Isaya Mlango 30 Isaiah

Isaya 30:1 Isaiah 30:1

Ole wa watoto waasi; asema Bwana; watakao mashauri lakini hawayataki kwangu mimi; wajifunikao kifuniko lakini si cha roho yangu; wapate kuongeza dhambi juu ya dhambi;

Isaya 30:2 Isaiah 30:2

waendao kutelemkia Misri wala hawakuuliza kinywani mwangu; ili wajitie nguvu kwa nguvu za Farao, na kutumainia kivuli cha Misri.

Isaya 30:3 Isaiah 30:3

Basi, nguvu za Farao zitakuwa aibu yenu, na kutumainia kivuli cha Misri kutakuwa kufadhaika kwenu.

Isaya 30:4 Isaiah 30:4

Kwa maana wakuu wake wako Soani, na wajumbe wake wamefika Hanesi.

Isaya 30:5 Isaiah 30:5

Wote watawaonea haya watu wasioweza kuwafaidia, wasio na msaada wala faida, bali ni aibu na sababu ya kushutumiwa.

Isaya 30:6 Isaiah 30:6

Ufunuo juu ya hayawani wa Negebu. Katikati ya nchi ya taabu na dhiki, Ambayo hutoka huko simba jike na simba, Nyoka na joka la moto arukaye, Huchukua mali zao mabegani mwa punda wachanga, Na hazina zao juu ya nundu za ngamia Waende kwa watu ambao hawatawafaa kitu.

Isaya 30:7 Isaiah 30:7

Kwa maana Misri huwasaidia bure, bila faida; Kwa hiyo nimemwita, Rahabu aketiye kimya.

Isaya 30:8 Isaiah 30:8

Haya, enenda sasa, andika neno hili katika kibao mbele ya macho yao, lichore katika kitabu ili liwe kwa ajili ya majira yatakayokuja, kwa ushuhuda hata milele.

Isaya 30:9 Isaiah 30:9

Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya Bwana;

Isaya 30:10 Isaiah 30:10

wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, tuambieni maneno laini, hubirini maneno yadanganyayo;

Isaya 30:11 Isaiah 30:11

tokeni katika njia, geukeni mtoke katika mapito; mkomesheni Mtakatifu wa Israeli mbele yetu.

Isaya 30:12 Isaiah 30:12

Basi kwa ajili ya hayo Mtakatifu wa Israeli asema hivi, Kwa sababu mwalidharau neno hili, na kutumainia jeuri na ukaidi, na kuyategemea hayo;

Isaya 30:13 Isaiah 30:13

basi, uovu huu utakuwa kwenu kama mahali palipobomoka, palipo tayari kuanguka patokezapo katika ukuta mrefu, ambapo kuvunjika kwake huja ghafula kwa mara moja.

Isaya 30:14 Isaiah 30:14

Naye atapavunja kama chombo cha mfinyanzi kivunjwavyo, akikivunja-vunja asiache kukivunja, hata hakipatikani katika vipande vyake kigae kitoshacho kutwaa moto jikoni, au kuteka maji kisimani.

Isaya 30:15 Isaiah 30:15

Kwa maana Bwana MUNGU, Mtakatifu wa Israeli, asema hivi, Kwa kurudi na kustarehe mtaokolewa; nguvu zenu zitakuwa katika kutulia na kutumaini; lakini hamkukubali.

Isaya 30:16 Isaiah 30:16

Bali ninyi mlisema, La! Maana tutakimbia juu ya farasi; basi, ni kweli, mtakimbia; tena, Sisi tutakimbia juu ya wanyama waendao upesi; basi, wale watakaowafuatia watakuwa wepesi.

Isaya 30:17 Isaiah 30:17

Elfu moja watakimbia kwa kukemewa na mtu mmoja; kwa kukemewa na watano mtakimbia; hata mtakapoachwa kama mlingoti juu ya kilele cha mlima, na kama bendera juu ya kilima.

Isaya 30:18 Isaiah 30:18

Kwa ajili ya hayo Bwana atangoja, ili awaonee huruma, na kwa ajili ya hayo atatukuzwa, ili awarehemu; kwa maana Bwana ni Mungu wa hukumu; heri wote wamngojao.

