Isaya Mlango 22 Isaiah

Isaya 22:1 Isaiah 22:1

Ufunuo juu ya bonde la maono. Sasa una nini, wewe, Hata umepanda pia juu ya dari za nyumba?

Isaya 22:2 Isaiah 22:2

Ewe uliyejaa makelele, Mji wa ghasia, mji wenye furaha; Watu wako waliouawa hawakuuawa kwa upanga, Wala hawakufa vitani.

Isaya 22:3 Isaiah 22:3

Wakuu wako wote wamekimbia pamoja, Wamefungwa wasiutumie upinde. Wote walioonekana wamefungwa pamoja, Wamekimbia mbali sana.

Isaya 22:4 Isaiah 22:4

Kwa sababu hiyo nasema, Geuza uso wako usinitazame, nipate kulia kwa uchungu; usijishughulishe kunifariji, kwa ajili ya kuharibika kwake binti ya watu wangu.

Isaya 22:5 Isaiah 22:5

Kwa maana siku ya kutaabika, siku ya kukanyagwa, siku ya fujo inakuja, itokayo kwa Bwana, Bwana wa majeshi, katika bonde la Maono; inabomoa kuta; na kuililia milima.

Isaya 22:6 Isaiah 22:6

Na Elamu wameshika podo, pamoja na magari ya vita, na watu wenye kupanda farasi; na Kiri wameifunua ngao.

Isaya 22:7 Isaiah 22:7

Hata ikawa mabonde yako mateule yamejaa magari ya vita, nao wapandao farasi wamejipanga wakielekea malango.

Isaya 22:8 Isaiah 22:8

Kisha alikiondoa kifuniko cha Yuda, nawe siku hiyo ulivitazama vyombo vya vita katika nyumba ya mwituni.

Isaya 22:9 Isaiah 22:9

Nanyi mlipaona mahali palipobomoka katika mji wa Daudi ya kuwa ni pengi, nanyi mliyakusanya maji ya birika la chini.

Isaya 22:10 Isaiah 22:10

Nanyi mlizihesabu nyumba za Yerusalemu, mkazibomoa nyumba ili kuutia nguvu ukuta.

Isaya 22:11 Isaiah 22:11

Nanyi mlifanya birika la maji katikati ya kuta mbili, la kuwekea maji ya birika la kale; lakini hamkumwangalia yeye aliyeyafanya hayo, wala kumjali yeye aliyeyatengeneza zamani.

Isaya 22:12 Isaiah 22:12

Siku hiyo Bwana, Bwana wa majeshi, akawaita watu walie na kuomboleza, na kung'oa nywele zao, na kuvaa nguo za magunia;

Isaya 22:13 Isaiah 22:13

na kumbe! Furaha, na kuchekelea, na kuchinja ng'ombe, na kuchinja kondoo, na kula nyama, na kunywa mvinyo; tule, tunywe, kwa maana kesho tutakufa.

Isaya 22:14 Isaiah 22:14

Na yeye Bwana wa majeshi akafunua haya masikioni mwangu, Ni kweli, uovu huu hautatakaswa wala kuwatokeni hata mfe; asema Bwana, Bwana wa majeshi.

Isaya 22:15 Isaiah 22:15

Bwana, Bwana wa majeshi, asema hivi, Haya! Enenda kwa huyu mtunza hazina, yaani, Shebna, aliye juu ya nyumba, ukamwambie,

Isaya 22:16 Isaiah 22:16

Unafanyaje hapa? Nawe una nani hapa? Hata ukachimba kaburi hapa; ukamchimbia kaburi huko juu, na kumchongea makao katika jabali!

Isaya 22:17 Isaiah 22:17

Tazama, Bwana atakutupa kwa nguvu, kama mtu mwenye nguvu; naam, atakuzonga-zonga.

Isaya 22:18 Isaiah 22:18

Hakika atakukunja na kukutupa kama mpira, mpaka nchi iliyo mbali; huko utakufa, na magari ya utukufu wako yatakuwa kuko huko, ewe uliye aibu ya nyumba ya bwana wako.

Isaya 22:19 Isaiah 22:19

Nami nitakusukuma na kukutoa katika mahali pako, naye atakushusha utoke hapa usimamapo.

Isaya 22:20 Isaiah 22:20

Na itakuwa katika siku ile nitamwita mtumishi wangu Eliakimu, mwana wa Hilkia;

Isaya 22:21 Isaiah 22:21

nami nitamvika vazi lako, nitamtia nguvu kwa mshipi wako, nami nitamkabidhi yeye mamlaka yako; naye atakuwa baba kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa nyumba ya Yuda.

Isaya 22:22 Isaiah 22:22

Na ufunguo wa nyumba ya Daudi nitauweka begani mwake; yeye atafungua wala hapana atakayefunga; naye atafunga wala hapana atakayefungua.

Isaya 22:23 Isaiah 22:23

Nami nitamkaza kama msumari mahali palipo imara; naye atakuwa kiti cha utukufu kwa nyumba ya baba yake.

Isaya 22:24 Isaiah 22:24

Nao wataangika juu yake utukufu wote wa nyumba ya baba yake; wazao wake na watoto wao, kila chombo kidogo tangu vyombo vya vikombe hata vyombo vya makopo vyote pia.

Isaya 22:25 Isaiah 22:25

Katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, ule msumari uliokazwa katika mahali palipo imara utalegea; nao utakatwa na kuanguka chini, na ule mzigo uliokuwa juu yake utakatiliwa mbali; maana Bwana amesema haya.