Isaya Mlango 14 Isaiah

Isaya 14:1 Isaiah 14:1

Maana Bwana atamhurumia Yakobo, atamchagua Israeli tena, naye atawaweka katika nchi yao wenyewe; na mgeni atajiunga nao, nao wataambatana na nyumba ya Yakobo.

Isaya 14:2 Isaiah 14:2

Na hao mataifa watawatwaa na kuwaleta mpaka mahali pao wenyewe, na nyumba ya Israeli watawamiliki, na kuwafanya watumishi na wajakazi katika nchi ya Bwana; nao watawachukua hali ya kufungwa watu wale waliowafunga wao, nao watawamiliki watu wale waliowaonea.

Isaya 14:3 Isaiah 14:3

Tena itakuwa katika siku ile, ambayo Bwana atakupa raha baada ya huzuni yako, na baada ya taabu yako, na baada ya utumishi ule mgumu uliotumikishwa;

Isaya 14:4 Isaiah 14:4

utatunga mithali hii juu ya mfalme wa Babeli, na kusema, Jinsi alivyokoma mwenye kuonea; Jinsi ulivyokoma mji ule wenye jeuri!

Isaya 14:5 Isaiah 14:5

Bwana amelivunja gongo la wabaya, Fimbo ya enzi yao wenye kutawala.

Isaya 14:6 Isaiah 14:6

Yeye aliyewapiga mataifa kwa ghadhabu, Kwa mapigo yasiyokoma; Aliyewatawala mataifa kwa hasira, Ameadhibiwa asizuie mtu.

Isaya 14:7 Isaiah 14:7

Dunia yote inastarehe na kutulia; Hata huanzilisha kuimba.

Isaya 14:8 Isaiah 14:8

Naam, misunobari inakufurahia, Na mierezi ya Lebanoni, ikisema, Tokea wakati ulipolazwa chini wewe, Hapana mkata miti aliyetujia.

Isaya 14:9 Isaiah 14:9

Kuzimu chini kumetaharuki kwa ajili yako, Ili kukulaki utakapokuja; Huwaamsha waliokufa kwa ajili yako, Naam, walio wakuu wote wa dunia; Huwainua wafalme wote wa mataifa, Watoke katika viti vyao vya enzi.

Isaya 14:10 Isaiah 14:10

Hao wote watajibu na kukuambia, Je! Wewe nawe umekuwa dhaifu kama sisi! Wewe nawe umekuwa kama sisi!

Isaya 14:11 Isaiah 14:11

Fahari yako imeshushwa hata kuzimu, Na sauti ya vinanda vyako; Funza wametandazwa chini yako, Na vidudu vinakufunika.

Isaya 14:12 Isaiah 14:12

Jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni, Ewe nyota ya alfajiri, mwana wa asubuhi! Jinsi ulivyokatwa kabisa, Ewe uliyewaangusha mataifa!

Isaya 14:13 Isaiah 14:13

Nawe ulisema moyoni mwako, Nitapanda mpaka mbinguni, Nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu; Nami nitaketi juu ya mlima wa mkutano, Katika pande za mwisho za kaskazini.

Isaya 14:14 Isaiah 14:14

Nitapaa kupita vimo vya mawingu, Nitafanana na yeye Aliye juu.

Isaya 14:15 Isaiah 14:15

Lakini utashushwa mpaka kuzimu; Mpaka pande za mwisho za shimo.

Isaya 14:16 Isaiah 14:16

Wao wakuonao watakukazia macho, Watakuangalia sana, wakisema, Je! Huyu ndiye aliyeitetemesha dunia, Huyu ndiye aliyetikisa falme;

Isaya 14:17 Isaiah 14:17

Aliyeufanya ulimwengu ukiwa, akaipindua miji yake; Asiyewafungua wafungwa wake waende kwao?

Isaya 14:18 Isaiah 14:18

Wafalme wote wa mataifa wamezikwa wote kwa heshima, Kila mmoja ndani ya nyumba yake mwenyewe;

Isaya 14:19 Isaiah 14:19

Bali wewe umetupwa mbali na kaburi lako, Kama chipukizi lililochukiza kabisa; Kama vazi la wale waliouawa, Wale waliochomwa kwa upanga, Wale washukao mpaka misingi ya shimo; Kama mzoga uliokanyagwa chini ya miguu.

Isaya 14:20 Isaiah 14:20

Hutaungamanishwa pamoja nao katika mazishi, Kwa maana umeiharibu nchi yako, Umewaua watu wako; Kizazi chao watendao uovu hakitatajwa milele.

Isaya 14:21 Isaiah 14:21

Fanyeni tayari machinjo kwa watoto wake. Kwa sababu ya uovu wa baba zao; Wasije wakainuka na kuitamalaki nchi, Na kuujaza miji uso wa ulimwengu.

Isaya 14:22 Isaiah 14:22

Nami nitainuka, nishindane nao; asema Bwana wa majeshi; na katika Babeli nitang'oa jina na mabaki, mwana na mjukuu; asema Bwana.

Isaya 14:23 Isaiah 14:23

Tena nitaifanya hiyo nchi kuwa makao ya nungu, na maziwa ya maji; nami nitaifagilia mbali kwa ufagio wa uharibifu; asema Bwana wa majeshi.

Isaya 14:24 Isaiah 14:24

Bwana wa majeshi ameapa, akisema, Hakika yangu kama vile vilivyoazimia, ndivyo itakavyokuwa; na kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyotokea;

Isaya 14:25 Isaiah 14:25

kwamba nitamvunja huyo Mwashuri vipande vipande katika nchi yangu, na juu ya mlima wangu nitamkanyaga chini ya miguu yangu; ndipo nira yake iliyo juu yao itakapoondoka, na mzigo wake utatoka mabegani mwao.

Isaya 14:26 Isaiah 14:26

Hilo ndilo kusudi lililokusudiwa duniani mwote, na huo ndio mkono ulionyoshwa juu ya mataifa yote.

Isaya 14:27 Isaiah 14:27

Maana Bwana wa majeshi amekusudia, naye ni nani atakayelibatili? Na mkono wake ulionyoshwa, ni nani atakayeugeuza nyuma?

Isaya 14:28 Isaiah 14:28

Ufunuo huu ulikuja mwaka ule alipokufa mfalme Ahazi.

Isaya 14:29 Isaiah 14:29

Usifurahi, Ee Ufilisti, pia wote, Kwa sababu fimbo ile iliyokupiga imevunjika; Maana katika shina la nyoka atatoka fira, Na uzao wake ni joka la moto arukaye

Isaya 14:30 Isaiah 14:30

Nao walio maskini kabisa watakula, Na wahitaji watajilaza salama; Nami nitatia shina lako kwa njaa, Na mabaki yako watauawa.

Isaya 14:31 Isaiah 14:31

Piga yowe, Ee lango; lia, Ee mji; Ee Ufilisti, pia wote, umeyeyuka kabisa; Maana moshi unakuja toka kaskazini, Wala hakuna atakayechelewa katika majeshi yake.

Isaya 14:32 Isaiah 14:32

Wajumbe wa taifa hilo waletewe jibu gani? Ya kuwa Bwana ameiweka misingi ya Sayuni, na ndani yake wale walioonewa katika watu wake wataona kimbilio.