Isaya Mlango 43 Isaiah

Isaya 43:1 Isaiah 43:1

Lakini sasa, Bwana aliyekuhuluku, Ee Yakobo, yeye aliyekuumba, Ee Israeli, asema hivi, Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu.

Isaya 43:2 Isaiah 43:2

Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.

Isaya 43:3 Isaiah 43:3

Maana mimi ni Bwana, Mungu wako; Mtakatifu wa Israeli, mwokozi wako, nimetoa Misri kuwa ukombozi wako; nimetoa Kushi na Seba kwa ajili yako.

Isaya 43:4 Isaiah 43:4

Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako.

Isaya 43:5 Isaiah 43:5

Usiogope; maana mimi ni pamoja nawe; nitaleta wazao wako toka mashariki, nitakukusanya toka magharibi;

Isaya 43:6 Isaiah 43:6

nitaiambia kaskazi, Toa; nayo kusi, Usizuie; waleteni wana wangu kutoka mbali, na binti zangu kutoka miisho ya dunia.

Isaya 43:7 Isaiah 43:7

Kila mmoja aliyeitwa kwa jina langu, niliyemwumba kwa ajili ya utukufu wangu; mimi nimemwumba, naam, mimi nimemfanya.

Isaya 43:8 Isaiah 43:8

Walete vipofu walio na macho, na viziwi walio na masikio.

Isaya 43:9 Isaiah 43:9

Na wakusanyike mataifa yote, kabila zote wakutanike; ni nani miongoni mwao awezaye kuhubiri neno hili, na kutuonyesha mambo ya zamani? Na walete mashahidi wao, wapate kuhesabiwa kuwa na haki; au na wasikie, wakaseme, Ni kweli.

Isaya 43:10 Isaiah 43:10

Ninyi ni mashahidi wangu, asema Bwana, na mtumishi niliyemchagua; mpate kujua, na kuniamini, na kufahamu ya kuwa mimi ndiye; kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine.

Isaya 43:11 Isaiah 43:11

Mimi, naam, mimi, ni Bwana, zaidi yangu mimi hapana mwokozi.

Isaya 43:12 Isaiah 43:12

Nimetangaza habari, nimeokoa, nimeonyesha, na hapakuwa mungu wa kigeni kati yenu; kwa sababu hiyo ninyi ni mashahidi wangu, asema Bwana, nami ni Mungu.

Isaya 43:13 Isaiah 43:13

Naam, tangu siku ya leo, mimi ndiye; wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu; mimi nitatenda kazi, naye ni nani awezaye kuizuia?

Isaya 43:14 Isaiah 43:14

Bwana, Mkombozi wenu, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi; Kwa ajili yenu nimetuma ujumbe Babeli nami nitawashusha wote mfano wa wakimbizi, naam, Wakaldayo, katika merikebu zao walizozifurahia.

Isaya 43:15 Isaiah 43:15

Mimi ni Bwana, Mtakatifu wenu, Muumba wa Israeli, mfalme wenu.

Isaya 43:16 Isaiah 43:16

Bwana asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari; na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu;

Isaya 43:17 Isaiah 43:17

atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano wa utambi.

Isaya 43:18 Isaiah 43:18

Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani.

Isaya 43:19 Isaiah 43:19

Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je! Hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani.

Isaya 43:20 Isaiah 43:20

Wanyama wa kondeni wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu;

Isaya 43:21 Isaiah 43:21

watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.

Isaya 43:22 Isaiah 43:22

Lakini hukuniita, Ee Yakobo, bali umechoka nami, Ee Israeli.

Isaya 43:23 Isaiah 43:23

Hukuniletea wana-kondoo kuwa kafara zako, wala hukuniheshimu kwa dhabihu zako. Sikukutumikisha kwa matoleo, wala sikukuchosha kwa ubani.

Isaya 43:24 Isaiah 43:24

Hukuninunulia manukato kwa fedha, wala hukunishibisha kwa mafuta ya sadaka zako; bali umenitumikisha kwa dhambi zako, umenichosha kwa maovu yako.

Isaya 43:25 Isaiah 43:25

Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.

Isaya 43:26 Isaiah 43:26

Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.

Isaya 43:27 Isaiah 43:27

Baba yako wa kwanza alifanya dhambi, na wakalimani wako wameniasi.

Isaya 43:28 Isaiah 43:28

Kwa hiyo nitawatia unajisi wakuu wa patakatifu, nami nitamfanya Yakobo kuwalaani, na Israeli kuwa tukano.