Mwanzo Mlango 24 Genesis

Mwanzo 24:1 Genesis 24:1

Basi Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi, na Bwana alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote.

Mwanzo 24:2 Genesis 24:2

Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu,

Mwanzo 24:3 Genesis 24:3

nami nitakuapisha kwa Bwana, Mungu wa mbingu, na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za Wakanaani ambao nakaa kati yao;

Mwanzo 24:4 Genesis 24:4

bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke.

Mwanzo 24:5 Genesis 24:5

Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, je! Nimrudishe mwanao mpaka nchi ulikotoka?

Mwanzo 24:6 Genesis 24:6

Ibrahimu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko.

Mwanzo 24:7 Genesis 24:7

Bwana, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko;

Mwanzo 24:8 Genesis 24:8

na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko.

Mwanzo 24:9 Genesis 24:9

Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Ibrahimu bwana wake, akamwapia katika neno hilo.

Mwanzo 24:10 Genesis 24:10

Kisha huyo mtumishi akatwaa ngamia kumi katika ngamia za bwana wake akaenda zake, maana mali zote za bwana wake zilikuwa mkononi mwake, akaondoka, akaja mpaka Mesopotamia, mpaka mji wa Nahori.

Mwanzo 24:11 Genesis 24:11

Akawapigisha magoti ngamia nje ya mji karibu na kisima cha maji wakati wa jioni, wakati ambapo wanawake wanakwenda kuteka maji.

Mwanzo 24:12 Genesis 24:12

Naye akasema, Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu.

Mwanzo 24:13 Genesis 24:13

Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji,

Mwanzo 24:14 Genesis 24:14

basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu.

Mwanzo 24:15 Genesis 24:15

Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake.

Mwanzo 24:16 Genesis 24:16

Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda.

Mwanzo 24:17 Genesis 24:17

Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe.

Mwanzo 24:18 Genesis 24:18

Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha.

Mwanzo 24:19 Genesis 24:19

Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa.

Mwanzo 24:20 Genesis 24:20

Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote.

Mwanzo 24:21 Genesis 24:21

Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kwamba Bwana ameifanikisha safari yake ama sivyo.

Mwanzo 24:22 Genesis 24:22

Ikawa, ngamia walipokwisha kunywa, yule mtu akatwaa pete ya dhahabu, uzani wake ulikuwa nusu shekeli, na vikuku viwili kwa mikono yake, uzani wake ulikuwa shekeli kumi za dhahabu,

Mwanzo 24:23 Genesis 24:23

akasema, U binti wa nani wewe? Tafadhali uniambie. Je! Iko nafasi katika nyumba ya baba yako tupate mahali pa kukaa kwa muda?

Mwanzo 24:24 Genesis 24:24

Akasema, Mimi ni binti wa Bethueli mwana wa Milka, aliyemzalia Nahori.

Mwanzo 24:25 Genesis 24:25

Tena akamwambia, Kwetu kuna majani na malisho ya kutosha, na mahali pa kukaa wageni.

Mwanzo 24:26 Genesis 24:26

Yule mtu akainama akamsujudu Bwana.

Mwanzo 24:27 Genesis 24:27

Akasema, Na atukuzwe Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ambaye hakuacha rehema zake na kweli yake kwa bwana wangu. Bwana akaniongoza mimi nami njiani hata nyumba ya nduguze bwana wangu.

Mwanzo 24:28 Genesis 24:28

Basi yule msichana akapiga mbio, akawaambia watu wa nyumba ya mama yake mambo hayo.

Mwanzo 24:29 Genesis 24:29

Na Rebeka alikuwa na kaka, jina lake Labani. Labani akatoka mbio kumwendea yule mtu kisimani.

Mwanzo 24:30 Genesis 24:30

Ikawa, alipoiona ile pete, na vikuku mikononi mwa nduguye, akasikia maneno ya Rebeka nduguye, akisema, Hivyo ndivyo alivyoniambia mtu huyo, basi akamjia mtu yule, na tazama, amesimama karibu na ngamia kisimani.

Mwanzo 24:31 Genesis 24:31

Akasema, Karibu, wewe uliyebarikiwa na Bwana, mbona unasimama nje? Kwa maana nimeiweka nyumba tayari, na nafasi kwa ngamia.

Mwanzo 24:32 Genesis 24:32

Na mtu yule akaingia katika nyumba, akawafungua ngamia; naye akatoa majani na malisho kwa ngamia, na maji ya kuoshea miguu yake, na miguu ya watu waliokuwa pamoja naye.

Mwanzo 24:33 Genesis 24:33

Akaandaliwa chakula, lakini akasema, Sili mpaka niseme kwanza maneno yangu. Akamwambia, Haya, sema.

Mwanzo 24:34 Genesis 24:34

Akasema, Mimi ni mtumwa wa Ibrahimu,

Mwanzo 24:35 Genesis 24:35

na Bwana amembarikia sana bwana wangu, amekuwa mtu mkuu; amempa kondoo, na ng'ombe, na fedha, na dhahabu, na watumwa, na wajakazi, na ngamia, na punda.

Mwanzo 24:36 Genesis 24:36

Naye Sara, mkewe bwana wangu, akamzalia bwana wangu mwana wa kiume, katika uzee wake; naye amempa yote aliyo nayo.

Mwanzo 24:37 Genesis 24:37

Kisha bwana wangu akaniapisha akisema, Usimtwalie mwanangu mke wa binti za Wakanaani, ambao nakaa katika nchi yao.

Mwanzo 24:38 Genesis 24:38

Ila uende mpaka nyumbani kwa babangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu mke.

