Mwanzo Mlango 42 Genesis

Mwanzo 42:1 Genesis 42:1

Basi Yakobo akaona ya kuwa kuna nafaka katika Misri, Yakobo akawaambia wanawe, Kwa nini mnatazamana?

Mwanzo 42:2 Genesis 42:2

Akasema, Angalia, nimesikia ya kuwa kuna nafaka Misri; shukeni huko mkatununulie chakula, tupate kuishi wala tusife.

Mwanzo 42:3 Genesis 42:3

Basi ndugu kumi wa Yusufu wakashuka Misri ili wanunue nafaka.

Mwanzo 42:4 Genesis 42:4

Walakini Benyamini, ndugu wa Yusufu, Yakobo hakumpeleka pamoja na ndugu zake, maana alisema, Mabaya yasimpate.

Mwanzo 42:5 Genesis 42:5

Wana wa Israeli wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani.

Mwanzo 42:6 Genesis 42:6

Naye Yusufu alikuwa ni liwali juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake.

Mwanzo 42:7 Genesis 42:7

Yusufu akawaona nduguze, akawatambua, lakini alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema. Tumetoka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula.

Mwanzo 42:8 Genesis 42:8

Yusufu akawatambua nduguze, bali wao hawakumtambua yeye.

Mwanzo 42:9 Genesis 42:9

Yusufu akazikumbuka zile ndoto alizowaotea. Akawaambia, Wapelelezi ninyi, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi.

Mwanzo 42:10 Genesis 42:10

Wakamwambia, Hasha, bwana, watumwa wako tumekuja ili tununue chakula.

Mwanzo 42:11 Genesis 42:11

Sisi sote ni wana wa mtu mmoja tu watu wa kweli sisi; watumwa wako si wapelelezi.

Mwanzo 42:12 Genesis 42:12

Akawaambia, Sivyo, mmekuja ili mwuone utupu wa nchi.

Mwanzo 42:13 Genesis 42:13

Wakamwambia, Sisi watumwa wako tu ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja katika nchi ya Kanaani; na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo, na mmoja hayuko.

Mwanzo 42:14 Genesis 42:14

Yusufu akawaambia, Ndivyo nilivyowaambia, nikisema, Wapelelezi ninyi.

Mwanzo 42:15 Genesis 42:15

Mtabainika kwa njia hii; aishivyo Farao, hamtoki hapa, asipokuja huku huyo ndugu yenu mdogo.

Mwanzo 42:16 Genesis 42:16

Mpelekeni mmoja wenu, aende akamlete ndugu yenu, na ninyi mtafungwa, hata maneno yenu yahakikishwe, kama mna kweli ninyi; ikiwa sivyo, aishivyo Farao, ninyi ni wapelelezi.

Mwanzo 42:17 Genesis 42:17

Akawatia wote gerezani siku tatu.

Mwanzo 42:18 Genesis 42:18

Yusufu akawaambia siku ya tatu, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu.

Mwanzo 42:19 Genesis 42:19

Kama ni wa kweli ninyi ndugu yenu mmoja na afungwe gerezani, nanyi nendeni mkachukue nafaka kwa njaa ya nyumba zenu,

Mwanzo 42:20 Genesis 42:20

mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya.

Mwanzo 42:21 Genesis 42:21

Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia kwa hiyo shida hii imetupata.

Mwanzo 42:22 Genesis 42:22

Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena.

Mwanzo 42:23 Genesis 42:23

Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alikuwapo mkalimani kati yao.

Mwanzo 42:24 Genesis 42:24

Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao.

Mwanzo 42:25 Genesis 42:25

Yusufu akaamuru kuvijaza vyombo vyao nafaka, na kumrudishia kila mtu fedha yake katika gunia lake, na kuwapa chakula cha njiani.

Mwanzo 42:26 Genesis 42:26

Navyo ndivyo walivyofanyiwa. Wakaweka nafaka yao juu ya punda zao, wakatoka huko.

Mwanzo 42:27 Genesis 42:27

Mmoja wao alipofungua gunia lake ili ampe punda wake chakula katika nyumba ya wageni, aliiona fedha yake; kumbe! Iko kinywani mwa gunia lake.

Mwanzo 42:28 Genesis 42:28

Akawaambia nduguze, Fedha yangu imerudishwa, angalia, imo humo guniani mwangu. Mioyo yao ikazimia, wakageukiana wakitetemeka, wakasema, N'nini hii Mungu aliyotutendea?

Mwanzo 42:29 Genesis 42:29

Wakaja kwa Yakobo, baba yao, katika nchi ya Kanaani, wakampasha habari za yote yaliyowapata, wakisema,

Mwanzo 42:30 Genesis 42:30

Mtu yule aliye bwana wa nchi alisema nasi kwa maneno makali, akatufanya tu wapelelezi wa nchi.

Mwanzo 42:31 Genesis 42:31

Tukamwambia, Tu watu wa kweli sisi, wala si wapelelezi.

Mwanzo 42:32 Genesis 42:32

Sisi tu ndugu kumi na wawili, wana wa baba yetu. Mmoja hayuko, na mdogo wetu yuko pamoja na baba yetu leo katika nchi ya Kanaani.

Mwanzo 42:33 Genesis 42:33

Yule mtu, bwana wa nchi, akatuambia, Kwa njia hii nitawajua kama ninyi ni watu wa kweli; ndugu yenu mmoja mwacheni huku kwangu, kachukueni nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mwende zenu.

Mwanzo 42:34 Genesis 42:34

Mkaniletee ndugu yenu mdogo; ndipo nitakapojua kama ninyi si wapelelezi, bali ni watu wa kweli; basi nitawarudishia ndugu yenu, nanyi mtafanya biashara katika nchi hii.

Mwanzo 42:35 Genesis 42:35

Ikawa walipomimina magunia yao, kumbe! Bahasha ya fedha ya kila mtu imo katika gunia lake. Nao walipoziona bahasha za fedha zao, wao na baba yao waliogopa.

Mwanzo 42:36 Genesis 42:36

Yakobo baba yao akawaambia, Mmeniondolea watoto wangu; Yusufu hayuko, wala Simeoni hayuko, na Benyamini mnataka kumchukua naye; mambo hayo yote yamenipata mimi.

Mwanzo 42:37 Genesis 42:37

Reubeni akamwambia babaye, akasema, Uwaue wanangu wawili nisipomrudisha kwako; mtie katika mikono yangu, nami nitamrudisha kwako.

Mwanzo 42:38 Genesis 42:38

Akasema, Mwanangu hatashuka pamoja nanyi, maana nduguye amekufa, naye amesalia peke yake; mabaya yakimpata katika njia mtakayoiendea ndipo mtakaposhusha mvi zangu kwa sikitiko mpaka kaburini.