Ibrahimu akasema, Nitaapa.

Mwanzo 21:25 Genesis 21:25

Kisha Ibrahimu akamlaumu Abimeleki kwa sababu ya kisima cha maji ambacho watumwa wa Abimeleki wamekinyang'anya.

Mwanzo 21:26 Genesis 21:26

Abimeleki akasema, Mimi sijui ni nani aliyetenda neno hili, wala hukuniambia, wala sikusikia habari hii ila leo tu.

Mwanzo 21:27 Genesis 21:27

Ibrahimu akatwaa kondoo na ng'ombe akampa Abimeleki, na hao wawili wakafanya mapatano.

Mwanzo 21:28 Genesis 21:28

Ibrahimu akaweka wana kondoo wa kike saba peke yao.

Mwanzo 21:29 Genesis 21:29

Abimeleki akamwambia Ibrahimu, Hawa wana kondoo wa kike saba, uliowaweka peke yao, maana yake nini?

Mwanzo 21:30 Genesis 21:30

Akasema, Hawa wana kondoo wa kike saba utawapokea mkononi mwangu, wawe ushuhuda ya kuwa ni mimi niliyekichimba kisima hiki.

Mwanzo 21:31 Genesis 21:31

Kwa hiyo akapaita mahali pale Beer-sheba, kwa sababu waliapa huko wote wawili.

Mwanzo 21:32 Genesis 21:32

Basi wakafanya mapatano huko Beer-sheba. Abimeleki, na Fikoli mkuu wa jeshi lake, wakaondoka wakarudi hata nchi ya Wafilisti.

Mwanzo 21:33 Genesis 21:33

Ibrahimu akapanda mkwaju huko Beer-sheba, akaliitia huko jina la Bwana Mungu wa milele.

Mwanzo 21:34 Genesis 21:34

Ibrahimu akakaa hali ya ugeni katika nchi ya Wafilisti siku nyingi.