Isaya Mlango 44 Isaiah

Isaya 44:1 Isaiah 44:1

Lakini sikia sasa, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na Israeli, niliyekuchagua;

Isaya 44:2 Isaiah 44:2

Bwana, aliyekufanya, na kukuumba toka tumboni, yeye atakayekusaidia, asema hivi; Usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu; na wewe, Yeshuruni, niliyekuchagua.

Isaya 44:3 Isaiah 44:3

Kwa maana nitamimina maji juu yake aliye na kiu, na vijito vya maji juu ya mahali pakavu; nitamwaga roho yangu juu ya wazao wako, na baraka yangu juu yao utakaowazaa;

Isaya 44:4 Isaiah 44:4

nao watatokea katika manyasi, kama mierebi karibu na mifereji ya maji.

Isaya 44:5 Isaiah 44:5

Mmoja atasema, Mimi ni wa Bwana; na mwingine atajiita kwa jina la Yakobo; na mwingine ataandika juu ya mkono wake, Kwa Bwana, na kujiita kwa jina la Israeli.

Isaya 44:6 Isaiah 44:6

Bwana, Mfalme wa Israeli, Mkombozi wako, Bwana wa majeshi, asema hivi; Mimi ni wa kwanza, na mimi ni wa mwisho; zaidi yangu mimi hapana Mungu.

Isaya 44:7 Isaiah 44:7

Naye ni nani kama mimi atakayeita, na kuyahubiri haya, na kunitengenezea, tangu nilipowaweka watu wa kale? Na mambo yanayokuja na yatakayotokea, wayatangaze.

Isaya 44:8 Isaiah 44:8

Msiogope wala msifanye hofu; je! Sikukuhubiri haya zamani na kuyaonyesha? Na ninyi ni mashahidi wangu. Je! Yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hakika hapana Mwamba; mimi sijui mwingine.

Isaya 44:9 Isaiah 44:9

Wachongao sanamu, wote ni ubatili; wala mambo yao yawapendezayo hayatafaa kitu; wala mashahidi wao wenyewe hawaoni, wala hawajui; ili watahayarike.

Isaya 44:10 Isaiah 44:10

Ni nani aliyejichongea mungu mmoja, au aliyesubu sanamu isiyofaa kitu?

Isaya 44:11 Isaiah 44:11

Tazama, wenziwe wote watatahayari; na mafundi, hao ni wanadamu; na wakusanyike pamoja, wakasimame; wataogopa na kutahayari pamoja.

Isaya 44:12 Isaiah 44:12

Mfua chuma hufanza shoka, hufanya kazi kwa makaa, huitengeneza sanamu kwa nyundo, huifanyiza kwa nguvu za mkono wake; naam, huona njaa, nguvu zake zikampungukia; asipokunywa maji huzimia.

Isaya 44:13 Isaiah 44:13

Seremala hunyosha uzi; huiandika kwa kalamu ya mate; huitengeneza kwa randa, huiandika kwa bikari, huifanza kwa mfano wa mwanadamu, sawasawa na uzuri wa mwanadamu, ili ikae nyumbani.

Isaya 44:14 Isaiah 44:14

Yeye hujikatia mierezi, hutwaa mtiriza, na mwaloni, hujichagulia mti mmoja katika miti ya msituni; hupanda mvinje, mvua ikausitawisha.

Isaya 44:15 Isaiah 44:15

Kisha utamfaa mwanadamu kwa kuni; hutwaa kipande, akaota moto; naam, huuwasha moto, akaoka mkate; naam, huufanya mungu, akauabudu; huifanya sanamu ya kuchonga, akaisujudia.

Isaya 44:16 Isaiah 44:16

Sehemu moja huiteketeza; kwa sehemu nyingine hula nyama; huoka chakula kiokwacho, akashiba; naam, huota moto, akasema, Aha, nimeota moto, nimeona moto;

Isaya 44:17 Isaiah 44:17

na kwa sehemu iliyobakia hufanya mungu, yaani, sanamu yake ya kuchonga; husujudu mbele yake akaiabudu, akaiomba, akasema, Uniokoe; maana wewe u mungu wangu.

Isaya 44:18 Isaiah 44:18

Hawajui wala hawafikiri; maana amewafumba macho, wasione, na mioyo yao, wasiweze kufahamu.

Isaya 44:19 Isaiah 44:19

Wala hapana atiaye moyoni, wala hapana maarifa, wala fahamu kusema, Nimeteketeza sehemu motoni, naam, pia nimeoka mkate juu ya makaa yake; nimeoka nyama nikaila; nami, je! Kilichobaki nikifanye kuwa chukizo? Je! Nisujudie shina la mti?

Isaya 44:20 Isaiah 44:20

Hula majivu; moyo uliodanganyika umempotosha, asiweze kuiokoa nafsi yake, wala kusema, Je! Sio uongo mkononi mwangu?

Isaya 44:21 Isaiah 44:21

Kumbuka haya, Ee Yakobo; nawe Israeli, maana wewe u mtumishi wangu; nimekuumba; u mtumishi wangu; Ee Israeli, hutasahauliwa na mimi.

Isaya 44:22 Isaiah 44:22

Nimeyafuta makosa yako kama wingu zito, na dhambi zako kama wingu; unirudie; maana nimekukomboa.

Isaya 44:23 Isaiah 44:23

Imbeni, enyi mbingu, maana Bwana ametenda hayo; Pigeni kelele, enyi mabonde ya nchi; Pazeni nyimbo, enyi milima; Nawe, msitu, na kila mti ndani yake. Maana Bwana amemkomboa Yakobo, Naye atajitukuza katika Israeli.

Isaya 44:24 Isaiah 44:24

Bwana, mkombozi wako, yeye aliyekuumba tumboni, asema hivi; Mimi ni Bwana, nifanyaye vitu vyote; nizitandaye mbingu peke yangu; niienezaye nchi; ni nani aliye pamoja nami?

Isaya 44:25 Isaiah 44:25

Nizitanguaye ishara za waongo, na kuwatia waganga wazimu; niwarudishaye nyuma wenye hekima, na kuyageuza maarifa yao kuwa ujinga;

Isaya 44:26 Isaiah 44:26

nilithibitishaye neno la mtumishi wangu, na kuyafikiliza mashauri ya wajumbe wangu; niuambiaye Yerusalemu, Utakaliwa na watu, nayo miji ya Yuda, Itajengwa, nami nitapainua mahali pake palipobomoka;

Isaya 44:27 Isaiah 44:27

niviambiaye vilindi, Kauka, nami nitaikausha mito yako;

Isaya 44:28 Isaiah 44:28

nimwambiaye Koreshi, Mchungaji wangu, naye atayatenda mapenzi yangu; hata ataunena Yerusalemu, Utajengwa; na hilo hekalu, Msingi wako utawekwa.