Mwanzo Mlango 3 Genesis

Mwanzo 3:1 Genesis 3:1

Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani?

Mwanzo 3:2 Genesis 3:2

Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula;

Mwanzo 3:3 Genesis 3:3

lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa.

Mwanzo 3:4 Genesis 3:4

Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa,

Mwanzo 3:5 Genesis 3:5

kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.

Mwanzo 3:6 Genesis 3:6

Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala.

Mwanzo 3:7 Genesis 3:7

Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo.

Mwanzo 3:8 Genesis 3:8

Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone.

Mwanzo 3:9 Genesis 3:9

Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi?

Mwanzo 3:10 Genesis 3:10

Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.

Mwanzo 3:11 Genesis 3:11

Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale?

Mwanzo 3:12 Genesis 3:12

Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala.

Mwanzo 3:13 Genesis 3:13

Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala.

Mwanzo 3:14 Genesis 3:14

Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako;

Mwanzo 3:15 Genesis 3:15

nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino.

Mwanzo 3:16 Genesis 3:16

Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala.

Mwanzo 3:17 Genesis 3:17

Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako;

Mwanzo 3:18 Genesis 3:18

michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni;

Mwanzo 3:19 Genesis 3:19

kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi.

Mwanzo 3:20 Genesis 3:20

Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai.

Mwanzo 3:21 Genesis 3:21

Bwana Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika.

Mwanzo 3:22 Genesis 3:22

Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele;

Mwanzo 3:23 Genesis 3:23

kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa.

Mwanzo 3:24 Genesis 3:24

Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima.