Isaya Mlango 36 Isaiah

Isaya 36:1 Isaiah 36:1

Ikawa, katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa.

Isaya 36:2 Isaiah 36:2

Mfalme wa Ashuru akamtuma amiri toka Lakishi hata Yerusalemu,kwa mfalme Hezekia,pamoja na jeshi kubwa. Naye akasimama karibu na mfereji wa birika ya juu,iliyo katika njia kuu ya kuuendea uwanda wa dobi.

Isaya 36:3 Isaiah 36:3

Wakamtokea Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe.

Isaya 36:4 Isaiah 36:4

Yule amiri akawaambia, Haya, mwambieni Hezekia, kwamba mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia?

Isaya 36:5 Isaiah 36:5

Nasema, mashauri yako, na nguvu zako kwa vita, ni maneno yasiyo na maana; basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi?

Isaya 36:6 Isaiah 36:6

Tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliopondeka, yaani, Misri, ambayo, mtu akitegemea juu yake, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio.

Isaya 36:7 Isaiah 36:7

Lakini ukiniambia, Tunamtumaini Bwana, Mungu wetu, je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake mlimoinuka, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii?

Isaya 36:8 Isaiah 36:8

Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao.

Isaya 36:9 Isaiah 36:9

Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa akida mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi?

Isaya 36:10 Isaiah 36:10

Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la Bwana? Bwana ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza.

Isaya 36:11 Isaiah 36:11

Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule amiri, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa watu wote walio ukutani.

Isaya 36:12 Isaiah 36:12

Lakini yule amiri akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma kwa bwana wako, na kwako wewe, niseme maneno haya? Hakunituma kwa watu hawa walio ukutani, ili wale mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi?

Isaya 36:13 Isaiah 36:13

Kisha yule amiri akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akisema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru.

Isaya 36:14 Isaiah 36:14

Mfalme asema hivi; Hezekia asiwadanganye, kwa maana hataweza kuwaokoa;

Isaya 36:15 Isaiah 36:15

wala msimwache Hezekia kuwatia moyo wa kumtumaini Bwana; akisema, Bwana bila shaka atatuokoa, mji huu hautatiwa katika mkono wa mfalme wa Ashuru.

Isaya 36:16 Isaiah 36:16

Msimsikilize Hezekia; maana mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie, mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika yake mwenyewe;

Isaya 36:17 Isaiah 36:17

hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya mkate na mashamba ya mizabibu.

Isaya 36:18 Isaiah 36:18

Jihadharini, asije Hezekia akawadanganya, akisema, Bwana atatuokoa. Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake na mkono wa mfalme wa Ashuru?

Isaya 36:19 Isaiah 36:19

Wako wapi miungu ya Hamathi na ya Arpadi? Wako wapi miungu ya Sefarvaimu? Je! Wameiokoa Samaria na mkono wangu?

Isaya 36:20 Isaiah 36:20

Katika miungu yote ya nchi hizi ni nani waliookoa nchi yao na mkono wangu, hata Bwana auokoe Yerusalemu na mkono wangu?

Isaya 36:21 Isaiah 36:21

Lakini watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana ilikuwa amri ya mfalme, kwamba, Msimjibu neno.

Isaya 36:22 Isaiah 36:22

Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu mwenye kuandika tarehe, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zimeraruliwa, wakamwambia Hezekia maneno ya yule amiri.