Mwanzo Mlango 22 Genesis

Mwanzo 22:1 Genesis 22:1

Ikawa baada ya mambo hayo Mungu alimjaribu Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.

Mwanzo 22:2 Genesis 22:2

Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.

Mwanzo 22:3 Genesis 22:3

Ibrahimu akaondoka alfajiri, akatandika punda wake, akachukua vijana wawili pamoja naye, na Isaka mwanawe, akachanja kuni kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka, akaenda mpaka mahali alipoambiwa na Mungu.

Mwanzo 22:4 Genesis 22:4

Siku ya tatu Ibrahimu akainua macho yake, akapaona mahali pakali mbali.

Mwanzo 22:5 Genesis 22:5

Ibrahimu akawaambia vijana wake, Kaeni ninyi hapa pamoja na punda, na mimi na kijana tutakwenda kule, tukaabudu, na kuwarudia tena.

Mwanzo 22:6 Genesis 22:6

Basi Ibrahimu akazitwaa kuni za hiyo sadaka, akamtwika Isaka mwanawe; akatwaa moto na kisu mkononi mwake, wakaenda wote wawili pamoja.

Mwanzo 22:7 Genesis 22:7

Isaka akasema na Ibrahimu baba yake, akinena, Babangu! Naye akasema, Mimi hapa, mwanangu. Akasema, Tazama! Moto upo, na kuni zipo, lakini yuko wapi mwana-kondoo kwa sadaka ya kuteketezwa?

Mwanzo 22:8 Genesis 22:8

Ibrahimu akasema, Mungu atajipatia mwana-kondoo kwa hiyo sadaka, mwanangu. Basi wakaendelea wote wawili pamoja.

Mwanzo 22:9 Genesis 22:9

Wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kisha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni.

Mwanzo 22:10 Genesis 22:10

Ibrahimu akanyosha mkono wake, akakitwaa kisu ili amchinje mwanawe.

Mwanzo 22:11 Genesis 22:11

Ndipo malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akasema, Ibrahimu! Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.

Mwanzo 22:12 Genesis 22:12

Akasema, Usimnyoshee kijana mkono wako, wala usimtendee neno; kwa maana sasa ninajua ya kuwa unamcha Mungu, iwapo hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee.

Mwanzo 22:13 Genesis 22:13

Ibrahimu akainua macho yake, akaangalia, na tazama, kondoo mume yuko nyuma yake, amenaswa pembe zake katika kichaka. Basi Ibrahimu akaenda akamtwaa huyo kondoo, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.

Mwanzo 22:14 Genesis 22:14

Ibrahimu akapaita mahali hapo Yehova-yire,kama watu wasemavyo hata leo,Katika mlima wa BWANA itapatikana.

Mwanzo 22:15 Genesis 22:15

Malaika wa Bwana akamwita Ibrahimu mara ya pili kutoka mbinguni

Mwanzo 22:16 Genesis 22:16

akasema, Nimeapa kwa nafsi yangu asema Bwana, kwa kuwa umetenda neno hili, wala hukunizuilia mwanao, mwanao wa pekee,

Mwanzo 22:17 Genesis 22:17

katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako kama nyota za mbinguni, na kama mchanga ulioko pwani; na uzao wako utamiliki mlango wa adui zao;

Mwanzo 22:18 Genesis 22:18

na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu umetii sauti yangu.

Mwanzo 22:19 Genesis 22:19

Basi Ibrahimu akawarudia vijana wake, wakaondoka, wakaenda zao pamoja mpaka Beer-sheba; Ibrahimu akakaa huko Beer-sheba.

Mwanzo 22:20 Genesis 22:20

Ikawa baada ya mambo hayo, Ibrahimu akaambiwa ya kwamba, Tazama, Milka naye amemzalia Nahori ndugu yako wana;

Mwanzo 22:21 Genesis 22:21

Usi, mzaliwa wa kwanza wake, na Buzi nduguye, na Kemueli, baba wa Aramu;

Mwanzo 22:22 Genesis 22:22

na Kesedi, na Hazo, na Pildashi, na Yidlafu, na Bethueli.

Mwanzo 22:23 Genesis 22:23

Bethueli akamzaa Rebeka; hao wanane Milka alimzalia Nahori ndugu wa Ibrahimu.

Mwanzo 22:24 Genesis 22:24

Na suria wake Reuma naye alizaa Teba na Gahamu na Tahashi na Maaka.