Isaya Mlango 42 Isaiah

Isaya 42:1 Isaiah 42:1

Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu.

Isaya 42:2 Isaiah 42:2

Hatalia, wala hatapaza sauti yake, wala kuifanya isikiwe katika njia kuu.

Isaya 42:3 Isaiah 42:3

Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli.

Isaya 42:4 Isaiah 42:4

Hatazimia, wala hatakata tamaa, hata atakapoweka hukumu duniani; na visiwa vitaingojea sheria yake.

Isaya 42:5 Isaiah 42:5

Mungu Bwana anena, yeye aliyeziumba mbingu, na kuzitanda; yeye aliyeitandaza nchi na mazao yake; yeye awapaye pumzi watu walio juu yake; yeye awapaye roho wao waendao ndani yake.

Isaya 42:6 Isaiah 42:6

Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa;

Isaya 42:7 Isaiah 42:7

kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa.

Isaya 42:8 Isaiah 42:8

Mimi ni Bwana; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu.

Isaya 42:9 Isaiah 42:9

Tazama, mambo ya kwanza yamekuwa, nami nayahubiri mambo mapya; kabla hayajatokea nawapasheni habari zake.

Isaya 42:10 Isaiah 42:10

Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Na sifa zake tokea mwisho wa dunia; Ninyi mshukao baharini, na vyote vilivyomo, Na visiwa, nao wakaao humo.

Isaya 42:11 Isaiah 42:11

Jangwa na miji yake na ipaze sauti zao, Vijiji vinavyokaliwa na Kedari; Na waimbe wenyeji wa Sela, Wapige kelele toka vilele vya milima.

Isaya 42:12 Isaiah 42:12

Na wamtukuze Bwana, Na kutangaza sifa zake visiwani.

Isaya 42:13 Isaiah 42:13

Bwana atatokea kama shujaa; Ataamsha wivu kama mtu wa vita; Atalia, naam, atapiga kelele; Atawatenda adui zake mambo makuu.

Isaya 42:14 Isaiah 42:14

Siku nyingi nimenyamaza kimya; nimenyamaza, nikajizuia; sasa nitapiga kelele kama mwanamke aliye katika kuzaa; nitaugua na kutweta pamoja.

Isaya 42:15 Isaiah 42:15

Nitaharibu milima na vilima, nitavikausha vyote vimeavyo; nitaifanya mito ya maji kuwa visiwa, na kuyakausha maziwa ya maji.

Isaya 42:16 Isaiah 42:16

Nitawaleta vipofu kwa njia wasiyoijua; katika mapito wasiyoyajua nitawaongoza; nitafanya giza kuwa nuru mbele yao; na mahali palipopotoka kuwa pamenyoka. Haya nitayatenda, wala sitawaacha.

Isaya 42:17 Isaiah 42:17

Watarudishwa nyuma, wataaibishwa sana, hao wanaotumainia sanamu za mawe, na kuziambia sanamu za madini, Ninyi ndinyi miungu yetu.

Isaya 42:18 Isaiah 42:18

Sikilizeni, enyi viziwi; tazameni, enyi vipofu, mpate kuona.

Isaya 42:19 Isaiah 42:19

Ni nani aliye kipofu, ila mtumishi wangu? Au aliye kiziwi, kama mjumbe wangu nimtumaye? Ni nani aliye kipofu, kama yeye aliye na amani? Naam, kipofu kama mtumishi wa Bwana?

Isaya 42:20 Isaiah 42:20

Unaona mambo mengi, lakini huyatii moyoni; masikio yake ya wazi, lakini hasikii.

Isaya 42:21 Isaiah 42:21

Bwana akapendezwa, kwa ajili ya haki yake, kuitukuza sheria, na kuiadhimisha.

Isaya 42:22 Isaiah 42:22

Lakini watu hawa ni watu walioibiwa na kutekwa; wote wamenaswa katika mashimo, wamefichwa katika magereza; wamekuwa mawindo, wala hapana aokoaye; wamekuwa mateka, wala hapana asemaye, Rudisha.

Isaya 42:23 Isaiah 42:23

Ni nani miongoni mwenu atakayetega sikio lake kuyasikia hayo? Atakayesikiliza na kusikia kwa wakati ujao?

Isaya 42:24 Isaiah 42:24

Ni nani aliyemtoa Yakobo awe mateka, aliyemtia Israeli katika mikono ya wanyang'anyi? Si yeye, Bwana? Yeye tuliyemkosa, ambaye hawakutaka kwenda katika njia zake, wala hawakuitii sheria yake.

Isaya 42:25 Isaiah 42:25

Kwa sababu hiyo alimwaga ukali wa hasira yake juu yake, na nguvu za vita; ukawasha moto wa kumzunguka pande zote, wala hakujua; ukamteketeza, wala hakuyatia hayo moyoni mwake.