Isaya 30:19 Isaiah 30:19

Kwa maana watu watakaa katika Sayuni huko Yerusalemu; wewe hutalia tena; hakika yake atakuonea rehema nyingi kwa sauti ya kilio chako; asikiapo ndipo atakapokujibu.

Isaya 30:20 Isaiah 30:20

Na ingawa Bwana atawapeni chakula cha shida na maji ya msiba, lakini waalimu wako hawatafichwa tena, ila macho yako yatawaona waalimu wako;

Isaya 30:21 Isaiah 30:21

na masikio yako yatasikia neno nyuma yako, likisema, Njia ni hii, ifuateni; mgeukapo kwenda mkono wa kulia, na mgeukapo kwenda mkono wa kushoto.

Isaya 30:22 Isaiah 30:22

Nanyi mtakitia najisi kifuniko cha sanamu zenu za fedha zilizochongwa, na mabamba ya sanamu zenu za dhahabu zilizoyeyushwa; utazitupilia mbali kama kitu kilicho najisi; utasema, Haya, toka hapa.

Isaya 30:23 Isaiah 30:23

Naye atatoa mvua juu ya mbegu zako, upate kuipanda nchi hii; na mkate wa mazao ya nchi, nayo itasitawi na kuzaa tele; katika siku hiyo ng'ombe zako watakula katika malisho mapana.

Isaya 30:24 Isaiah 30:24

Ng'ombe pia na wana-punda wailimao nchi watakula chakula kilichokolea, kilichopepetwa kwa ungo na kwa pepeo.

Isaya 30:25 Isaiah 30:25

Na juu ya kila mlima mrefu, na juu ya kila kilima kilichoinuka, itakuwapo mito na vijito vya maji, katika siku ya machinjo makuu itakapoanguka minara.

Isaya 30:26 Isaiah 30:26

Na tena nuru ya mwezi itakuwa kama nuru ya jua, na nuru ya jua itaongezeka mara saba, kama nuru ya siku saba, katika siku ile Bwana atakapofunga mapigo ya watu wake, na kuliponya pigo la jeraha yao.

Isaya 30:27 Isaiah 30:27

Tazama, jina la Bwana linakuja kutoka mbali sana, linawaka kwa hasira yake, kwa moshi mwingi sana unaopaa juu; midomo yake imejaa ghadhabu, na ulimi wake ni moto ulao;

Isaya 30:28 Isaiah 30:28

na pumzi yake ni kijito kifurikacho, kifikacho hata shingoni, kupepeta mataifa kwa ungo wa ubatili; na lijamu ikoseshayo itakuwa katika taya za watu.

Isaya 30:29 Isaiah 30:29

Mtakuwa na wimbo kama vile wakati wa usiku, ishikwapo sikukuu takatifu, mtakuwa na furaha ya moyo kama vile mtu aendapo na filimbi katika mlima wa Bwana, aliye Mwamba wa Israeli.

Isaya 30:30 Isaiah 30:30

Naye Bwana atawasikizisha watu sauti yake ya utukufu, naye atawaonyesha jinsi mkono wake ushukavyo, na ghadhabu ya hasira yake, na mwako wa moto ulao, pamoja na dhoruba, na tufani, na mvua ya mawe ya barafu.

Isaya 30:31 Isaiah 30:31

Maana kwa sauti ya Bwana, Mwashuri atavunjika-vunjika, yeye apigaye kwa bakora.

Isaya 30:32 Isaiah 30:32

Na kila pigo la fimbo iliyoamriwa, ambayo Bwana ataliweka juu yake, litakuwa pamoja na matari na vinanda, na kwa mapigano yenye kutikisa atapigana nao.

Isaya 30:33 Isaiah 30:33

Maana Tofethi imewekwa tayari tokea zamani, naam, imewekwa tayari kwa mfalme huyo; ameifanya kubwa, inakwenda chini sana; tanuru yake ni moto na kuni nyingi; pumzi ya Bwana, kama mto wa kiberiti, huiwasha.