Mwanzo Mlango 37 Genesis

Mwanzo 37:1 Genesis 37:1

Yakobo akakaa katika nchi aliyosafiri baba yake, katika nchi ya Kanaani.

Mwanzo 37:2 Genesis 37:2

Hivi ndivyo vizazi vya Yakobo. Yusufu, aliyekuwa mwenye miaka kumi na saba, alikuwa akichunga kondoo pamoja na ndugu zake; naye alikuwa kijana pamoja na wana wa Bilha, na wana wa Zilpa, wake wa baba yake. Yusufu akamletea baba yao habari zao mbaya.

Mwanzo 37:3 Genesis 37:3

Basi Israeli akampenda Yusufu kuliko wanawe wote, maana ni mwana wa uzee wake, akamfanyia kanzu ndefu.

Mwanzo 37:4 Genesis 37:4

Ndugu zake wakaona ya kuwa baba yao anampenda kuliko ndugu zake wote, wakamchukia, wala hawakuweza kusema naye kwa amani.

Mwanzo 37:5 Genesis 37:5

Yusufu akaota ndoto, akawapa ndugu zake habari, nao wakazidi kumchukia;

Mwanzo 37:6 Genesis 37:6

akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota.

Mwanzo 37:7 Genesis 37:7

Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.

Mwanzo 37:8 Genesis 37:8

Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake.

Mwanzo 37:9 Genesis 37:9

Akaota tena ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake, akasema, Angalieni, nimeota ndoto nyingine; na tazama, jua na mwezi na nyota kumi na moja zikaniinamia.

Mwanzo 37:10 Genesis 37:10

Akawaambia baba yake na ndugu zake; baba yake akamkemea akamwambia, Ni ndoto gani hii uliyoiota? Je! Mimi na mama yako na ndugu zako tutakuja tukusujudie hata nchi?

Mwanzo 37:11 Genesis 37:11

Ndugu zake wakamhusudu; bali baba yake akalihifadhi neno hili.

Mwanzo 37:12 Genesis 37:12

Ndugu zake wakaenda kuchunga kondoo za baba yao huko Shekemu.

Mwanzo 37:13 Genesis 37:13

Israeli akamwambia Yusufu, Je! Ndugu zako hawachungi kondoo katika Shekemu? Njoo, nikutume kwao. Akamwambia, Mimi hapa.

Mwanzo 37:14 Genesis 37:14

Akamwambia, Enenda, basi, ukaone kama ndugu zako hawajambo, na kundi nalo li salama, ukaniletee habari. Basi akampeleka kutoka bonde la Hebroni, akafika Shekemu.

Mwanzo 37:15 Genesis 37:15

Mtu mmoja akamkuta, naye alikuwa anazunguka-zunguka katika nyika; yule mtu akamwuliza, akisema, Unatafuta nini?

Mwanzo 37:16 Genesis 37:16

Akasema, Nawatafuta ndugu zangu; tafadhali uniambie mahali wanakochunga.

Mwanzo 37:17 Genesis 37:17

Yule mtu akasema, Wametoka hapa, maana niliwasikia wakisema, Twendeni Dothani. Basi Yusufu akawafuata ndugu zake akawakuta huko Dothani.

Mwanzo 37:18 Genesis 37:18

Wakamwona toka mbali, na kabla hajawakaribia, wakafanya shauri juu yake ili wamwue.

Mwanzo 37:19 Genesis 37:19

Wakasemezana wao kwa wao, Tazama, yule bwana wa ndoto anakuja.

Mwanzo 37:20 Genesis 37:20

Haya, twende, tukamwue na kumtupa katika birika mojawapo, nasi tutasema, Mnyama mkali amemla; kisha tutaona zitakuwaje ndoto zake.

Mwanzo 37:21 Genesis 37:21

Reubeni akasikia akamwokoa katika mikono yao, akasema, Tusimwue.

Mwanzo 37:22 Genesis 37:22

Reubeni akawaambia, Msimwage damu; mtupeni katika birika hii iliyopo nyikani, wala msimguse; ili apate kumwokoa katika mikono yao, akamrudishe kwa baba yake.

Mwanzo 37:23 Genesis 37:23

Ikawa Yusufu alipofika kwa ndugu zake, wakamvua Yusufu kanzu yake, kanzu ile ndefu aliyoivaa,

Mwanzo 37:24 Genesis 37:24

wakamtwaa wakamtupa katika birika; na hiyo birika ilikuwa tupu, hamna maji.

Mwanzo 37:25 Genesis 37:25

Nao wakakaa kitako kula chakula; wakainua macho yao, wakaona, msafara wa Waishmaeli wanakuja wakitoka Gileadi na ngamia zao, wakichukua ubani na zeri na manemane, wakisafiri kuvichukua mpaka Misri.

Mwanzo 37:26 Genesis 37:26

Yuda akawaambia ndugu zake, Kwafaa nini kumwua ndugu yetu, na kuificha damu yake?

Mwanzo 37:27 Genesis 37:27

Haya, na tumwuze kwa hawa Waishmaeli, wala mikono yetu isimdhuru, maana yeye ni ndugu yetu, na damu yetu. Ndugu zake wakakubali.

Mwanzo 37:28 Genesis 37:28

Wakapita wafanya biashara Wamidiani; basi wakamtoa Yusufu, wakampandisha kumtoa katika birika, wakamwuza Yusufu kwa Waishmaeli kwa vipande vya fedha ishirini; nao wakamchukua Yusufu mpaka Misri.

Mwanzo 37:29 Genesis 37:29

Akarudi Reubeni birikani, kumbe! Yusufu hayumo katika birika, akararua nguo zake.

Mwanzo 37:30 Genesis 37:30

Akarudi kwa ndugu zake, akasema, Mtoto hayuko, nami niende wapi?

Mwanzo 37:31 Genesis 37:31

Wakaitwaa kanzu ya Yusufu, wakachinja mwana-mbuzi, na kuichovya kanzu katika damu.

Mwanzo 37:32 Genesis 37:32

Wakaenda nayo ile kanzu ndefu, wakamletea baba yao, wakasema, Tumeona hii; basi, utambue kama kanzu hii ni ya mwanao, ama siyo.

Mwanzo 37:33 Genesis 37:33

Akaitambua, akasema, Ndiyo kanzu ya mwanangu, mnyama mkali amemla; bila shaka Yusufu ameraruliwa.

Mwanzo 37:34 Genesis 37:34

Yakobo akararua mavazi yake, akajivika gunia viunoni, na kumlilia mwanawe siku nyingi.

Mwanzo 37:35 Genesis 37:35

Wanawe wote, na binti zake wote, wakaondoka wamtulize, lakini akakataa kutulizwa, akasema, La! Nitamshukia mwanangu, nikisikitika, hata kuzimu. Baba yake akamlilia.

Mwanzo 37:36 Genesis 37:36

Nao Wamidiani wakamwuza huko Misri, kwa Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari.