Isaya Mlango 50 Isaiah

Isaya 50:1 Isaiah 50:1

Bwana asema hivi, Iko wapi hati ya talaka ya mama yenu, ambayo kwa hiyo naliachana naye? Au nimewauza ninyi kwa nani katika watu wanaoniwia? Ninyi mliuzwa kwa sababu ya maovu yenu; tena mama yenu ameachwa kwa sababu ya makosa yenu.

Isaya 50:2 Isaiah 50:2

Basi, nilipokuja, mbona hapakuwa na mtu? Nilipoita, mbona hapakuwa na mtu aliyenijibu? Je! Mkono wangu ni mfupi, hata nisiweze kukomboa? Au je! Mimi sina nguvu za kuponya? Tazama, kwa kukemea kwangu naikausha bahari, mito ya maji naifanya kuwa jangwa; samaki wao wanuka kwa sababu hapana maji, nao wafa kwa kiu.

Isaya 50:3 Isaiah 50:3

Mimi nazivika mbingu weusi, nami nafanya nguo ya magunia kuwa kifuniko chao.

Isaya 50:4 Isaiah 50:4

Bwana MUNGU amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao.

Isaya 50:5 Isaiah 50:5

Bwana MUNGU amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma.

Isaya 50:6 Isaiah 50:6

Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang'oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate.

Isaya 50:7 Isaiah 50:7

Maana Bwana MUNGU atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.

Isaya 50:8 Isaiah 50:8

Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi.

Isaya 50:9 Isaiah 50:9

Tazama, Bwana MUNGU atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa? Tazama hao wote watachakaa kama vazi; nondo atawala.

Isaya 50:10 Isaiah 50:10

Ni nani miongoni mwenu amchaye Bwana, aitiiye sauti ya mtumishi wake? Yeye aendaye katika giza, wala hana nuru, naye alitumainia jina la Bwana, na kumtegemea Mungu wake.

Isaya 50:11 Isaiah 50:11

Tazama, ninyi nyote mwashao moto, mjifungiao hiyo mienge; endeni ninyi katika mwali wa moto wenu, na katikati ya mienge mliyoiwasha. Mtayapata haya kwa mkono wangu; mtalala kwa huzuni.