Mwanzo 24:39 Genesis 24:39

Nikamwambia bwana wangu, Labda huyo mwanamke hatafuatana nami.

Mwanzo 24:40 Genesis 24:40

Akaniambia, Bwana, ambaye naenenda machoni pake, atapeleka malaika wake pamoja nawe, atafanikisha njia yako; nawe umtwalie mwanangu mke katika jamaa zangu, na wa nyumba ya babangu.

Mwanzo 24:41 Genesis 24:41

Ndipo utafunguliwa kiapo changu hapo utakapowafikilia jamaa zangu; nao wasipokupa msichana huyo, utafunguliwa kiapo changu.

Mwanzo 24:42 Genesis 24:42

Nami nikaja leo kisimani, nikasema, Ee Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, ukinifanikishia sasa njia yangu niendayo mimi,

Mwanzo 24:43 Genesis 24:43

tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji; basi na iwe hivi, msichana ajaye kuteka maji, nikamwambia, Nipe, nakuomba, maji kidogo katika mtungi wako ninywe,

Mwanzo 24:44 Genesis 24:44

naye akaniambia, Unywe wewe, na ngamia zako pia nitawatekea, huyo na awe ndiye mke Bwana aliyemwekea mwana wa bwana wangu.

Mwanzo 24:45 Genesis 24:45

Hata kabla sijaisha kusema moyoni mwangu, tazama! Rebeka akatokea, na mtungi begani mwake. Akashuka kisimani akateka. Nami nikamwambia, Tafadhali nipe maji ninywe.

Mwanzo 24:46 Genesis 24:46

Akafanya haraka akatua mtungi wake chini, akanena, Unywe, na ngamia zako nitawanywesha pia; basi nikanywa, akawanywesha na ngamia nao.

Mwanzo 24:47 Genesis 24:47

Kisha nikamwuliza nikasema, U binti wa nani wewe? Naye akasema, Mimi ni binti Bethueli, mwana wa Nahori, Milka aliyemzalia. Nami nikamtia hazama puani mwake na vikuku mikononi mwake.

Mwanzo 24:48 Genesis 24:48

Nikainama, nikamsujudia Bwana, nikamtukuza Bwana, Mungu wa bwana wangu Ibrahimu, aliyeniongoza njiani, nimtwalie mwana wa bwana wangu binti wa ndugu yake.

Mwanzo 24:49 Genesis 24:49

Basi, kama mnataka kumfanyia rehema na kweli bwana wangu, niambieni kama sivyo, niambieni; ili nigeuke upande wa kuume au wa kushoto.

Mwanzo 24:50 Genesis 24:50

Ndipo Labani na Bethueli wakajibu wakasema, Neno hili limetoka kwa Bwana, wala sisi hatuwezi kukuambia neno jema wala baya.

Mwanzo 24:51 Genesis 24:51

Tazama, huyo Rebeka yuko mbele yako, umchukue, ukaende zako awe mke wa mwana wa bwana wako, kama alivyosema Bwana.

Mwanzo 24:52 Genesis 24:52

Ikawa mtumishi wa Ibrahimu aliposikia maneno yao, akainama hata nchi mbele za Bwana.

Mwanzo 24:53 Genesis 24:53

Kisha huyo mtumishi akatoa vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, akampa Rebeka; na vitu vya thamani akampa nduguye na mamaye pia.

Mwanzo 24:54 Genesis 24:54

Wakala wakanywa, yeye na watu waliokuwa pamoja naye, nao wakakaa usiku. Wakaondoka asubuhi, naye akasema, Nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu.

Mwanzo 24:55 Genesis 24:55

Ndugu yake na mama yake wakasema, Msichana na akae kwetu kama siku kumi, zisipungue, baadaye aende.

Mwanzo 24:56 Genesis 24:56

Naye akawaambia, Msinikawilishe, mradi Bwana amefanikisha njia yangu; nipeni ruhusa niende kwa bwana wangu.

Mwanzo 24:57 Genesis 24:57

Wakasema, Na tumwite huyo msichana, tumwulize mwenyewe.

Mwanzo 24:58 Genesis 24:58

Wakamwita Rebeka wakamwuliza, Je! Utakwenda na mtu huyu? Akasema, Nitakwenda.

Mwanzo 24:59 Genesis 24:59

Ndipo wakampeleka Rebeka ndugu yao, na yaya wake, na mtumishi wa Ibrahimu, na watu wake.

Mwanzo 24:60 Genesis 24:60

Wakambarikia Rebeka, wakamwambia, Ndugu yetu, uwe wewe mama wa kumi elfu, mara elfu nyingi, na wazao wako waurithi mlango wa hao wawachukiao.

Mwanzo 24:61 Genesis 24:61

Rebeka akaondoka na vijakazi wake, nao wakapanda juu ya ngamia, wakamfuata yule mtu. Naye huyo mtumishi akamchukua Rebeka akaenda zake.

Mwanzo 24:62 Genesis 24:62

Basi Isaka alikuwa amekuja kwa njia ya Beer-lahai-roi, maana alikaa katika nchi ya kusini.

Mwanzo 24:63 Genesis 24:63

Isaka akatoka ili kutafakari kondeni wakati wa jioni; akainua macho yake, akaona, kuna ngamia wanakuja.

Mwanzo 24:64 Genesis 24:64

Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia.

Mwanzo 24:65 Genesis 24:65

Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika.

Mwanzo 24:66 Genesis 24:66

Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda.

Mwanzo 24:67 Genesis 24:67

Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.