Mwanzo Mlango 47 Genesis

Mwanzo 47:1 Genesis 47:1

Ndipo Yusufu akaja akamwarifu Farao, akasema, Baba yangu, na ndugu zangu, na kondoo zao, na ng'ombe zao, na yote waliyo nayo, wamekuja kutoka nchi ya Kanaani, nao wako katika nchi ya Gosheni.

Mwanzo 47:2 Genesis 47:2

Akatwaa watu watano miongoni mwa nduguze, akawasimamisha mbele ya Farao.

Mwanzo 47:3 Genesis 47:3

Farao akawauliza hao nduguze, Kazi yenu ni nini? Wakamwambia Farao, Watumwa wako tu wachunga wanyama, sisi, na baba zetu.

Mwanzo 47:4 Genesis 47:4

Wakamwambia Farao, Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwa sababu wanyama wa watumwa wako hawana malisho, maana njaa ni nzito sana katika nchi ya Kanaani. Basi, twakusihi, uturuhusu sisi watumwa wako tukae katika nchi ya Gosheni.

Mwanzo 47:5 Genesis 47:5

Farao akamwambia Yusufu, akisema, Baba yako na ndugu zako wamekujia;

Mwanzo 47:6 Genesis 47:6

nchi ya Misri iko mbele yako, palipo pema pa nchi uwakalishe baba yako na ndugu zako; na wakae katika nchi ya Gosheni. Tena ukijua ya kuwa wako watu hodari miongoni mwao, uwaweke wawe wakuu wa wanyama wangu.

Mwanzo 47:7 Genesis 47:7

Yusufu akamleta Yakobo babaye ndani akamweka mbele ya Farao Yakobo akambariki Farao.

Mwanzo 47:8 Genesis 47:8

Farao akamwuliza Yakobo, Je! Siku za miaka ya maisha yako ni ngapi?

Mwanzo 47:9 Genesis 47:9

Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, tena za taabu, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao.

Mwanzo 47:10 Genesis 47:10

Yakobo akambariki Farao, akatoka mbele ya Farao.

Mwanzo 47:11 Genesis 47:11

Yusufu akawakalisha babaye na nduguze, na kuwapa milki katika nchi ya Misri, katika mahali pazuri pa nchi, katika nchi ya Ramesesi, kama Farao alivyoamuru.

Mwanzo 47:12 Genesis 47:12

Naye Yusufu akawalisha babaye na nduguze na nyumba yote ya babaye, kwa kadiri ya hesabu ya watoto wao.

Mwanzo 47:13 Genesis 47:13

Wala hapakuwa na chakula katika nchi yote, kwa kuwa njaa ilikuwa nzito sana, hata nchi ya Misri, na nchi ya Kanaani zikataabika, kwa sababu ya njaa.

Mwanzo 47:14 Genesis 47:14

Yusufu akakusanya fedha zote zilizoonekana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, kwa nafaka waliyoinunua. Yusufu akazileta zile fedha nyumbani mwa Farao.

Mwanzo 47:15 Genesis 47:15

Fedha zote zilipokwisha katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani, Wamisri wote walimjia Yusufu, wakisema, Tupe sisi chakula, kwa nini tufe mbele ya macho yako? Maana fedha zetu zimekwisha.

Mwanzo 47:16 Genesis 47:16

Yusufu akasema, Toeni wanyama wenu, nami nitawapa chakula badala ya wanyama wenu, kama fedha zenu zimekwisha.

Mwanzo 47:17 Genesis 47:17

Wakaleta wanyama wao kwa Yusufu; Yusufu akawapa chakula badala ya farasi, na badala ya kondoo, na badala ya ng'ombe, na badala ya punda, naye akawalisha chakula badala ya wanyama wao wote mwaka ule.

Mwanzo 47:18 Genesis 47:18

Na mwaka ule ulipokwisha wakamjia mwaka wa pili, wakamwambia, Hatumfichi bwana wetu ya kwamba fedha zetu zimekwisha, na makundi ya wanyama ni mali ya bwana wetu, hakikusalia kitu mbele ya bwana wetu, ila miili yetu na nchi zetu.

Mwanzo 47:19 Genesis 47:19

Kwa nini tufe mbele ya macho yako, sisi na nchi yetu? Utununue sisi na nchi yetu kwa chakula, na sisi na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao; kisha utupe mbegu, tuishi wala tusife, wala nchi yetu isipotee.

Mwanzo 47:20 Genesis 47:20

Basi Yusufu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri; maana Wamisri waliuza kila mtu shamba lake; kwa sababu njaa ilikuwa imewazidi sana, nchi ikawa mali yake Farao.

Mwanzo 47:21 Genesis 47:21

Akawahamisha hao watu, akawaweka katika miji, tangu upande huu wa Misri hata upande huu.

Mwanzo 47:22 Genesis 47:22

Ila nchi ya makuhani hakuinunua; maana makuhani walikuwa na posho yao kutoka kwa Farao, wakala posho yao waliyopewa na Farao. Kwa hiyo hawakuuza nchi yao.

Mwanzo 47:23 Genesis 47:23

Yusufu akawaambia watu, Angalieni, nimewanunua leo, ninyi, na nchi yenu, kuwa mali ya Farao; basi mbegu zenu ni hizi, zipandeni katika nchi.

Mwanzo 47:24 Genesis 47:24

Itakuwa wakati wa mavuno mtampa Farao sehemu ya tano, na sehemu nne zitakuwa zenu wenyewe, kuwa mbegu za nchi, na chakula chenu, na chakula chao waliomo nyumbani mwenu, na chakula cha watoto wenu.

Mwanzo 47:25 Genesis 47:25

Wakasema, Umetulinda hai, na tuone kibali machoni pa bwana wetu, nasi tutakuwa watumwa wa Farao.

Mwanzo 47:26 Genesis 47:26

Yusufu akaifanya sheria kwa habari ya nchi ya Misri hata leo, ya kwamba sehemu ya tano iwe mali ya Farao. Ila nchi ya makuhani tu haikuwa mali ya Farao.

Mwanzo 47:27 Genesis 47:27

Israeli akakaa katika nchi ya Misri, katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali humo, wakaongezeka na kuzidi sana.

Mwanzo 47:28 Genesis 47:28

Yakobo akaishi katika nchi ya Misri miaka kumi na saba, basi siku za miaka ya maisha yake Yakobo ilikuwa miaka mia moja na arobaini na saba.

Mwanzo 47:29 Genesis 47:29

Siku za kufa kwake Israeli zikakaribia; akamwita mwanawe Yusufu, akamwambia, Kama nimeona kibali machoni pako, weka mkono wako chini ya paja langu, ukanifanyie rehema na kweli; nakusihi usinizike katika Misri.

Mwanzo 47:30 Genesis 47:30

Lakini nitakapolala pamoja na baba zangu, unichukue toka Misri, unizike katika kaburi lao. Akasema, Nitafanya kama ulivyosema.

Mwanzo 47:31 Genesis 47:31

Akanena, Niapie. Naye akamwapia. Israeli akajiinamisha kwenye mchago wa kitanda.