Isaya Mlango 33 Isaiah

Isaya 33:1 Isaiah 33:1

Ole wako uharibuye ila hukuharibiwa, utendaye hila wala hukutendwa hila! Utakapokwisha kuharibu, utaharibiwa wewe; na utakapokwisha kutenda kwa hila, wao watakutenda hila wewe.

Isaya 33:2 Isaiah 33:2

Ee Bwana, uturehemu; tumekungoja wewe; uwe wewe mkono wetu kila asubuhi,na wokovu wetu pia wakati wa taabu.

Isaya 33:3 Isaiah 33:3

Kabila za watu wamekimbia wakisikia kelele za fujo; mataifa wametawanyika ulipojiinua nafsi yako.

Isaya 33:4 Isaiah 33:4

Na mateka yako yatakumbwa kama wadudu wakumbavyo, wataruka juu yake kama arukavyo nzige.

Isaya 33:5 Isaiah 33:5

Bwana ametukuka; kwa maana anakaa juu; amejaza Sayuni hukumu na haki.

Isaya 33:6 Isaiah 33:6

Nyakati zako zitakuwa nyakati za kukaa imara; za wokovu tele na hekima na maarifa; kumcha Bwana ni hazina yake ya akiba.

Isaya 33:7 Isaiah 33:7

Angalia, mashujaa wao wanalia nje, wajumbe wa amani wanalia kwa uchungu.

Isaya 33:8 Isaiah 33:8

Njia kuu zimeachwa, msafiri amekoma; ameyavunja maagano, ameidharau miji, hamjali mtu.

Isaya 33:9 Isaiah 33:9

Nchi inaomboleza, na kulegea; Lebanoni imetahayarika na kunyauka; Sharoni imekuwa kama jangwa; Bashani na Karmeli zimepukutika majani.

Isaya 33:10 Isaiah 33:10

Basi, sasa nitasimama; asema Bwana; sasa nitajiinua, sasa nitajitukuza.

Isaya 33:11 Isaiah 33:11

Ninyi mtachukua mimba ya makapi, mtazaa majani makavu; pumzi yenu ni moto utakaowateketeza wenyewe.

Isaya 33:12 Isaiah 33:12

Nao mataifa watakuwa kama kuchoma chokaa, kama miiba iliyokatika, iteketezwayo motoni.

Isaya 33:13 Isaiah 33:13

Sikieni, ninyi mlio mbali, niliyoyatenda; na ninyi mlio karibu, kirini uweza wangu.

Isaya 33:14 Isaiah 33:14

Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?

Isaya 33:15 Isaiah 33:15

Ni yeye aendaye kwa haki, anenaye maneno ya adili; ni yeye anayedharau faida ipatikanayo kwa dhuluma; akung'utaye mikono yake asipokee rushwa; azibaye masikio yake asisikie habari za damu; afumbaye macho yake asitazame uovu.

Isaya 33:16 Isaiah 33:16

Huyu ndiye atakayekaa juu; majabali ni ngome yake; atapewa chakula chake; maji yake hayatakoma.

Isaya 33:17 Isaiah 33:17

Macho yako yatamwona mfalme katika uzuri wake, yataona nchi iliyoenea sana.

Isaya 33:18 Isaiah 33:18

Moyo wako utatafakari hofu ile; Yuko wapi yeye aliyehesabu? Yuko wapi yeye aliyeupima ushuru? Yuko wapi yeye aliyeihesabu minara?

Isaya 33:19 Isaiah 33:19

Hutawaona watu wale wakali; watu wa maneno magumu usiyoweza kuyafahamu; wenye lugha ya kigeni usiyoweza kuelewa nayo.

Isaya 33:20 Isaiah 33:20

Angalia Sayuni, mji wa sikukuu zetu; macho yako yatauona Yerusalemu umekuwa kao la raha; hema isiyotanga-tanga; vigingi vyake havitang'olewa, wala kamba zake hazitakatika.

Isaya 33:21 Isaiah 33:21

Bali huko Bwana atakuwa pamoja nasi, mwenye adhama; mahali penye mito mipana na vijito, pasipopita mashua na makasia yake; wala hapana merikebu ya vita itakayopita hapo.

Isaya 33:22 Isaiah 33:22

Kwa maana Bwana ndiye mwamuzi wetu; Bwana ndiye mfanya sheria wetu; Bwana ndiye mfalme wetu; ndiye atakayetuokoa.

Isaya 33:23 Isaiah 33:23

Kamba zako zimelegea; hawakuweza kukaza sana shina la mlingoti wao; hawakuweza kulikunjua tanga; ndipo mapato ya mateka yaligawanywa, hata wachechemeao walipata mateka.

Isaya 33:24 Isaiah 33:24

Wala hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa; watu wakaao humo watasamehewa uovu wao.