Isaya Mlango 11 Isaiah

Isaya 11:1 Isaiah 11:1

Basi litatoka chipukizi katika shina la Yese, na tawi litakalotoka katika mizizi yake litazaa matunda.

Isaya 11:2 Isaiah 11:2

Na roho ya Bwana atakaa juu yake, roho ya hekima na ufahamu, roho ya shauri na uweza, roho ya maarifa na ya kumcha Bwana;

Isaya 11:3 Isaiah 11:3

na furaha yake itakuwa katika kumcha Bwana; wala hatahukumu kwa kuyafuata ayaonayo kwa macho yake, wala hataonya kwa kuyafuata ayasikiayo kwa masikio yake;

Isaya 11:4 Isaiah 11:4

bali kwa haki atawahukumu maskini, naye atawaonya wanyenyekevu wa dunia kwa adili; naye ataipiga dunia kwa fimbo ya kinywa chake, na kwa pumzi ya midomo yake atawaua wabaya.

Isaya 11:5 Isaiah 11:5

Na haki itakuwa mshipi wa viuno vyake, na uaminifu mshipi wa kujifungia.

Isaya 11:6 Isaiah 11:6

Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.

Isaya 11:7 Isaiah 11:7

Ng'ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng'ombe.

Isaya 11:8 Isaiah 11:8

Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.

Isaya 11:9 Isaiah 11:9

Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.

Isaya 11:10 Isaiah 11:10

Na itakuwa katika siku hiyo, shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta; na mahali pake pa kupumzikia patakuwa na utukufu.

Isaya 11:11 Isaiah 11:11

Na itakuwa katika siku hiyo, Bwana atapeleka mkono wake mara ya pili, ili ajipatie watu wake watakaosalia, kutoka Ashuru, na kutoka Misri, na kutoka Pathrosi, na kutoka Kushi, na kutoka Elamu, na kutoka Shinari, na kutoka Hamathi, na kutoka visiwa vya bahari.

Isaya 11:12 Isaiah 11:12

Naye atawatwekea mataifa bendera, atawakutanisha watu wa Israeli waliotupwa, atawakusanya watu wa Yuda waliotawanyika, kutoka ncha nne za dunia.

Isaya 11:13 Isaiah 11:13

Na wivu wa Efraimu utaondoka, na wale wanaomwudhi Yuda watakatiliwa mbali; Efraimu hatamhusudu Yuda, wala Yuda hatamwudhi Efraimu.

Isaya 11:14 Isaiah 11:14

Nao watashuka, watalirukia bega la Wafilisti upande wa magharibi; nao pamoja watawateka wana wa mashariki; watanyosha mkono juu ya Edomu na Moabu; na wana wa Amoni watawatii.

Isaya 11:15 Isaiah 11:15

Na Bwana atauangamiza kabisa ulimi wa bahari ya Misri; na kwa upepo wake uteketezao atatikisa mkono wake juu ya Mto, naye ataupiga, uwe vijito saba, na kuwavusha watu wenye viatu vikavu.

Isaya 11:16 Isaiah 11:16

Itakuwako njia kuu kwa mabaki ya watu wake watakaobaki, watokao Ashuru, kama vile ilivyokuwako kwa Israeli, katika siku ile waliyotoka katika nchi ya Misri.