Mwanzo Mlango 28 Genesis

Mwanzo 28:1 Genesis 28:1

Basi Isaka akamwita Yakobo, akambariki, akamwagiza akamwambia, Usitwae mke wa binti za Kanaani.

Mwanzo 28:2 Genesis 28:2

Ondoka, uende Padan-aramu, mpaka nyumba ya Bethueli baba ya mama yako, ukajitwalie huko mke katika binti za Labani, ndugu wa mama yako.

Mwanzo 28:3 Genesis 28:3

Na Mungu Mwenyezi, akubariki, akuzidishe, na kukuongeza, ili uwe mkutano wa makabila.

Mwanzo 28:4 Genesis 28:4

Akupe mbaraka wa Ibrahimu, wewe na uzao wako pamoja nawe, upate kuirithi nchi ya kusafiri kwako, Mungu aliyompa Ibrahimu.

Mwanzo 28:5 Genesis 28:5

Basi Isaka akampeleka Yakobo, naye akaenda Padan-aramu, kwa Labani, mwana wa Bethueli, Mshami, ndugu wa Rebeka, mama yao Yakobo na Esau.

Mwanzo 28:6 Genesis 28:6

Esau akaona ya kwamba Isaka amembariki Yakobo na kumpeleka Padan-aramu, ili ajitwalie mke huko, na katika kumbariki akamwagiza, akasema, Usitwae mke wa binti za Kanaani,

Mwanzo 28:7 Genesis 28:7

na ya kuwa Yakobo amewatii babaye na mamaye, akaenda Padan-aramu.

Mwanzo 28:8 Genesis 28:8

Esau akaona ya kuwa binti za Kanaani hawakumpendeza Isaka, baba yake.

Mwanzo 28:9 Genesis 28:9

Basi Esau akaenda kwa Ishmaeli akamtwaa Mahalathi, binti Ishmaeli mwana wa Ibrahimu, ndugu wa Nebayothi, kuwa mkewe pamoja na wakeze aliokuwa nao.

Mwanzo 28:10 Genesis 28:10

Yakobo akatoka Beer-sheba, kwenda Harani.

Mwanzo 28:11 Genesis 28:11

Akafika mahali fulani akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale.

Mwanzo 28:12 Genesis 28:12

Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamishwa juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama, malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake.

Mwanzo 28:13 Genesis 28:13

Na tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako.

Mwanzo 28:14 Genesis 28:14

Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa.

Mwanzo 28:15 Genesis 28:15

Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia.

Mwanzo 28:16 Genesis 28:16

Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua.

Mwanzo 28:17 Genesis 28:17

Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni.

Mwanzo 28:18 Genesis 28:18

Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake.

Mwanzo 28:19 Genesis 28:19

Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu.

Mwanzo 28:20 Genesis 28:20

Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae;

Mwanzo 28:21 Genesis 28:21

nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu.

Mwanzo 28:22 Genesis 28:22

Na jiwe hili nililolisimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.