Isaya Mlango 41 Isaiah

Isaya 41:1 Isaiah 41:1

Nyamazeni mbele zangu, enyi visiwa, na mataifa wajipatie nguvu mpya; na waje karibu wakanene; na tukaribiane pamoja kwa hukumu.

Isaya 41:2 Isaiah 41:2

Ni nani aliyemwinua mmoja atokaye mashariki, ambaye katika haki amemwita mguuni pake? Ampa mataifa mbele yake, na kumtawaza juu ya wafalme; awatoa wawe kama mavumbi kwa upanga wake, kama makapi yaliyopeperushwa kwa upinde wake.

Isaya 41:3 Isaiah 41:3

Awafuatia, apita salama hata kwa njia asiyoikanyaga kamwe kwa miguu yake.

Isaya 41:4 Isaiah 41:4

Ni nani aliyetenda na kufanya jambo hilo, aviitaye vizazi tangu mwanzo? Mimi, Bwana, wa kwanza na wa mwisho, mimi ndiye.

Isaya 41:5 Isaiah 41:5

Visiwa vimeona, vikaogopa; ncha za dunia zilitetemeka; walikaribia, walikuja.

Isaya 41:6 Isaiah 41:6

Wakasaidiana, kila mtu na mwenzake, kila mtu akamwambia ndugu yake; Uwe na moyo mkuu.

Isaya 41:7 Isaiah 41:7

Seremala akamtia moyo mfua dhahabu, na yeye alainishaye kwa nyundo akamhimiza yule apigaye fuawe, akiisifu kazi ya kuunga, akisema, Ni kazi njema; naye akaikaza kwa misumari isitikisike.

Isaya 41:8 Isaiah 41:8

Nawe, Israeli, mtumishi wangu; Yakobo, niliyekuchagua; mzao wa Ibrahimu, rafiki yangu;

Isaya 41:9 Isaiah 41:9

wewe niliyekushika toka miisho ya dunia, na kukuita toka pembe zake, nikikuambia, Wewe u mtumishi wangu; nimekuchagua wala sikukutupa;

Isaya 41:10 Isaiah 41:10

usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu, naam, nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu.

Isaya 41:11 Isaiah 41:11

Tazama, wote walioona hasira juu yako watatahayarika na kufadhaika; watu washindanao nawe watakuwa si kitu, na kuangamia.

Isaya 41:12 Isaiah 41:12

Utawatafuta wala hutawaona wale wapiganao nawe; watakuwa si kitu; watakuwa kama kitu kisichokuwa, wale waliofanya vita juu yako.

Isaya 41:13 Isaiah 41:13

Kwa maana mimi, Bwana, Mungu wako, nitakushika mkono wako wa kuume, nikikuambia, Usiogope; mimi nitakusaidia.

Isaya 41:14 Isaiah 41:14

Usiogope, Yakobo uliye mdudu, nanyi watu wa Israeli; mimi nitakusaidia, asema Bwana, na mkombozi wako ni Mtakatifu wa Israeli.

Isaya 41:15 Isaiah 41:15

Tazama, nitakufanya kuwa chombo kikali kipya cha kupuria, chenye meno; utaifikicha milima, na kuisaga; nawe utafanya vilima kuwa kama makapi.

Isaya 41:16 Isaiah 41:16

Utawapepeta, na upepo utawapeperusha; upepo wa kisulisuli utawatawanya; nawe utamfurahia Bwana, utajitukuza katika Mtakatifu wa Israeli.

Isaya 41:17 Isaiah 41:17

Maskini na wahitaji wanatafuta maji, wala hapana; ndimi zao zimekauka kwa kiu; mimi, Bwana, nitawasikia, mimi, Mungu wa Israeli, sitawaacha.

Isaya 41:18 Isaiah 41:18

Nitafunua vijito vya maji juu ya vilima, na chemchemi katikati ya mabonde; nitageuza jangwa kuwa ziwa la maji, na mahali pakavu kuwa vijito vya maji.

Isaya 41:19 Isaiah 41:19

Nitapanda katika jangwa mwerezi, mshita, mhadasi, na mbono; nitatia katika nyika mberoshi, mtidhari, na mteashuri pamoja;

Isaya 41:20 Isaiah 41:20

ili waone, na kujua, wakafikiri, na kufahamu pamoja, ya kuwa mkono wa Bwana ndio uliofanya jambo hilo. Mtakatifu wa Israeli ndiye aliyeliumba.

Isaya 41:21 Isaiah 41:21

Haya, leteni maneno yenu, asema Bwana; toeni hoja zenu zenye nguvu, asema mfalme wa Yakobo.

Isaya 41:22 Isaiah 41:22

Wayatangaze na kutujulisha yatakayokuwa; watuonyeshe mambo ya zamani, ni mambo gani, tukapate kuyatia moyoni, tukajue mwisho wake; au wamdhihirishie yatakayotokea baadaye.

Isaya 41:23 Isaiah 41:23

Tujulisheni yatakayokuwa baadaye, nasi tutakiri ya kuwa ninyi ni miungu; naam, tendeni mema au tendeni mabaya, ili tujipime, tukaone pamoja.

Isaya 41:24 Isaiah 41:24

Tazameni, ninyi si kitu, tena kazi yenu si kitu; awachaguaye ninyi ni chukizo.

Isaya 41:25 Isaiah 41:25

Nimemwinua mtu toka kaskazini, naye amekuja; toka maawio ya jua amekuja anitajaye jina langu; naye atawajilia maliwali kama akanyagaye matope, na kama mfinyanzi afinyangaye udongo.

Isaya 41:26 Isaiah 41:26

Ni nani aliyeihubiri habari tokea mwanzo, tupate kuijua? Na tokea zamani, tupate kusema, Yeye ni mwenye haki? Naam, hapana hata mmoja aliyetujulisha; naam, hapana hata mmoja aliyetuonyesha; naam, hapana hata mmoja aliyesikia maneno yenu.

Isaya 41:27 Isaiah 41:27

Mimi kwanza nitauambia Sayuni, Tazama; hawa ndio; nami nitampa Yerusalemu mletaji wa habari njema.

Isaya 41:28 Isaiah 41:28

Na nitazamapo, hapana mtu, hata katika watu hao hapana mshauri mmoja, ambaye, nikimwuliza, aweza kunijibu neno.

Isaya 41:29 Isaiah 41:29

Tazama, hao wote ni ubatili; kazi zao si kitu; sanamu zao ni upepo na fujo.