Isaya Mlango 65 Isaiah

Isaya 65:1 Isaiah 65:1

Watu wasionitaka wanauliza habari zangu; nimeonekana na hao wasionitafuta; naliliambia taifa lisiloitwa kwa jina langu,

Isaya 65:2 Isaiah 65:2

Nitazameni, nitazameni. Mchana kutwa nimewanyoshea mikono yangu watu walioasi, watu waendao katika njia isiyo njema, wakifuata mawazo yao wenyewe;

Isaya 65:3 Isaiah 65:3

watu wanikasirishao mbele za uso wangu daima, wakitoa dhabihu katika bustani zao, na kufukiza uvumba juu ya matofali;

Isaya 65:4 Isaiah 65:4

waketio kati ya makaburi, na kulala katika mahali pao pa siri; walao nyama ya nguruwe, na mchuzi wa vitu vinichukizavyo u katika vyombo vyao;

Isaya 65:5 Isaiah 65:5

watu wasemao, Simama peke yako, usinikaribie mimi, kwa maana mimi ni mtakatifu kuliko wewe; watu hao ni moshi puani mwangu, moto uwakao mchana kutwa.

Isaya 65:6 Isaiah 65:6

Tazama, neno hili limeandikwa mbele zangu. Sitanyamaza, lakini nitalipa, naam, mimi nitawalipa ujira wao vifuani mwao;

Isaya 65:7 Isaiah 65:7

maovu yenu na maovu ya baba zenu pamoja, asema Bwana, ninyi mliofukiza uvumba juu ya milima, na kunitukana juu ya vilima; basi, kwa ajili ya hayo nitawapimia kwanza kazi yao vifuani mwao.

Isaya 65:8 Isaiah 65:8

Bwana asema hivi, Kama vile divai mpya ipatikanavyo katika kichala, na mtu mmoja husema, Usikiharibu kwa maana mna baraka ndani yake; ndivyo nitakavyotenda kwa ajili ya watumishi wangu, ili nisiwaharibu wote.

Isaya 65:9 Isaiah 65:9

Nami nitaleta uzao toka Yakobo, na mrithi wa milima yangu toka Yuda, na mteule wangu atairithi, na watumishi wangu watakaa huko.

Isaya 65:10 Isaiah 65:10

Na Sharoni itakuwa zizi la makundi ya kondoo, na bonde la Akori mahali pa kulala makundi ya ng'ombe, kwa ajili ya watu wangu walionitafuta.

Isaya 65:11 Isaiah 65:11

Bali ninyi mmwachao Bwana, na kuusahau mlima wangu mtakatifu, na kuandika meza kwa ajili ya Bahati, na kuijazia Ajali vyombo vya divai iliyochanganyika;

Isaya 65:12 Isaiah 65:12

mimi nitawaandikia kuuawa kwa upanga, na ninyi nyote mtainama ili kuchinjwa; kwa sababu nilipoita hamkuitika; niliponena, hamkusikia; bali mlitenda yaliyo mabaya machoni pangu, mlichagua mambo nisiyoyafurahia.

Isaya 65:13 Isaiah 65:13

Kwa hiyo Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, watumishi wangu watakula, bali ninyi mtaona njaa; tazama, watumishi wangu watakunywa, bali ninyi mtaona kiu; tazama, watumishi wangu watafurahi, bali ninyi mtatahayarika;

Isaya 65:14 Isaiah 65:14

tazama, watumishi wangu wataimba kwa furaha ya moyo, bali ninyi mtalia kwa huzuni ya moyo; mtapiga kelele kwa sababu ya uchungu wa roho zenu.

Isaya 65:15 Isaiah 65:15

Nanyi mtaliacha jina lenu kuwa laana kwa wateule wangu. Na Bwana MUNGU atakuua; naye atawaita watumishi wake kwa jina lingine.

Isaya 65:16 Isaiah 65:16

Hata itakuwa yeye atakayejibariki duniani, atajibariki kwa Mungu wa kweli; naye atakayeapa duniani, ataapa kwa Mungu wa kweli. Kwa kuwa taabu za kwanza zimesahauliwa, na kwa kuwa zimefichwa machoni pangu.

Isaya 65:17 Isaiah 65:17

Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni.

Isaya 65:18 Isaiah 65:18

Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.

Isaya 65:19 Isaiah 65:19

Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza.

Isaya 65:20 Isaiah 65:20

Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa.

Isaya 65:21 Isaiah 65:21

Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.

Isaya 65:22 Isaiah 65:22

Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.

Isaya 65:23 Isaiah 65:23

Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na Bwana, na watoto wao pamoja nao.

Isaya 65:24 Isaiah 65:24

Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia.

Isaya 65:25 Isaiah 65:25

Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng'ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema Bwana.