Mwanzo Mlango 48 Genesis

Mwanzo 48:1 Genesis 48:1

Ikawa, baada ya mambo hayo, Yusufu akaambiwa, Tazama, baba yako hawezi; akawatwaa wanawe wawili, Manase na Efraimu, pamoja naye.

Mwanzo 48:2 Genesis 48:2

Naye akaarifiwa Yakobo ya kwamba, Angalia, mwanao Yusufu anakuja kwako. Israeli akajitia nguvu, akaketi juu ya kitanda.

Mwanzo 48:3 Genesis 48:3

Yakobo akamwambia Yusufu, Mungu Mwenyezi alinitokea huko Luzu, katika nchi ya Kanaani, akanibariki,

Mwanzo 48:4 Genesis 48:4

akaniambia, Mimi hapa, nitakuongezea uzao wako, na kukuzidisha, nami nitakufanya uwe kundi la mataifa; kisha nitawapa wazao wako nchi hii baada yako, iwe milki ya milele.

Mwanzo 48:5 Genesis 48:5

Basi sasa wanao wawili uliozaliwa katika nchi ya Misri kabla sijaja kwako Misri ni watoto wangu, yaani, Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama Reubeni na Simeoni.

Mwanzo 48:6 Genesis 48:6

Na wazao wako utakaozaa baada ya hawa watakuwa wako; kwa jina la ndugu zao wataitwa katika urithi wao.

Mwanzo 48:7 Genesis 48:7

Na mimi nilipokuja kutoka Padan, Raheli akanifia katika nchi ya Kanaani, njiani, si mwendo mkubwa kabla ya kufika Efrathi. Nikamzika katika njia ya Efrathi, ndio Bethlehemu.

Mwanzo 48:8 Genesis 48:8

Israeli akawaona wana wa Yusufu, akasema, Ni nani hawa?

Mwanzo 48:9 Genesis 48:9

Yusufu akamwambia babaye, Hawa ni wanangu, Mungu alionipa hapa. Akasema, Tafadhali uwalete kwangu nami nitawabariki.

Mwanzo 48:10 Genesis 48:10

Na macho ya Israeli yalikuwa mazito kwa uzee, wala hakuweza kuona. Akawaleta kwake, naye akawabusu, na kuwakumbatia.

Mwanzo 48:11 Genesis 48:11

Israeli akamwambia Yusufu, Sikudhani ya kwamba nitakuona uso wako, na Mungu amenionyesha na uzao wako pia.

Mwanzo 48:12 Genesis 48:12

Yusufu akawatoa katika magoti yake, naye akainama kifudifudi

Mwanzo 48:13 Genesis 48:13

Yusufu akawaweka wote wawili, Efraimu katika mkono wake wa kuume, kuelekea mkono wa kushoto wa Israeli; na Manase katika mkono wake wa kushoto, kuelekea mkono wa kuume wa Israeli, akawasogeza karibu naye.

Mwanzo 48:14 Genesis 48:14

Israeli akanyosha mkono wake wa kuume akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, aliyekuwa mdogo, na mkono wake wa kushoto akauweka juu ya kichwa cha Manase, huku akijua atiavyo mikono; maana Manase ndiye aliyezaliwa kwanza.

Mwanzo 48:15 Genesis 48:15

Akambariki Yusufu, akasema, Mungu ambaye baba zangu, Ibrahimu na Isaka, walienenda mbele zake, yeye Mungu aliyenilisha, maisha yangu yote, hata siku hii ya leo,

Mwanzo 48:16 Genesis 48:16

naye Malaika aliyeniokoa na maovu yote, na awabariki vijana hawa; jina langu na litajwe juu yao, na jina la baba zangu, Ibrahimu na Isaka; na wawe wingi wa watu kati ya nchi.

Mwanzo 48:17 Genesis 48:17

Yusufu alipoona kwamba babaye anaweka mkono wake wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, ikawa vibaya machoni pake. Akauinua mkono wa babaye auondoe katika kichwa cha Efraimu, ili auweke juu ya kichwa cha Manase.

Mwanzo 48:18 Genesis 48:18

Yusufu akamwambia babaye, Sivyo, babangu, maana huyu ni mzaliwa wa kwanza; weka mkono wako wa kuume kichwani pake.

Mwanzo 48:19 Genesis 48:19

Babaye akakataa, akasema, Najua, mwanangu najua, yeye naye atakuwa taifa, yeye naye atakuwa mkuu; lakini ndugu yake mdogo atakuwa mkubwa kuliko yeye, na uzao wake watakuwa wingi wa mataifa.

Mwanzo 48:20 Genesis 48:20

Akawabariki siku ile akasema, Katika ninyi Waisraeli watabariki, wakisema, Mungu na akufanye kama Efraimu na Manase. Akamweka Efraimu mbele ya Manase.

Mwanzo 48:21 Genesis 48:21

Israeli akamwambia Yusufu, Angalia, mimi ninakufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, naye atawarudisha mpaka nchi ya baba zenu.

Mwanzo 48:22 Genesis 48:22

Nami nimekupa wewe sehemu moja zaidi kuliko ndugu zako, niliyoitwaa katika mikono ya Waamori, kwa upanga wangu na upinde wangu.